WACHEZAJI WA ENGLAND WAMEPOTEA ULAYA, AJABU ZAIDI HATA ENGLAND KWENYEWE HAWAPO
Na Saleh Ally
UNAWEZA ukajiuliza kwani hawa Waingereza kutokea England wako wapi? Tatizo lao ni lipi hasa, maana hawaonekani tena Ulaya!
Miaka
mitano hadi kumi iliyopita, ilikuwa ni kitu cha kawaida kabisa kusikia
Timu ya Hispania au Italia ina mchezaji kutoka England ambaye anafanya
vizuri na timu hiyo.
Lakini
safari hii katika michuano ya Ulaya kuanzia msimu uliopita inaonekana
wachezaji kutoka England wamekuwa wakipotea katika timu mbalimbali
zinazofanya vizuri Ulaya.
Ajabu
zaidi, hadi katika timu zinazotokea England, bado hakuna nafasi kwa
wachezaji wanaotokea England hata kama timu zao zitafanya vizuri.
Mfano
mzuri ni huu, ukichukua timu nne zilizoingia nusu fainali ya Ligi ya
Mabingwa Ulaya msimu huu, utaona namna wachezaji kutoka England
wanavyozidi kupotea kwa maana ya ubora linapofikia suala la ubora katika
Bara la Ulaya.
Timu
ya kwanza ni Bayern Munich ya Ujerumani ambayo haina mchezaji hata
mmoja kutoka England. Kikosi hicho kimejaza Wajerumani, Wahispania,
Wafaransa, Wabrazil na wengine kutoka Uholanzi, Poland, Chile na
kwingineko.
Hatua
ya nusu fainali ni Top Four ya Ulaya. Timu nyingine iliyoingia ilikuwa
ni Atletico Madrid, nayo haina hata mchezaji mmoja kutoka England.
Badala yake Wahispania ni wengi zaidi wakifuatiwa na Wabrazil,
Waargentina, pia kutoka katika mataifa ya Ureno, Ghana, Slovenia na
mengineyo.
Timu
ya tatu ni Real Madrid, hawa pia hawana mchezaji anayetokea England.
Isipokuwa wana mchezaji kutoka Uingereza. Huenda ninaweza kufafanua
kidogo hapa.
Wales
ni sehemu ya Uingereza kama ilivyo England. Kawaida England imekuwa
ndiyo inatamba zaidi kwa ubora wa soka katika muunganiko wa nchi za
Uingereza yaani Great Britain.
Madrid zaidi ina wachezaji kutoka mataifa ya Hispania, Ureno, Ufaransa, Croatia, Wales, Ujerumani, Colombia na Costa Rica.
Sasa
labda twende kwa timu ya nne, hii ni Manchester City ya England.
Ilijitahidi sana ingawa imetolewa hatua hiyo ambayo ilikuwa ni mara yake
ya kwanza kufika.
Man
City katika kikosi chake cha timu ya wakubwa ina wachezaji wanne tu
kutoka England ambao ni Joe Hart, Richard Wright, Fabian Delph na Raheem
Sterling.
Katika
wachezaji hao watatu, katika mechi za Ligi ya Mabingwa mwenye uhakika
wa kuanza alikuwa mmoja tu, Hart ambaye ni kipa na angalau Sterling
amekuwa akipata nafasi ya kuingia.
Lakini Wright ambaye ni kipa na kiungo Delph, hawa maisha yao yalikuwa ni nje ya uwanja.
Timu
inayotokea England, ni mmoja tu tokea England mwenye uhakika wa kuanza
tena ni kipa! Wako wapi wachezaji kutoka nchi hiyo inayoelezwa ni
nyumbani kwa soka?
Angalia
Man City, katika mechi zake za Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa asilimia 95
inategemea wachezaji kutoka katika nchi za Argentina, Ufaransa,
Hispania, Ubelgiji, Brazil, Ivory Coast, Nigeria na kwingineko?
Majigambo ya watu hawa yako wapi na wapi walipokosea?
Wakati
wakina David Beckham, Michael Owen, Steve McManamann walifanya vizuri
wakiwa Madrid ambayo ilikuwa na wachezaji nyota kabisa duniani kama
Zinedine Zidane na Ronaldo na wakaonyesha ushindani.
Sasa
hakuna wachezaji bora wanaotokea England wenye uwezo wa juu wa
kushindana na wachezaji kutokea Hispania, Ufaransa na kwingineko
duniani.
Waingereza
wakiwa kwao walikuwa wakitamba zaidi na mfano mzuri ni Wayne Rooney.
Ikaonekana wanaibuka akina Danny Welbeck na wengineo lakini sasa wote
wamepotea. Vijana na walioonekana ni wakongwe.
Inaonekana
England imepoteza mwelekeo na sasa inaanza kutengeneza mastaa wapya
kama akina Harry Kane, Jamie Vardy na wengine wachache. Lakini hauwezi
kusema ina wachezaji wa kiwango cha juu duniani ambao unaweza kusikia
wanawaniwa na Real Madrid au Barcelona.
Lakini
bado katika timu nyingi kubwa ni nadra kusikia mchezaji wa England ni
tishio na gumzo hadi nje ya England. Sasa hakuna ubishi tena kuwa
England na Uingereza kwa ujumla wanatakiwa kufanya kazi ya ziada ili
warejee juu katika soka la dunia, la sivyo wataingia kwenye hofu ya
kupotea katika heshima ya ubora wa juu kisoka kama ilivyo hofu ya
kupotea kwa vifaru kwenye mbuga za wanyama. Maana England hawapo
England, hawapo Ulaya!





Post a Comment