Wanafunzi kurudi Loliondo kutetea ardhi yao
WANAFUNZI wa vyuo mbalimbali mkoani Arusha wanaotoka Tarafa ya
Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro wametangaza kuacha masomo ili warejee
vijijini kutetea ardhi ya wazee wao.
Wamefikia uamuzi huo kufuatia mgogoro wa ardhi unaoendelea katika Kata
ya Ololosokwani na tarafa nzima ya Loliondo baina ya wakazi wa maeneo
hayo na serikali.
Akisoma tamko la pamoja la wanafunzi jana jijini hapa, Mwenyekiti wa
wanafunzi hao Albert Selembo alisema kama vijana wanaotoka wilayani
Ngorongoro wamesikitishwa na uamuzi wa serikali juu ya ardhi yao
inayozidi kuporwa kila kukicha.
“Tumeona hatuna sababu ya kuendelea na masomo, ni bora turudi vijijini
ili kuungana na wazee wetu kutetea ardhi ya malisho ya mifugo yetu.
“Tunapinga kwa nguvu zetu zote serikali kumega ardhi katika eneo la
pori tengefu la Loliondo kwa kigezo cha uhifadhi wakati si kweli eneo
lile linamegwa kwa sababu ya maslahi ya mwekezaji,” alisema Selembo.
Tayari serikali imetangaza urekebishaji wa mipaka na ukubwa wa eneo la
pori tengefu la Loliondo kwa kuchukua kilomita za mraba 1,500 kati ya
4,000 ili kumaliza mgogoro unaotokana na muingiliano wa matumizi ya
ardhi.
Katibu wa umoja huo Flavian Massango anayesoma Chuo Kikuu cha Makumira
mkoani Arusha, alisema serikali inatumia jina la uhifadhi kwa kulaghai
ardhi hivyo mpango huo hautafanikiwa.
Alisema wao wakiwa wanazuoni wanaunga mkono maazimio yaliyotolewa na
Baraza la Malaigwanani (viongozi wa mila) pamoja na viongozi wa siasa,
ya kutoitambua Kampuni ya Uwekezaji ya Ottler (OBC) wilayani Ngorongoro.
Alisema azimio jingine wanaloliunga mkono ni la kuishitaki serikali Kwa uamuzi wake wa kunyang’anya wananchi ardhi yao.
“Tupo tayari kwa hali na mali kuitetea ardhi yetu na kuhakikisha
serikali haifanikiwi kwa namna yoyote, lakini tunapongeza uamuzi wa
viongozi ngazi ya shina, tawi, kijiji, kata na ubunge kujiuzulu,”
alisema Massango.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam hivi karibuni,
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamisi Kagasheki alitangaza
uamuzi wa serikali wa kuchukua eneo hilo.
Alisema pori tengefu kisheria ni eneo la serikali, lakini baadhi ya
vijiji wamelichukua na kulifanya lao huku wakiingia mikataba na kampuni
binafsi zinazofanya shughuli za uwindaji na utalii wa picha bila kufuata
taratibu.
“Serikali imeona tatizo la ardhi kwa wanavijiji Loliondo. Hata hivyo
nasisitiza sehemu ya vyanzo vya maji, mazalia ya wanyama na mapito ya
wanyama katu serikali haitakubali kuwapa wananchi,” alisema Kagasheki.
Alisema serikali ipo tayari kuangalia upya eneo kubwa la mwekezaji OBC
ili kuona jinsi linavyoweza kupunguzwa na wananchi wakapata maeneo ya
kufanyia shughuli zao na si kumfukuza mwekezaji huyo.

Post a Comment