WAKALA WA SHETANI - 11

MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
“Mmh! Vyombo vya sheria kwa vile wamekufa wao, mbona vifo vya watoto albino hamkuwahi kuja hata siku moja ila hivi ndio mmetengeneza mtego wa kuninasa, ndio maana nikasema nipelekeni mkani.ni..ni..ni.. Haaa!”
Ngwana Bupilipili alishika chini ya titi la mkono wa kushoto baada ya kusikia mchomo mkali kwa ndani kama kumepasulika.
Maumivu yalikuwa makali na kuhisi kama mbavu zinagusana. Alipiga kelele za maumivu na kuanguka chini akiwa amepoteza fahamu.
SASA ENDELEA...
****
Ng’wana Bupilipili baada ya kurudiwa na fahamu alipofumbua macho alijiona yupo ndani ya hema amelazwa chini kwenye turubai lililokuwa limetandikwa chini na pembeni yake alikuwepo mwanaye Kusekwa ambaye alikuwa amepitiwa usingizi.
Alijikuta akijiuliza pale ni wapi na amefikaje, alimuangalia mwanaye ambaye alikuwa amelala huku akioneka yupo katika hali ya kawaida. Ili kuhakikisha mwanaye ni mzima aliweka sikio kifuani ambako alimsikia akihewa vizuri.
Akiwa bado anamuangalia vizuri mwanaye alishtushwa na sauti za watu waliokuwa wakisogea kwenye hema lile huku wakizungumza.
“Huenda kaisha pata fahamu ngoja tukamuangalie, yule mwanamke simuamini kabisa.”
“Lakini mbona sifa za yule mwanamke hazilingani naye huenda kuna wahusika wakuu na yeye ni mtu wa kutumwa tu,” askari mmoja alisikika akisema.
Ngw’ana Bupilipili alipowasikia wamekaribia alirudi sehemu aliyokuwa amelala na kujilaza kama kwamba hajarudiwa na fahamu kwa kujitahidi kuhema kwa taratibu sana. Askari wale waliingia hadi ndani na kumkuta amelala hata kuhema kwake haikuwa kwa kawaida.
“Bado hajaamka twende zetu,” alisema mmoja baada kuwa na uhakika mtuhumiwa bado amelala.
“Sasa tutaondoka saa ngapi?”
“Mkuu amesema tumsikilizie kwa muda zaidi ya hapo tutambeba na kuondoka naye.”
“Unajua bado siamini kama ni yeye ambaye katupatisha taabu ya miezi zaidi ya sita.”
“John anasema yule mama kwa macho haoneshi hatari yake kwani alisema alifanya vile kulipa kisasi cha mume na mtoto wake aliyeuawa na wana kijiji kwa imani za kishirikina.”
“Mmh! Basi ni kiboko, ni wanawake wachache wenye moyo wa ujasiri kama yeye.”
“Ndio maana ulinzi mkuu amesema uwe mkali.”
“Sasa unataka kuniambia huyu mwanamke na mtoto wake walikuwa wanaishi wapi na hii mvua?”
“Kutokana na maelezo ya John alisema anaishi porini kama mnyama.”
“Utani huo kwa muda gani?”
“Huu ni mwezi wa saba sasa.”
“My God, alikuwa anakula nini na kulala wapi?”
“Hapo ndipo unatakiwa ujiulize juu ya uwezo wa kikomandoo wa huyu mwanamke.”
“Au ameisha wahi kupitia jeshi?”
“Hilo kwa kweli sijui, ila mwanamke huyu kama ni kweli ni zaidi ya mwanajeshi wa kawaida.”
“Ina maana yupo peke yake?”
“Kutokana na maelezo inaonekana aliondoka kijiji pale baada ya kuuawa mtoto na mumewe na kuamua kulipa kisasi kwa mkono wake.”
“Lakini mkuu si amesema lazima aseme ukweli au ateswe sana, kwa mateso ya bosi hata awe komandoo lazima atasema.”
“Ngoja tuone.”
“Mmh, twende tupeleke taarifa.”
Ng’wana Bupilipili aliwasikia wakiondoka, alitulia kwa muda kisha alijinyanyua taratibu alipolala na kunyata hadi mlango wa kutokea. Alichungulia kwa chati nje, aliwaona askari wawili waliokuwa juu ya gogo la mti wakicheza karata wakiwa wamempa mgongo.
Aliangalia upande mwingine aliwaona wengine kwa mbali wakinywa kinywaji kikali ilionesha kukata baridi. Upande wa pili kulikuwa na mbuga ambayo ilikuwa ni vigumu mtu kutoka nje ya hema bila kuonekana.
Akiwa na wazo la kutoroka kwa kuamini akifikishwa mbele ya vyombo vya sheria lazima hukumu itamuumiza yeye. Aliamini anaweza kupita kwa mwendo wa kunyata nyuma ya wale askari. Lakini wasi wasi wake mkubwa ulikuwa kama ataonekana basi atajiweka katika wakati mgumu sana.
Aliamini ukweli wowote hautaaminiwa zaidi ya kuteswa ili kulazimishwa asema asichokijua. Aliamini njia nyepesi ni kutoroka na kupania kama atafanikiwa kutoroka asingesimama kwa siku mbili kutembea pori kwa pori mpaka atakapo tokea.
Akiwa bado anatakakali jinsi ya kutoka ndani ya hema lile, macho yake yalitua kwenye uwazi uliokuwa upande wa chini ya hema. Wazo la haraka lilikuwa kupitia katika upenyo ule ambao hakukuwa na ulinzi wowote, wazo la kumbeba mtoto wake aliliweka pembeni kwani aliamini kutokana na kauli za wale watu mwanae yupo salama.
Alimchukua mtoto wake na kumkumbatia kwa muda huku machozi yakimtoka, kwa sauti ya chini alimueleza mtoto wake.
“Kusekwa baba nakupenda sana mtoto wangu, nina imani mpaka sasa upo katika mikono salama ila mama yako hatari nzito ipo mbele yangu. Nakuacha baba ili nami niokoe maisha yangu bila hivyo kitanzi kipo shingoni kwangu.
“Kusekwa baba, mama yako sijui niendako japo mtoto usiyejua lolote lakini niombee mama yako nitoke salama na safari yangu iwe yenye muongozo mwema na Mungu aniongoze nifike kwenye mikono salama.
“Nakupenda mwanangu nakupenda sana na Mungu akulinde kwa jambo lolote baya, Mungu akipenda tutaonana siku yoyote kama bado tunaishi na kama sio duniani basi kwenye ufalme wake wa milele.”
Baada ya maombi yaliyomtoa machozi huku moyo ukimuuma kutengana na mwanaye kipenzi kama angefanikiwa kuwatoroka. Alimrudisha mwanaye kwenye turubai na kusimama kwa muda akimuangalia mwanaye huku moyo ukizidi kumuuma sana.
Alishika mikono kifuani huku akilia aligeuka na kupiga magoti kupekenyua sehemu iliyokuwa na uwazi kwa chini na kutoka kwa kutambaa. Baada ya kufanikiwa kutoka bila kuonekana, aliingia porini kwa mwendo wa kuinama na kunyata.
Ilifikia hatua ya kutembelea tumbo kama komandoo aliyekuwa ikivamia kambi, baada ya kufanikiwa kufika mbali kidogo ambako aliamini kabisa hawezi kuonekana alitimua mbio kukata pori bila kujua hatari atakayokutana nayo mbele.
Alikimbia kwa mwendo wa mbio za marathoni bila kupumzika kwa kuamini uwezo wake wa kukimbia bila kupumzika ndio utakao okoa maisha yake. Alikimbia kwa masaa matatu bila kupumzika na kujikuta ametokea kwenye barabara kubwa ya lami.
Alisimama na kuanza kuhema kwa kasi kitu kilichomfanya ahisi kizunguzungu bila kupenda alianguka chini na kupoteza fahamu.
*******
Baada ya muda kukatika mkuu wa kikosi maalumu cha kumsaka muuaji wa kijiji cha Nyasha alimtuma askari akamuangalie tena kama Ng’wana Bupilipili kama ameamka ili kama bado amelala wambebe na kuondoka naye.
Askari alikwenda hadi kwenye hema kuangalia kama mtuhumiwa wao ameamka. Alikwenda hadi ndani ya hema lakini ilikuwa ajabu ndani ya hema hakukuwa na mtu yeyote zaidi ya mtoto aliyekuwa bado amelala. Ilibidi awaulize wenzake waliokuwa wamezama kwenye karata.
“Oyaa washikaji yule mwanamke yupo wapi?”
“Si amelala humo ndani.”
“Mbona simuoni?”
“Sele hebu acha utani, yupo humo ndani.”
“Kweli washikaji yupo mtoto peke yake.”
Wale askari waliokuwa wakicheza karata walinyanyuka na kwenda hadi ndani ambako walikuta patupu. Walijikuta wakichanganyikiwa na kuanza msako kuzungaka hema lakini hakukuwa na mtu yoyote eneo lile.
Walijikuta wakipagawa na kujiuliza watamwambia nini mkuu wao aliyewapa jukumu la kumlinda yule mwanamke aliyeonekana dhaifu mbele ya macho ya watu lakini ni hatari kwa vitendo.
Waliotumwa walirudisha taarifa za kutoweka kwa Ng’wana Bupilipili na kumtelekeza mtoto. Sherehe yote ya kumpata mtuhumiwa iliyeyuka na kuamuliwa kufanya msako wa haraka.
Kila askari alitawanyika kwenda anapopajua ili mradi arudi na mtuhumiwa. Askari wote walitawanyika huku waliofanya makosa ya kizembe wakichanganyikwa zaidi kwa kukimbia ovyo bila kujua wanakwenda wapi.
Askari wengine walibakia pamoja na mkuu wao kwa ajili ya kulinda usalama wa mtoto. Msako ulifanyika mpaka usiku wa manane lakini hawakupata chochote, mkuu wa operesheni ile aliwaeleza waliofanya uzembe wahakikishe mtuhumiwa anapatikana bila hivyo wasirudi.
Hawakupata muda wa kupumzika walirudi kufanya msako. Waliona hawawezi kukaa na yule mtoto aliyeanza kumlilia mama yake. Kwa vile kituo cha kulea watu wanaoishi katika mazingira magumu kilikuwa karibu, siku ya pili walimchukua na kumpeleka katika kituo kile.
Walipofika mkuu wa kikosi cha kumsaka muuaji alijitambulisha kwa Father Joe, baada ya kujitambulisha walimueleza sababu ya kuwepo pale.
Father alikubali kumpokea mtoto yule na kumlea, lakini alishangaa kumuona ni mtoto wanaye mfahamu.
“Ha! Huyu mtoto si wa hapahapa kambini?”
“Hapana Father huyu tumemuokota porini na mama yake,” alijibu mkuu wa operesheni.
“Huyu wa hapahapa kambini na mama yake anakaa hapahapa kambini na jina lake anaitwa Kusekwa.”
“Hapana huyu mama yake ni muuaji tena amekimbia baada ya kumkamata na kumtelekeza huyu mtoto,” mkuu wa opereshani alizidi kubisha.
“Hapana mama yake ni mkimbizi wa kijiji cha Nyasa si muuaji,” Father Joe alimtetea Ng’wana Bupilipili.
“Father hebu tuitie huyo mwanamke tumuone na amtambue mtoto wake,” mkuu wa operesheni alimuomba Father Joe.
Father Joe alinyanyua simu na kumwita Sister mmoja, baada ya muda mfupi Sister Mary aliingia.
“Sister Mary naomba uniitie Ng’wana Bupilipili.”
“Sawa Father,” Sister aligeuka na kuondoka.
Baada ya muda alirudi akiwa peke yake.
“Vipi yupo wapi?”
“Hatupo Father.”
“Atakuwa amekwenda wapi?”
“Kwa kweli jirani zake hawana taarifa zozote mpaka jana usiku wanakwenda kulala walikuwa wote.”
“Chumba chake kina vitu vyake?”
“Ngoja nikahakikishe,” Sister alisema huku akiondoka.
Sister alitoka tena na kwenda chumba cha Ng’wana Bupilipili ambako hakukuwa na mabadiliko yoyote. Alirudi na kutoa taarifa, baada ya kusikia vile mkuu wa operesheni aliuliza.
“Kwani huyo mnayemsema mnayo picha yake?”
“Ndiyo.”
“Basi tupeni tuiangalie kama siyo yeye tuondoke tukaendelee na msako wetu.”
Father Joe alifunua faili lililokuwa na picha za watu wote waliokuwa kwenye kambi ile. Alichambua picha mojamoja kwa umakini mpaka akaipata picha nusu ya Ng’wana Bupilipili.
“Picha yake hii hapa,” Father Joe alisema huku aliwakabidhi.
Waliichukua ile picha na kuitazama kwa muda na kugundua kumbe mbaya wao hakuwa akikaa porini kama alivyojinadi bali anakuwa anakaa kwenye kambi ile.
“Ha! Father ndiye huyu.”
“Mna uhakika?” Father Joe aliuliza macho yamemtoka pima.
Itaendelea
Post a Comment