ad

ad

WAKALA WA SHETANI - 12



MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
Waliichukua ile picha na kuitazama kwa muda na kugundua kumbe mbaya wao hakuwa akikaa porini kama alivyojinadi bali anakuwa anakaa kwenye kambi ile.
“Ha! Father ndiye huyu.”
“Mna uhakika?” Father Joe aliuliza macho yamemtoka pima.
SASA ENDELEA...
“Kwa asilimia mia moja.”
“Mmh! Mnataka kuniambia huyu mwanamke ni muuaji?” Father alishtuka.
“Ndiyo Father ameua watu wengi kijiji cha Nyasha na askari wenzetu wawili.”
“Lakini si ndiyo kijiji alichokuwa akiishia zamani kabla ya kukimbia kuokoa maisha ya mwanaye huyu mlemavu wa ngozi na kujikuta akimpoteza mumewe aliyeuawa na wana kijiji na kufanikiwa kukimbilia hapa tulipowahifadhi siku zote za maisha yao.”
“Ni kweli Father upo sawa maelezo yako na ya huyo mwanamke yapo sawa, aliahidi mbele yangu kuwa analipa kisasi na kama asiponyongwa baada ya kumkamata, aliapa hata akitoka mzee atahakikisha kijiji cha Nyasha kinabakia historia atakifagia chote,” alisema askari aliyemkamata Ng’wana Bupilipili.
“Mmh, kumbe ndiyo hivyo mbona mimi nilikuwa sijui!” Father alishtuka huku sister Marry naye akisikia habari ya kumshangaza.
“Basi Father yule mwanamke zaidi ya gaidi, ameua watu wengi kwa sumu ya dawa ya kuulia wadudu katika maji.”
“Dawa ya kuua wadudu ni dawa gani hiyo?”
“Kwa kauli yao nakubaliana nao Ng’wana Bupilipili anahusika, chumbani kwake chini ya godoro hiyo dawa nimeikuta zaidi ya paketi tatu” Sister Mary aliwaunga mkono.
“Mmh, kama ni hivyo yule mwanamke ni mbaya sana, nilikaa naye na kumweleza awasamehe na kumuachia Mungu na kunikubalia. Lakini kumbe alikuwa na siri yake nzito moyoni ambayo sote humu ndani tulikuwa hatujui,” Father Joe alisema kwa maskitiko.
“Kwa kuonesha huyu mwanamke ni mzoefu hii ni mara ya pili tunamkamata na kutoroka juzi tulimkamata lakini alifanikiwa kututoroka.”
“Mmh, sasa napata picha inawezekana siku hiyo ndiyo aliyokimbia na kuangukia mlango wa kuingilia getini na kudanganya alikimbizwa na mnyama mkali,” Father alitoa ushuhuda.
“Kwa usemi huo ni kweli kabisa, mmh! Mwanamke yule basi ni mzoefu kama ameweza kukaa hapa na kufanya mauaji bila mtu yeyote hapa kambini kujua ni mzoefu wa hali ya juu” Sister Mary alisema kwa maskitiko makubwa.
“Sasa atakuwa wapi?” Father Joe aliwauliza wale askari.
“Kwa kweli mpaka sasa hatufahamu kakimbilia wapi, kwa sababu mazingira ya kututoroka ni ya hali ya juu. Inawezekana aliisha pitia mafunzo fulani ya jeshi, si rahisi mtu wa kawaida akawa na uwezo wa kuyafanya vile hata kuweza kutembea porini peke yake hata kukimbia kwa umbali mrefu.”
“Sasa mtafanya nini?”
“Tutaondoka na picha hii ambayo tutaiweka katika vyombo vya habari lazima atakamatwa tu.”
“Lakini nina imani kama ni tabia yake ya kurudi kambini basi lazima atarudi na sisi tuitawajulisha mara moja,” Father Joe alitoa wazo.
“Mtatusaidia sana.”
Walikubaliana wamuache mtoto Kusekwa ambaye ni mlemavu wa ngozi na kuamua kuendelea kumsaka Ngw’ana Bupilipili.
******
Ng’wana Bupilipili aliposhtuka alijikuta amelala kwenye kitanda kilichomuashilia pale ni hospital. Alijiuliza pale ni wapi na amefikaje, alijikuta akichanganyikiwa. Alipotaka kuamka mwili ulikuwa hauna nguvu na kumfanya arudi kulala kitandani.
Akiwa bado amejilaza na maswali lukuki kichwani mlango ulifunguliwa kwa ghafla, Ng’wana Bupilipili alifumba macho kwa haraka na kutulia tuli kitandani kusikilizia aliyeingia ni nani.
“Itakuwa amepata nafuu,” ilikuwa sauti ya kiume.
“Ni kweli, ilionesha alitumia nguvu nyingi sana pia mwili umepungukiwa maji.”
“Atakuwa anatoka wapi?”
“Hilo swali tumsubiri aamke mwenyewe.”
“Kwa hiyo tumuache alale?”
“Hapana mshitue aamke ili apewe uji wa maziwa na baadaye chakula aweze kupata nguvu, zaidi ya hayo hana tatizo kubwa.”
Baada ya muda Ng’wana Bupilipili alisikia akitikiswa taratibu huku akiitwa.
“Mama mdogo...Mama mdogo.”
“Mmh,” Ng’wana Bupilipili aliitikia kama yupo usingizini.
“Dakta anaamka.”
“Muamshe kabisa kisha fanya nilivyo kueleza, mimi nipo ofisini taarifa zingine utaniletea.”
“Sawa Dokta.”
Yote Ng’wana Bupilipili aliyasikia na kuamini sehemu aliyokuwepo ni salama kwake. Alipoitwa mara ya pili aliitikia huku akifumbua macho ya kumuona muunguzi mbele yake.
“Pole,” muuguzi alisema kwa sauti ya upole.
“Asante.”
“Unajisikiaje?”
“Mwili hauna nguvu.”
“Basi amka upate uji kisha chakula utajisikia vizuri.”
Ngw’ana Bupilipili aliamka kitandani kwa msaada wa muuguzi na kukaa kitako, muuguzi alitembea naye akiwa amempa msaada wa kumshika mkono hadi chumba cha chakula.
Alimketisha kwenye kiti na kumfuatia uji wa maziwa ambao aliunywa wote. Baada ya kunywa uji alijikuta akitokwa na jasho jingi, muuguzi aliyetambulika kwa jina la Sabina alimuonesha bafuni ambako alijimwagia maji na kupata nguvu.
Alirudi naye chumba cha chakula na kumpatia chakula ambacho nacho alikikila chote kuonesha alikuwa na njaa kali.
Baada ya kula alirudishwa wodini ili apumzike kabla ya kuonana na mganga mkuu. Baada ya nusu saa alifuatwa na muuguzi kupelekwa kwa mganga mkuu. Ng’wana Bupilipili aliongozana na yule muuguzi akijua lazima kuna maswali ya kuulizwa juu ya kuwepo pale na katokea wapi.
Aliingizwa katika ofisi ambayo haikutofautiana na Father Joe, pia mganga mkuu alikuwa mzungu. Alipowaona wanaingia aliacha kazi zake na kuwakaribisha.
“Ooh, karibuni.”
“Asante,” alijibu Ng’wana Bupilipili.
“Pole na matatizo.”
“Asante.”
“Unaitwa nani?”
“Malimi,” Ng’wana Bupilipili alidanganya jina.
“Unatokea wapi?”
“Kijiji cha Sanza.”
“Kijiji cha Sanza mpaka huku umefikaje?”
“Kulitokea vita ya familia ambayo ilifanya wanakijiji tutawanyike na kukimbia kusikojulikana kuokoa maisha yetu.”
“Umetumia muda gani kufika barabara kuu?”
“Siku tatu.”
“Mmh, pole sana.”
“Asante.”
“Una mpango gani?”
“Kwa kweli mpaka sasa sijajua niende wapi hata hapa nimefika sijui ni wapi?”
“Hapa ni Sangema, je, upo tayari kurudi kijijini kwako?”
“Bora nife lakini sipo tayari kurudi huko.”
“Una familia?”
“Yote imeteketea na vita.”
“Pole sana.”
“Asante.”
“Basi mama, sijui unaitwa nani?”
“Baba si nimekueleza naitwa Malimi.”
“Ooh samahani, sasa mama Malimi itaishi hapa kwa vile kituo hiki kinatunza watu wenye shida.”
“Nashukuru baba yangu asanteni kwa moyo wenu wa kujitolea Mungu awazidishie.”
“Amen.”
“Sabina kamuoneshe chumba apumzike mambo mengine atapangiwa kesho.”
Sabina alimchukua Ng’wana Bupilipili na kwenda kumuonesha chumba cha kupumzika.
MIAKA SABA BAADAYE
Kuseka aliendelea kukua kufikia hatua ya kwenda shule ya msingi katika kambi aliyoachwa huku akiendelea na masomo ya awali ya chekechea na kuandaliwa kwenda shule ya msingi. Lakini kabla hajaanza shule ya msingi alitokea mzungu mmoja aliyekuwa akimiliki machimbo ya dhahabu.
Mzungu huyo aliyejulikana kwa jina la John Brown, Mr Brown alikuwa na mgodi mkubwa uliokuwa na wachimbaji wengi sana. Kutokana na uwezo wake wa kipesa aliweza kuwasaidia wana kijiji waliokuwa jirani na machimbo yale. Alijenga zahanati na miradi ya maji na umeme ambayo ilikuwa msaada tosha kwa wana kijiji ambao walifaidika na machimbo yake.
Mr Brown ndani ya eneo lake la machimbo alijenga shule kwa ajili ya watoto kuanzia miaka miwili na kuendelea. Sifa zake zilizagaa kila kona ya nchi na kuifanya serikali impunguzie kodi pamoja na kumpa misamaha katika vitu alivyokuwa akiingiza nchini.
Kingine ambacho kiliungwa mkono na wengi ilikuwa kuwachukua walemavu wa ngozi albino ambao walianza kusoma pale na baadaye kuwapeleka nje ya nchi kwa masomo zaidi.
Kusekwa naye alichukuliwa na Mr Brown na kuanza masomo yake ya darasa la kwanza. Baada ya miezi miwili Kusekwa alipata nafasi ya kusafiri kwenda Ulaya kimasomo.
Aliandaliwa sherehe kama wenzake waliotangulia na safari yake ilikuwa siku ya pili alfajiri.
Kama kawaida Kusekwa alikwenda kulala kusubiri asubuhi asafiri, na siku hiyo alilala sehemu tofauti na anapolala siku zote. Majira ya saa nane za usiku alishtushwa na watu walioingia chumbani kwake wakiwa wameziba nyuso zao kabla hajajua nini kinaendelea alikuvamiwa na kuzibwa mdomo kisha alibebwa juu juu na kupelekwa asikokujua.
Kusekwa alibakia na mawazo wale ni kina nani na mbona wamembeba vile au ndio mtindo wa wote wanaosafiri kwenda nje. Alijifikiria kama wangekuwa ni majambazi au watu wabaya wamepitia wapi mpaka kuingia kule chumbani kwenye kambi yenye ulinzi mkali.
Alijikuta akiwa njia panda huku wale watu wakimpeleka kimya kimya bila kuongea. Baada ya muda aliingizwa kwenye chumba kimoja ambacho kilikuwa na kiti na kukarishwa pale. Baada ya kuwekwa mtu mmoja aliwasha swichi, mikono na miguu ya Kusekwa ilishikiliwa na vyuma.
Kusekwa alizidi kushangaa watu wale kumfanya vile walikuwa na shida gani tena walionesha sio wema kwake. Baada ya kubanwa na vyuma mashine iliwashwa ili kumkata viungo.
Itaendelea

No comments

Powered by Blogger.