Watanzania wengine 13 wameangamia mkoani Arusha kwa kufukiwa na kifusi.
WAKATI shughuli ya uopoaji wa watu waliokufa kwa kuporomokewa na
ghorofa jijini Dar es Salaam zikimalizika kwa miili 36 kupatikana,
Watanzania wengine 13 wameangamia mkoani Arusha kwa kufukiwa na kifusi
kwenye machimbo.
Tukio hilo lilitokea jana jijini hapa, saa 5 asubuhi eneo la Moshono
kwenye machimbo ya kokoto ambayo hata hivyo hayaruhusiwi, kufanywa
shughuli hiyo, baada ya kumeguka kwa udongo uliosababishwa na mvua
zinazoendelea kunyesha.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alisema kuwa shughuli ya
uokoaji ilikuwa imekamilika jana jioni ambapo maiti 13 ziliopolewa na
watu wengine wawili walinusurika.
Hata hivyo, vifaa vya uokoaji navyo vilikuwa tatizo kutokana na zana
duni zilizokuwa zikitumika katika utafutaji wachimbaji wengine
wanodhaniwa kuwepo wakati ajali hiyo ikitokea katika machimbo hayo
maarufu kama Moivaro Tanganyika Packers.
Anadaiwa kuwa wachimbaji hao walikuwa wakichimba moramu hiyo na
kuiweka katika malori mawili aina ya Fuso na Scania na wakati
wakiendelea na kazi ndipo kifusi hicho kilipowafunika.
Baada ya tukio hilo, wananchi wakishirikiana na vyombo vya usalama
walijaribu kuokoa watu waliofukiwa ambapo miili iliyoopolewa
imehifadhiwa katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru.
Mulongo aliwataja waliokufa kuwa ni Kibobori Mwenda, Kababuu Luwasele,
Bariki Leseriani, Sauli Raphaeli, Hassan Hamis, Alex Maliaki, Gerald
Lukakijata na Japhet Jivaina.
Wengine ni Bernard Masai, Gerald Jacob, Christopher Gerald, Fredy Losiriani na Julius Peter.
Wachimbaji wawili walionusurika majina yao hayakuweza kupatikana mara moja.
Waliokufa Dar 36
Shughuli ya uopoaji wa miili ya watu waliofukiwa na kifusi baada ya
jengo la ghorofa 16 kuporomoka imekamilika huku idadi yao ikifikia 36.
Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio jana, Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, alisema kazi hiyo ilihusisha
vikosi mbalimbali kwa muda wa siku nne mfululizo usiku na mchana bila
kupumzika.
“Hata hivyo shukurani hizo na kuhitimisha huko vilipaswa kufanywa na
Rais Jakaya Kikwete, lakini kutokana Rais kupatwa na dharura ameshindwa
kuwa nasi hivyo, amemuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk.
Emmanuele Nchimbi, kuwasilisha salaam zake,” alisema Sadik.
Alisema katika uokoaji huo, awali wananchi wa kawaida walikuwa
wakishindwa kutofautisha, idadi ya miili kutokana na kutotambua tofauti
ya miili na viungo vyake kama vile mikono, miguu na vichwa vya binadamu
vilivyokuwa vikitolewa katika vifusi vya jengo hilo.
“Awali tuliweza kukagua viungo kadhaa, ikiwemo vichwa viwili, miguu
miwili na mikono miwili, kitaalamu ilipokaguliwa na madaktari wa
Hospitali ya Muhimbili kisha kuunganisha viwiliwili, tulipata miili
miwili,” alisema.
Alifafanua kuwa watu walioopolewa wakiwa na miili kamili ni 34 lakini
idadi kamili ilifikia 36 baada ya kuunganisha viungo vya miili miwili.
Sadik alisema miongoni mwa maiti hao, yumo mwanamke mmoja na kwamba
hadi sasa majeruhi waliobaki hospitalini ni wanne wakiwemo watoto wawili
waliokuwa wakicheza mpira chini ya jengo hilo kabla ya ajali.
Alisema kuwa uchunguzi utaenda sambamba na kuwatumia watu wa bodi ya
usajili wa wahandisi na makandarasi pamoja na wengine ambao ni
wanajeshi, jeshi la polisi, mainjinia kutoka tawala za mikoa na
wataalumu wengine wawili.
Mkuu huyo alibainisha kuwa kamati hiyo itachunguza jengo lingine
ambalo lilikuwa likihofiwa kuanguka wakati kazi ya kuondoa kifusi
ikifanyika kutokana na kampuni iliyojenga kuwa ile ile na kwamba ikiwa
litakutwa halina ubora litabomolewa.
Akizungumza kwa niaba ya Rais, Dk. Nchimbi alisema kiongozi huyo
alikuwa awepo hapo kutoa shukurani zake kwa kila mtu aliyehusika katika
shughuli hiyo ya uokoaji wa watu hao waliokumbwa na janga hilo lakini
ikashindikana.
Hata hivyo, Nchimbi alisema kuwa Rais amepamga siku ya Aprili 8
kukutana na wale wote waliojitolea kwa hali na mali katika kazi ya
uokoaji tangu Machi 29 mwaka huu, kwa ajili ya kula nao chakula cha
mchana.
Katika hatua nyingine, mmoja wa wafanyakazi wa Kampuni ya Khoja Shia
Ithinasheri, Ali Walji, aliwataka wananchi kuacha tabia ya kukusanyika
katika matukio kama hayo huku wakiwa hawana kazi maalumu.
Alisema wananchi hao wamekuwa chanzo cha kuchelewesha kazi ya uokoaji,
huku wakisambaza habari ambazo zimekuwa zikiwapotosha watu wengine
walio mbali na tukio.
Naye Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman
Kova, alisema kuwa mpaka sasa watu tisa wanashikiliwa na polisi kwa
mahojiano na watakaopatikana na hatia watapandishwa kizimbani mapema
wiki hii.
Wanaoshikiliwa ni Ogare Salu, Godluck Mbaga, Ibrahim Kisocky, Vedasto
Ferdnand mkazi wa Kimara, Raza Damji, Ally Damji na wengineo.
Habari hii imeandaliwa na Ramadhan Siwayombe, Happiness Mnale, Shehe Semtawa na Andrew Chale

Post a Comment