ad

ad

KIFO CHA MTU ASIYE NA HATIA - 07



Alisimama wima mbele ya askari magereza wa kike, mtoto wake Alicia akiwa mgongoni, mtoto huyo hakuelewa kitu chochote kilichoendelea aliendelea kulala mgongoni kwa mamaye. Baada ya kujieleza kwa muda mrefu akimbembeleza askari magereza amwitie Prosper ili aonane naye kabla ya kifo chake hatimaye askari alilainika na   kuanza kutembea kuondoka eneo hilo  na kuingia ndani ya gereza.
Hakurudi mpaka dakika kama kumi na tano hivi baadaye, askari huyo aliporejea  mbele yake  akiwepo Prosper! Tayari alishavalishwa nguo za wafungwa na alionekana kukonda  sana.
 Prosper alionekana kutoyaamini macho yake alipomwona Belinda! Alitaka kukimbia kwenda upande wa pili kumkumbatia lakini alizuiliwa na nondo nzito zilizotenganisha ndani na nje ya gereza! Ziliwekwa maalum kuwazuia wafungwa kutoroka.
“Afande nifungulie basi nisalimiane na mke wangu kwa karibu zaidi!”
“Haiwezekani hata kidogo Prosper kwanza si ruhusa  leo wafungwa kuonwa   nimewafanyia upendeleo  vinginevyo ningeweza kukataa  kwanza haraka kabla mkuu wa gereza hajaja mnasikia?” Askari magereza aliongea kwa msisitizo.
Hakuna aliyemjibu kitu afande bali Prosper alisogea  karibu na uzio  wa nondo, Belinda nae alifanya vivyo hivyo mpaka wakakaribiana kabisa na kupenyeza midomo yao katikati ya  nondo na kuanza kupigana mabusu mdomoni mbele ya askari bila kuogopa wala kuona aibu.
Ghafla kabla hawajasema lolote hata kusalimiana wote walianza kudondosha machozi na baadaye kulia kwa sauti, walionekana kuwa na uchungu mkubwa mioyoni mwao! Waliangaliana na kukumbuka mambo mengi yaliyotokea katika maisha yao tangu walipokutana mara ya kwanza shuleni, yalikuwa ni mateso makubwa mno waliyoyapitia na bado walikuwa wakiendelea kuteseka.
Waliendelea kulia kwa kwikwi kiasi kwamba hakuna mtu aliyeweza kumwambia mwenzake chochote  hadi Prosper alipoanza kuvutwa na askari magereza kurudishwa gerezani! Machozi yalimbubujika Belinda kwa wingi, alimwonea huruma sana Prosper  na kabla hajaingizwa ndani aligeuka nyuma na kuwaanglia Belinda na mtoto wake, roho   ilimuuma sana na alitamani mambo yangekuwa tofauti  na ilivyokuwa, ndani ya nafsi yake Prosper alijilaumu kwa uamuzi wake wa kuyakiri mauaji ambayo hakuyatenda jambo ambalo hata Belinda hakulifahamu.
Mtu aliyekiri mauaji hayo ili amuokoe kutoka gerezani,yaani  mama yake   tayari alikuwa ni marehemu na dada zake nao walishamtelekeza gerezani baada ya kutoka gerezani na yeye kuingia!
“Nakupenda Belinda, ahsante sana kwa kuja tena, nisamehe kwa kila kosa nililoliyafanya najua sina maisha marefu duniani, kwa sababu watu wenye virusi hufa upesi sana gerezani isitoshe nimeshahukumiwa kifo tayari, namuonea huruma sana mwanangu kwa sababu hataishi kuja kuniona mimi baba yake! Tafadhali Belinda mtunze vizuri mtoto wetu Alicia lakini usije kumwambia niliua!” Alisema Prosper huku askari magereza akisubiri amalizie.
“Prosper  elewa ninakupenda sana na nimekwishakukusamehe makosa yako yote  na nimesikitika kujua unakufa na kuniacha mimi!” Alisema Belinda akijua hiyo ndiyo ilikuwa mara ya mwisho kuonana na Prosper kwani angenyongwa kama hukumu ilivyotolewa.
Pamoja na kujua Prosper alikuwa na virusi vya Ukimwi kama ambavyo yeye Belinda aliamini kuvipata kutoka kwake na yeye kuvipeleka kwa mtoto wao Alicia, bado Belinda hakuwa tayari kukubali Prosper anyongwe, alimpenda mno na hakutaka kumpoteza! Alitaka waishi pamoja mpaka watakapozidiwa na kufa kwa Ukimwi ikiwezekana siku moja wote watatu.
“Sipendi Prosper anyongwe na ningekuwa na uwezo wa kuliepusha hili ningefanya, siku thelathini za kukata rufaa bado zipo kama ningekuwa na pesa ningeweka wakili ili angalau afungwe kifungo cha maisha si kunyongwa!”
Alishuhudia Prosper akisukumwa na  askari magereza kuingizwa gerezani,   Belinda alibaki  akishangaa  bila kujua la kufanya na hakujua baada ya kutoka  gerezani angeelekea wapi! Alitamani kurudi  nyumbani kwa baba yake lakini kila alipokumbuka yaliyompata mara ya mwisho alipokwenda alishindwa kufikia uamuzi huo.
“Mdogo wangu  unaweza kuja Jumamosi au Jumapili, ndiyo siku ya kuona wafungwa!” Alisema askari magereza baada ya kurudi na kumkuta Belinda.
“Ahsante  sana dada kwa kweli ninakushukuru mno kwa msaada wako Mungu atakulipa!”
“Huyo ndiye mumeo?”
“Ndiyo na  ndiye baba wa mtoto  huyu!”
“Ulisema wewe ni mtoto wa mzee Thomson Komba?”
“Ndiyo!”
“Mama yako ni yupi?”
“Mke wake wa kwanza achana na  huyu aliyepo hivi sasa ambaye ni mama wa David na John!”
“Kwa hiyo wewe mama yako ni aliyefariki?”
“Ndiyo!”
“Sasa kwanini usirudi ukae nyumbani kwa baba yako kama mumeo amehukumiwa kunyongwa?”
“Dada…wee acha tu!” Belinda aliongea kwa masikitiko.
“Kwanini unasema hivyo?”
“Huwezi kuamini baba yangu hataki hata kuniona, alinifukuza kama mbwa kila ninapokwenda nyumbani hunifukuza!”
“Kwanini?”
“Eti kwa sababu nilipata mimba ya huyu mtoto hawakutaka  iwe  hivyo  nimetengwa kabisa na familia yangu!”
“Pole sana, sasa ukitoka hapa utakwenda wapi?”
“Kwa kweli sijui ila Mungu mwenyewe anaelewa, najua hawezi kuniacha!”
“Ningeweza kukuchukua ukae nyumbani kwangu lakini  nina chumba kimoja tu na nina familia kubwa, ninakuhurumia lakini sina la kufanya kukusaidia!”
“Hakuna shida Mungu anafahamu yote!”
           *************
Baada ya kuondoka gerezani Belinda alianza kutembea kuelekea kituo cha mabasi cha Segerea, akiwa njiani mvua kubwa ilianza kunyesha na kuwalowanisha yeye   na mtoto wake. Alihofia mtoto wake  kupata kichomi lakini hakuwa na la kufanya ilibidi aendelee na safari yake hadi kituoni ambako alisimama  peke yake akisubiri magari lakini  halikupita gari lolote kuelekea mjini, alisongea pembeni na kujikinga mvua chini ya mti na kuendelea kusubiri gari ambalo lingepita.
Akiwa katika dimbwi la mawazo ghafla alishtukia gari moja likipita kwa kasi kubwa na mbele kidogo lilisimama na kuanza kurudi kinyumenyume, Belinda alipoliona alijua ni msamaria mwema  amemwona yeye na mtoto wake akawahurumia na kuamua kuwapa msaada wa usafiri.
Alianza kukimbia kulifuata gari hilo wakati  likirudi nyuma, alipolifikia alizunguka upande wa dereva na kuinamisha kichwa chake ili aongee naye lakini dirisha liliendelea kufungwa ilionekana watu waliokuwa ndani walikula kiyoyozi cha kasi, dakika moja baadaye Belinda akiendelea kulowa dirisha lilianza kufunguliwa taratibu.
Hakuyaamini macho yake kwa alichokiona ndani ya gari hilo, kulikuwa na watu wanne na kila mmoja wao alikuwa ameshika chupa ya bia mkononi mwake! Walionekana  ni watu waliolewa  na waliongea kwa sauti ya juu kupita kiasi!
“Wee kuku unakipeleka wapi hicho kifaranga chako?” Ilikuwa ni sauti ya dereva na sauti hiyo haikuwa ngeni kabisa masikioni pa Belinda ingawa dereva mwenyewe alivaa kofia kubwa iliyofunika uso wake na aliongea akiwa ameinamisha kichwa sababu ya kulewa!
Wasichana wote ndani ya gari hilo walicheka kusikia mwanamke mwenzao anaitwa kuku! Dereva alivua kofia yake ndipo Belinda alipotambua alikuwa  ni David kaka yake wa kambo! Nyuma alikaa mdogo wake John naye akiwa amekumbatiwa na  msichana mrembo kupita kiasi! Kila mtu alikuwa na chupa ya bia mkononi mwake.
“Ingia kwenye buti tukupe lifti kifaranga chako kitapata kichomi!” Lilikuwa ni tusi jingine tena kwa Belinda kutoka kwa mtu waliyechangia naye baba, roho ilimuuma sana Belinda ukizingatia mali zilizowatia kiburi zilikuwa ni za baba yao wote.
“Mpenzi ondoa gari bwana nini achana na kichaa huyo!” mrembo aliyekaa pembeni kwa David alisema na gari lilianza kuondoka kwa kasi likimmwagia Belinda matope mengi! Alisikia kitu kama miba kikimchoma moyoni mwake  yalikuwa ni maumivu ya moyo! Akajikuta amekaa chini kuanza kulia.
Belinda aliona dunia kwake ni kama jehanamu, alikuwa akiadhibiwa kwa kosa ambalo hakulielewa, kila upande ulikuwa umemgeukia yeye hakuwa tena na mahali pa kukimbilia, alijihisi kuwa na mkosi.
“Ee Mungu kwanini mimi tu?”Belinda alijiuliza huku akilia  machozi.
Sekunde chache baadaye akiwa amekaa chini mvua ikiendelea kumnyeshea, alisikia honi nyuma yake, kumbe alikuwa katikati ya barabara bila kufahamu, gari hilo lilikuwa ni daladala!
“Huyu sijui chizi?” Dereva aliwaambia abiria waliokuwa  ndani ya  gari.
“Inawezekana ni chizi kweli?””Piiiii!Piiiiii!Piiiii!” Dereva alizidi kupiga honi.
Belinda alijinyanyua taratibu kutoka katikati ya barabara huku akipunga mkono kumwomba dereva asimamishe gari ili apande lakini dereva  aliondoa gari bila kujali, alisimama aliposikia kelele za abiria   zikimwomba asimame na kumsaidia Belinda na mtoto wake.
“Simama bwana umsaidie hata kama ni chizi ana mtoto mdogo anayelowa na mvua!” Mama mmoja aling’aka ndani ya gari.
Gari lilisimama na Belinda alikimbia mbio na kupanda ndani ya gari, nguo zake zilidondosha maji kiasi cha kuwalowanisha  abiria wengine ndani ya daladala hilo! Wengi walifoka na watu wote waliokuwa karibu yake walilalamika vibaya, kabla hajakaa vizuri kitini  dereva alisikika akipiga kelele kwa sauti ya juu!
“Jamani ajali!Gari   linadumbukia darajani!”
Kufuatia sauti hiyo abiria wote walitupa macho yao mbele  kuangalia ni kitu gani kilikuwa kimetokea, Belinda alikuwa miongoni mwa watu waliofanya jambo hilo kweli gari lilikuwa    darajani tena ndani ya maji ya mto uliokwenda kwa kasi ni sehemu ya juu tu iliyoonekana.
Dereva alipolifikia daraja alilisimamisha gari pembeni na watu wote walishuka na kukimbia  darajani kwenda kuona kilichotokea hata Belinda   alifuata nyuma akiwa na mtoto wake mgongoni mvua ilikuwa bado ikinyesha!
“John tuna kamba kwenye gari?” Dereva alimuuliza konda.
“Ndiyo!”
“Itoe ili tujaribu kuvuta hii gari tuone itakuwaje inawezekana kuna watu ndani!”
“Poa Suka!”
Dereva na utingo wake walikimbia kwenda mahali lilipokuwa gari na dereva aliligeuza na kuanza kulirudisha kinyumenyume  kuelekea darajani, mita kama kumi hivi alilisimamisha na  likafungwa kwa kamba na kuanza kuvutwa!
 Ilikuwa kazi ngumu lakini  kama saa  nzima baadaye  magari la watu wengi wakiwepo eneo la tukio kutoa msaada gari liliopolewa kutoka majini.
“Masikini kuna watu ndani, tena wamekufa tena wakiwa wamekumbatiana” Mtu mmoja alipiga kelele baada ya kuchungulia ndani ya gari lilipotolewa majini.
Belinda hakutaka kuwa mvumilivu alisogea karibu ili naye ashuhudie kwa macho yake! Tukio hilo lilionekana kumsahaulisha kidogo matatizo aliyokuwa  nayo  hivyo alisogea karibu. Milango ya gari ilipofunguliwa mbele ya macho yake na maiti  kuanza kutolewa, alianguka chini na kulia alipogundua kuwa walikufa walikuwa ni kaka zake waliompita kituo cha basi na kumkebehi, pamoja na kumfanyia kitendo kibaya.
“Ni kaka zangu! Ni kaka zangu! Jamani ni kaka zangu!”Belinda alizidi kulia na kupiga kelele akipita  katikati ya makundi ya    watu,  alionekana kuwa amechanganyikiwa na wanawake wawili walimnyang’anya mtoto na wengine  walimshikilia ili asifanye vurugu zaidi.
“Unakaa wapi dada?” Mtu mmoja aliuliza lakini  Belinda hakujibu kitu, alishindwa kusema moja kwa moja kuwa aliishi kwa mzee Thomson Komba kwa sababu alikuwa na muda mrefu tangu afike eneo hilo.
“Nyumbani kwenu ni kwa nani dada?” Dereva wa gari hilo naye aliuliza swali hilo hilo!
“Kwa mzee Thomson Komba!”
“Mzee Thomson Komba? Una uhakika?”
“Mimi ndiye mtoto wake wa kwanza na hawa waliokufa ni kaka zangu ila wasichana wao ndiyo siwafahamu!” Belinda aliongea huku akilia machozi.
“Una namba za simu ya nyumbani kwenu?”
“Ndiyo ni 0744-382856, hiyo ndiyo namba ya simu ya baba ya mkononi”
“Jamani nani ana simu kati yetu?” Dereva aliuliza abiria mmoja aliyejitokeza na kutoa simu yake itumike, walimpigia mzee Komba na pia kuwataarifu polisi.
Mzee Komba alipata mshtuko mkubwa sana na saa moja tu baadaye alifika eneo la tukio akiwa na mke wake na kukuta maiti za watoto wake zikiwa zimelazwa chini kwenye nyasi! Alilia machozi kwa uchungu, Belinda alijificha katikati ya watu  akilia alimwogopa sana baba yake na alijua angeweza kumuaibisha mbele za watu!
“Watoto wangu hawa niliwaeleza kila siku juu ya tabia yao mbaya ya ulevi na  hawakunisikia, hatimaye leo mabaya yamewakuta!” Alisema mzee Thomson Komba kwa uchungu na mkewe aliitikia kwa kilio.
“Masikini sina mtoto tena zaidi, hivi sasa tegemeo langu ni kwa mwanangu Belinda! Nitamtafuta popote alipo ili arudi nyumbani haraka iwezekanavyo! Nitamtafuta  kwa gharama yoyote ile!” Alisema mzee Thomson kwa  sauti huku akilia, maneno hayo yalimfikia Belinda moja kwa moja  akiwa katikati ya watu.
Belinda hakuamini kama maneno yale yalitoka mdomoni mwa baba yake aliyemchukia siku zote! Belinda alijikuta  akimwonea huruma   baba yake na chuki yote aliyokuwa nayo moyoni  juu ya baba yake iliyeyuka! Belinda  akitetemeka alianza kutembea kupita katikati ya watu kwenda mbele alitaka amwambie baba yake kuwa  alikuwa  maeneo yale.
“Baba!Baba!Baba!” Hatua tatu kabla hajamfikia baba yake Belinda alimwita mzee Thomson  na aliisikia sauti hiyo na kugeuka nyuma kuangalia na kuanza kumfuata akiwa amepanua mikono yake ili amkumbatie.
“Mwanangu Belinda kaka zako wameku… ! Kabla mzee Thomson hajaimalizia sentensi yake, Belinda kwa macho yake alimshuhudia baba yake akilegea na kuanguka chini kama mzigo na kugeuza macho juu! Belinda akiwa na mtoto wake mgongoni alianguka juu ya baba yake na kuanza kumtingisha baba yake   lakini hakuitikia, na alianza kutoa damu mdomoni  na puani  watu wote walishangazwa na kilichokuwa kimetokea.
“Yaani watoto wamekufa na baba pia?” Abiria mmoja aliuliza kwa huzuni.






Maiti zote zilibebwa na kupakiwa ndani ya magari yaliyokuwepo eneo la tukio na mzee Komba akiwa hoi alipakiwa katika gari lake akifuatana na mkewe pamoja na Belinda akiwa na mwanae mgongoni wote ndani ya gari hilo walilia machozi, ilikuwa huzuni kubwa mno kwao.
 Pamoja na kulia kwa uchungu mke wa mzee Komba bado alionyesha chuki yake kwa Belinda waziwazi, kila mara alimwangalia  kwa macho ya hasira na kumsonya, alionekana kutopendezwa   na kuwepo kwa Belinda na mtoto wake katika tukio hilo.
“Na wewe umefikaje hapa na hicho kitoto chako si nilisikia ulikuwa Tabora?” Aliuliza mama huyo kwa nyodo.
“Mamaaa!” Belinda aliongea kwa sauti.
“Mama yako nani?”
“Tuyaache yote haya  ninachotaka kusema  ni  kuwa tusahau tofauti zetu ili tushughulikie matatizo yaliyopo , David na John wamefariki na baba ndiye huyu anaumwa kupita kiasi!” Alisema Belinda kwa uchungu.
Maneno ya Belinda yalimchoma sana mama huyo moyoni mwake na kumkumbusha watoto wake wawili ambao tayari walikuwa marehemu na walikuwa ndani ya gari lililokuwa mbele yao likielekea chumba cha maiti cha hospitali  ya Muhimbili.
Kwake yote yaliyotokea yalikuwa ni kama ndoto! Hakuamini kama David na John walikuwa wamekufa, Belinda alimshika begani na kuanza kumbembeleza ili  asilie zaidi lakini  aliendelea kulia zaidi, mama huyo aliushika mkono wake na kuutupa pembeni akionyesha kutofurahishwa kabisa na kitu ambacho Belinda alifanya.
“Toka hapa unanibembeleza kitu gani? Si ni heri ungekufa wewe na hicho kitoto chako kama kuzimu wahitajika watu wawili badala ya kufa watoto wangu!” Alisema mama huyo huku akimwangalia Belinda kuanzia miguuni, macho yake yalipofika kichwani  yalianza kushuka tena hadi miguuni   kisha akasonya kwa nguvu!
Belinda alijisikia kudhalilishwa kiasi cha kutosha alijisikia kama yu uchi wa mnyama! Alitamani kuwa na mama aliyempenda lakini mama yake hakuwepo duniani alishafariki miaka mingi na baada ya kufariki mama yake na kumwacha Belinda akiwa mtoto mchanga ndiyo baba yake alipomuoa mwanamke huyo.
Walipofika hospitali ya Muhimbili walipokelewa, gari lililobeba maiti lilipitiliza hadi chumba cha maiti  ambako miili ya John na David pamoja na wasichana waliokuwa nao ilihifadhiwa katika majokofu, baadaye  taarifa  ilitolewa polisi juu ya ajali hiyo.
Haikuchukua muda mrefu habari zikawa zimekwishasambaa kila sehemu  ya jiji la Dar es Salaam kuwa watoto wa mzee Komba walikuwa wamefariki dunia baada ya gari lao kuacha njia na kudumbukia mtoni! Shule ya makongo waliyosoma    watoto hao iligubikwa na masikitiko makubwa, karibu kila mtu shuleni hapo hadi walimu walilia.
            *********************
“Hiki ni kiharusi mzee huyu alishtuka sana ndiyo maana hali hii ilitokea!”!” Alisema daktari baada ya kumpima mzee Komba
Baada ya kupimwa alichukuliwa  na kupelekwa katika wodi ya wagonjwa mahututi,  iliyotumiwa na watu wenye pesa na viongozi  mbalimbali   na kuanza kupewa matibabu ya uhakika, fahamu zake hazikurejea mpaka baada ya siku  pili alipozinduka na  kumkuta Belinda pembeni ya kitanda chake akiwa na mtoto wake mgongoni.
“Baba!Baba!Baba!” Belinda aliita  hakuamini kama baba yake alikuwa amefumbua macho baada ya kukaa bila fahamu kwa  masaa zaidi ya arobaini na nane.
Mzee Komba aliangaza macho yake huku na kule chumbani hakuona mtu mwingine zaidi ya Belinda.
“Ma..ma..ya..ko..yu..po..wapi?” Aliuliza mzee Komba.
“Yupo nyumbani baba!”
“Nyumbani wapi?”
“Nyumbani kwetu!”
“Kwani hapa ni wapi?”
“Hapa ni hospitali!”
“Kwanini nipo hapa?” Mzee Komba aliuliza lakini Belinda alishindwa kumsimulia kilichotokea kwa kuogopa kumsababishia  matatizo zaidi.
“Kwanini nipo hapa?” Mzee Komba aliuliza tena.
“Uliugua ghafla!”
“Niliugua ugonjwa gani na kwanini?”
Kabla hajajibu mlango ulifunguliwa na daktari akaingia na kundi  la  wauguzi  na madaktari   kama watano hivi!
“Ha! Leo mzee Komba anaongea?” Daktari mkuu aliuliza, watu wote walionekana kushangazwa sana na hali hiyo, kila mtu alisogea karibu na kitanda cha mzee Komba na kuanza kushangaa.
“Dada tunaomba utupishe  kidogo tumpime  mzazi wako!”Daktari alimwomba Belinda na bila kusita  alifungua mlango na kutoka  nje akiwaacha madaktari bado wanamshangaa baba yake.
Akiwa nje ya wodi mawazo yake yalimrejesha tena gerezani  na kuanza kumfikiria Prosper, kila fikra  kuwa angenyongwa na kufa zilipomwijia kichwani mwake  aliumia zaidi na kulia! Kila upande kwake ulikuwa na maumivu, baba alikuwa mgonjwa na Prosper alikuwa gerezani.
Baadaye madaktari walitoka nje na kumwomba Belinda aingie lakini walimuonya juu ya kuongea habari yoyote ya  kusikitisha na baba yake, alipofika ndani alimkuta baba yake akibubujikwa na  machozi, Belinda aliinama na kuanza kumfariji.
“Tafadhali nieleze usifiche kitu ni nini  kilichotokea hadi nikawa hapa?”
“Uliugua tu baba!”
“Ugonjwa gani?”
“Homa!”
“Homa? Haiwezekani hata kidogo, hii siyo homa mbona mwili wangu umepooza wala sijisikii kabisa?”
“Usiwe na wasiwasi baba utapona tu!”
“Mwanangu Belinda naomba sana unisamehe kwa yote niliyokutendea ni mama yako wa kambo aliyesababisha! Najuta kwanini nilifanya hivyo! Hali yangu ni mbaya na  ninafahamu nitakufa, sitaki kukuachia matatizo baada ya kifo changu  ninaelewa ni kiasi gani mama yako hakupendi hivyo kuna uwezekano ukakosa kitu chochote kutoka katika mali zangu  nenda upesi ukalete karatasi nikuandikie urithi!”
Maneno hayo ya mze Komba yalimtisha   Belinda, alijua  pamoja na kuonyesha hali nzuri kulikuwa na jambo baya ambalo  lingetokea katika muda mfupi!
“Nipe maji ya kunywa kwanza kabla hujaondoka mwanangu!” Mzee Komba alisema.
 Mara nyingi Belinda alishasikia watu wakisema  kitendo cha mgonjwa kuomba maji akiwa katika hali mbaya ni dalili ya kuaga dunia! Aliyakumbuka maneno hayo lakini hakutaka kuyatilia maanani wala kuyachukulia kuwa ni kweli, aliiona ni imani ya watu na kunyanyuka kwenda kumimina  maji katika glasi na kumpa baba yake.
“Belinda fanya haraka   uniletee karatasi, sitaki upate shida nina wasiwasi mama yako hatakupa kitu chochote kile baada ya kifo changu!”
Belinda alitoka mbio hadi ofisini kwa wauguzi na kuomba msaada wa karatasi na kalamu, wauguzi  walimpatia vitu vyote alivyohitaji na kuondoka  mbio ofisini! Hali hiyo iliwashtua wauguzi ikabidi wamfuatilie,  walimkuta mzee Komba akiandika maneno fulani kwenye karatasi  huku mkono wake ukitetemeka, mwandiko ulikuwa mbaya mno na aliandika maneno machache sana yaliyotaja nyumba mbili zilizokuwa katikati ya jiji la Dar es Salaam  kuwa zilikuwa mali ya Belinda tangu siku hiyo! Alipomaliza kuandika aliwapa wauguzi wakaisoma karatasi hiyo.
“Man...esi nyie ndi..o mmes..huhudia jam...bo hili tafadhali nitili...eni sahihi  ze..nu hapo juu kabla sijafa!” Alisema mzee Komba na kuwapa manesi karatasi.
“Mzee Komba huwezi kufa utapona tu!”
“Mimi mwenyewe najua hali niliyonayo!”
Bila kusita wauguzi walifanya hivyo na kuanguka sahihi zao juu ya karatasi hiyo nyeupe, wauguzi wote pamoja na Belinda walikodolea macho karatasi na kumsahau mgonjwa kitandani kwa muda! Walipomaliza kutia sahihi waliirudisha karatasi hiyo kwa mzee Thomson Komba lakini  hakuipokea ingawa mkono wake ameunyoosha kama mtu aliyetaka kupokea kitu!
Walipoiweka barua hiyo mkononi ilidondoka chini, kila mtu alishangaa sana na  Belinda alipotupa macho yake usoni kwa baba yake alichokiona kilimfanya  alie kwa sauti ya juu macho ya mzee Komba yalikuwa yametoka nje na alikuwa akitupa shingo yake huku na kule kama mtu aliyekuwa akikata roho!
Mmoja wa wauguzi alipoona hivyo alitoka mbio kwenda hadi chumba cha daktari lakini hakumkuta, alikuwa wodini akiendelea na raundi yake,  alikimbia hadi wodini ambako alimkuta daktari na kumpa taarifa za tukio hilo na  wote waliondoka mbio kwenda hadi chumbani kwa mzee Komba.
Walipoingia chumbani walimkuta Belinda akilia machozi kwa sauti ya juu! Daktari alinyoosha hadi kitandani na kuanza kumpima mgonjwa, alinyanyua uso wake dakika kama mbili hivi baadaye alikuwa na huzuni kubwa alimkumbatia Belinda na kuanza kumpigapiga mgongoni.
“Binti nasikitika mzee amefariki! Nini kimetokea wakati nimemwacha anaongea?” Alisema  daktari.
“Hali yake ilibadilika ghafla!” Alijibu Belinda.
              ********************
Taarifa za kifo cha mzee Komba zilipelekwa nyumbani kwake  ambako shughuli za mazishi ya watoto wake wawili David na John ziliendelea, mke  wake alilia kupita kiasi kufuatia habari hizo na kuondoka kwenda hadi hospitali kuuchukua mwili wa mumewe! Ilikuwa ni siku ya huzuni kubwa mno kwake kupoteza watu watatu katika siku moja  kila mtu jijini Dar es Salaam alihuzunishwa na tukio hilo na  mamia ya watu walikusanyika nyumbani kwa mzee Komba  ambako mazishi yalifanyika.
Wote watatu wakawa wamezikwa kwa siku moja na Belinda akiwa nyumbani kwao kushuhudia mazishi hayo, alilia mno kila alipomfikiria baba yake na alijisikia kumsamehe kwa yote aliyomtendea.
Pamoja na kufiwa na baba na ndugu zake bado Belinda hakusahau hata siku moja kuwa Prosper alikuwa gerezani, Jumapili iliyofuata alikwenda tena gerezani na kuonana naye na alimpa taarifa juu ya kifo cha baba  yake, Prosper alionyesha masikitiko makubwa sana!
“Bahati mbaya sikuwahi kukutana na baba yako ana kwa ana!”
“Usijali Prosper haikupangwa mkutane!”
Wiki moja tu  baada ya kifo cha baba yake matatizo mazito yalianza kumpata Belinda nyumbani kwao, mama yake wa kambo alianza kumfukuza pale nyumbani akidai arudi alikotoka! Hilo halikumsumbua  sana  Belinda ukizingatia tayari alikuwa na wosia wa kurithishwa nyumba mbili za mamilioni ya pesa katikati ya jiji, alichofanya ni kuondoka nyumbani na kwenda kwenye moja ya nyumba zake na kujitambulisha kwa wapangaji ili wafahamu kama mmiliki wa nyumba walizoishi.
Moja ya nyumba iliyokuwa mtaa wa Mafia namba 30,   ilikuwa na chumba kimoja  katika ghorofa yake ya pili kilikuwa na kila kitu ndani,   kabla ya kifo  chake baba yake alikitumia kupumzika kila alipokuwa na mawazo.
Belinda alitafuta mafundi  wa ujenzi na mlango wa chumba  ukavunjwa,  akaingia ndani  hicho kikawa ndiyo chumba chake na maisha yake na mtoto wake  yakahamia hapo, pesa aliyopata kutoka kwa wapangaji ilimsaidia kuendesha maisha yake ya kila siku. Mambo yalianza kuwa mazuri  Belinda alianza kunawiri lakini mawazo yake yaliendelea kubaki kwa Prosper gerezani,   wazo la kumsaidia kutoka  gerezani lilianza kumwingia akilini.
“Labda nikikata rufaa   inawezekana  kumfanya asinyongwe, nitauza nyumba yangu moja pesa nitakayopata  nitamlipa wakili wa kunisaidia katika kesi  kwani nyumba ni bora kuliko Prosper?” Aliwaza Belinda na kweli siku iliyofuata alikwenda moja kwa moja   ofisini kwa mzee Rutashobya, mmoja wa  mawakili  maarufu  katika jiji la Dar es Slaam  na kumweleza matatizo aliyokuwa nayo ili aone kama angeweza kumsaidia.
“Ni lini hukumu  ilitolewa?”
“Wiki iliyopita tu!”
“Basi bado tuna muda wa kukata rufaa nitajaribu kufanya hivyo lakini utanilipa shilingi  milioni tano unazo pesa hizo?”
“Pesa sina ila nina nyumba ambayo nitaiuza kisha nitakulipa pesa hiyo!”
“Kwanini usinipe  hiyo nyumba mimi tumalizane?” Wakili aliingiwa na tamaa ya kujipatia mali kwa njia rahisi.
“Hapana ni vyema tu niiuze  na nikulipe pesa  unayodai na nyingine inisaidie mimi na mtoto wangu!”
“Sawa,  basi kesho nitasafiri kwenda Tabora kukata rufaa, nitakusaidia binti usiwe na shaka!” Alisema wakili Rutashobya mzee  mwenye  umri kati ya hamsini na sitini hivi!
Siku iliyofuata Belinda alitafuta madalali wa  City Auction Mart na kuwaeleza nia ya kuiuza moja ya nyumba zake na aliwaonyesha barua aliyoachiwa na marehemu baba yake, waliichukua barua hiyo hadi kwa mama yake wa kambo na kumwonyesha, hakuwa na kipingamizi chochote kwa  sababu mali aliyoachiwa ilikuwa nyingi zaidi.
Nyumba ikapigwa mnada kwa shilingi  milioni  25!  Belinda alifurahi kupata pesa na bila kuchelewa alifungua akaunti  katika benki ya NBC na  kuziweka pesa zote  benki ili zimsaidie katika kesi! Alitaka sana  kumtoa Prosper gerezani  pamoja na kuambukizwa Ukimwi bado Belinda alimpenda kupita kiasi.
“Sitaki  afe kwa kunyongwa! Nataka mimi na yeye na Alicia mtoto wetu tuishi pamoja  tena tukisubiri kifo chetu cha Ukimwi basi!” Aliwaza Belinda.

No comments

Powered by Blogger.