ad

ad

Nyaraka za Waislamu, Wakristo zamtisha JK

RAIS Jakaya Kikwete amesema kuwa nyaraka na kauli kali kali zinazotolewa na viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu zimelifikisha taifa mahali ambapo kama viongozi na waumini wa dini hizi hawatakubali kubadili muelekeo wa sasa, nchi inakoelekea ni kubaya.


Katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi kwa wananchi, Rais alisema licha ya kulizungumzia suala hilo mara kadhaa lakini kutokana na nyaraka na kauli hizo anashawishika kusema tena.


“Nyaraka na kauli hizo zina mambo mawili makuu. Kwanza, kwamba kila upande unatuhumu, kushutumu na kulaumu upande mwingine kwa kufanya vitendo viovu dhidi ya dini yake,” alisema.


Alisema kuwa kauli na mihadhara ya kudhalilisha dini za wengine, kunajisi vitabu vitakatifu, kuchoma moto nyumba za ibada, mzozo kuhusu nani achinje na kuuawa kwa viongozi wa dini ni baadhi ya mambo yanayotolewa mifano.


“Jambo la tatu ninalopenda kuzungumza nanyi leo ni uhusiano wa Waislamu na Wakristo nchini. Jambo hili nimeshalizungumzia mara kadhaa siku za nyuma, lakini nalazimika kulisemea tena kutokana na hali ilivyo sasa,” aliongeza.

Alisema Tanzania itaacha kuwa kisiwa cha amani na kuingia katika orodha ya nchi zenye migogoro na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe.


Aidha Wakristo wanateswa na viongozi wao kuuawa na Waislamu, lakini serikali haichukui hatua. Kwa ajili hiyo wanadai kuwa serikali imeshindwa kulinda uhai wa raia wake. Wanasema pia kwamba serikali inapendelea upande wa Waislamu.

“Waislamu nao wanadai kuwa kitabu chao kitakatifu, yaani Quran Tukufu, kinadhalilishwa kwa kuchanwa, kuchomwa moto na kukojolewa na Wakristo na serikali haichukui hatua yoyote ya maana,” alisema.


Alisema kuwa yeye binafsi anashutumiwa kuwa anapendelea kushiriki zaidi kwenye shughuli za Wakristo kuliko za Waislamu kama vile harambee za kujenga makanisa na shule za makanisa.

“Naambiwa kuwa mwepesi kushiriki maziko ya maaskofu kuliko masheikh wanapofariki. Ipo misikiti mitatu hapa Dar es Salaam wamenisomea itikafu nife. Katika itikafu hiyo wamewajumuisha Inspekta Jenerali wa Polisi, Saidi Mwema, na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Ndugu Suleiman Kova.
Powered by Blogger.