KIFO CHA MTU ASIYE NA HATIA - 06
Dunia ilionekana kubadilika
na
kuwa sehemu ya mateso
makubwa kwa Belinda. Hakuamini kama
binadamu wote waliishi katika shida kama alizokuwa nazo yeye, alibadili
matatizo kama nguo! Likitoka hili linaingia jingine, Belinda alihisi kukata
tamaa. Baya na lililomsumbua zaidi lilikuwa ni la virusi za Ukimwi ambavyo
alihisi Prosper aliambukizwa na Savimbi katika mchezo wa wanaume kwa wanaume kuingiliana gerezani.
Belinda alikuwa
ameamua kuufahamu ukweli wa majibu ya
damu kutoka kwa Prosper ili auondoe wasiwasi moyoni mwake
“Ulipimwa
damu?”Belinda alimuuliza Prosper!
“Ndiyo nilipima Belinda!”
“Majibu yako wapi?”
“Ninayo!”
“Nipe basi niyaone!”
“Naogopa kukupa!”
“Kwa nini? Wewe nipe tu!”
“Sijui kama utaweza kuyakubali!”
“Kwani una virusi katika damu yako Prosper?”
“Nd….i…o Belinda ila nisamahe sana!” Prosper alianza kulia machozi
na alishindwa kumwangalia Belinda usoni.
“Kweli?” Belinda aliuliza tena, hakuliamini jibu alilopewa.
“Prosper tafadhali nionyeshe cheti chako cha majibu!” Aliendelea
kusisitiza Belinda.
“Niamini na naomba unisamehe
sana Belinda!”
“Nipe cheti Prosper siwezi kuamini hivi hivi!” Belinda alisema kwa
ukali.
Katika maisha yake Prosper
hakuwahi kumwona Belinda katika hali hiyo, ilimlazimu aingize mkono
ndani ya kaptura yake, alionekana
akivuta kitu fulani ndani ya nguo
yake ya ndani na mkono ulipotoka ulikuwa na kikaratasi kidogo kilichokunjwa
kikiwa kimelowa jasho alimkabidhi Belinda!”
Huku akitetemeka Belinda
alianza kukikunjua kikaratasi hicho na kuanza kukisoma, kadri alivyozidi
kusoma ndivyo machozi yalivyozidi k ummiminika
hatimaye alijikuta akilia machozi huku kichwa chake akiwa amekiinamisha chini! Kilionyesha tayari
Prosper alikwishaambukizwa virusi vya Ukimwi.
“Hivi mimi nina mkosi gani?”
“Wewe huna mkosi hata kidogo Belinda, mwenye mkosi ni mimi
niliyewaua wewe na mwanangu bila hatia”
“Prosper ni heri ningekufa
mimi kuliko Alicia ana makosa gani mtoto
huyu?” Aliongea Belinda huku akizidi kulia.
Prosper alipomwangalia mwanae Alicia mikononi mwa mama yake naye
alijikuta machozi mengi zaidi yakimtoka, alijilaumu kwa kila kitu kilichotokea na alijilaumu kwa kuua watu wasio na hatia,
alijisikia mkosaji mbele za Mungu na mbele za Belinda na Alicia! Kwa kosa hilo
aliamini hakustahili kuishi.
“Prosper nimejitahidi kuwa mwaminifu kwako lakini bado umeniua,
nimeacha mambo mengi pamoja na utajiri wa baba yangu kwa ajili yako na ninateseka leo hii tena umenitia virusi vya
Ukimwi mwilini mwangu!”
“Belinda ni shetani aliniingia usinilaumu sana Belinda utanifanya nikose sababu ya kuishi!”
Prosper alipiga magoti mbele ya Belinda na kuanza kumshika miguu kama ishara ya
kumwomba msamaha!
“Hii haitoshi Prosper umekwishaniua basi inatosha!”
“Sikujua itakuwa hivyo Belinda ilitokea kama ajali
na kama ningepewa nafasi nyingine nisingefanya hivyo na ninajuta moyoni mwangu nisamahe Belinda kwa kukatisha maisha yako!”
Belinda hakujibu kitu alibaki amesimama wima mtoto wake akiwa mgongoni, alihisi akili yake kuchanganyika,
ubongo wake kusimama kufanya kazi sawasawa, alijilaumu kwa kila kitu
alichokifanya maishani mwake.
Hakuwa na kimbilio tena maishani kwake na alikiona kifo chake kikija kwa kasi!
Katika maisha yake hakuna kitu alichoogopa kama kifo cha Ukimwi kwani
kiliwatesa watu wengi na kilionekana kama kifo cha aibu na hakutaka
kufa katika jina la umalaya kama jinsi
watu wengi walivyokitafsiri kifo cha
Ukimwi, Belinda aliamini hakuwahi kuwa malaya katika maisha yake.
“Prosper!”
“Naam Belinda!”
“Sitakusamahe maishani mwangu na hata kama nitakusamahe basi
sitasahau siku zote!” Alisema Belinda na kuanza kutembea kwa haraka kutoka chumbani kwenda nje ya
gereza.
“Belinda! Belinda! Belinda usiondoke!” Prosper aliita wakati
Belinda akitoka chumbani lakini hakugeuka kuangalia nyuma alizidi kutembea
kwa haraka huku akilia.
*****************
Alitoka hadi nje ambako alitembea hadi kituo cha mabasi madogo na
muda mfupi baadaye daladala moja lilikuja na kusimama pembeni yake, alimbeba vizuri mtoto wake na kuingia
ndani na kuchukua kiti cha nyuma kabisa,
alikuwa bado na hofu ya kusababisha harufu lakini alipokumbuka kuwa
alishafanyiwa operesheni na kuwa mkavu hofu hiyo ilitoweka mara moja.
Belinda aliendelea kububujiwa
na machozi hadi wakati anafika
mjini, watu wote ndani ya gari walimshangaa na walipomuuliza ni kwanini alilia
machozi kiasi kile hakueleza chochote.
Alipomwangalia mtoto wake mzuri Alicia, aliyekuwa ameketi mikononi
mwake roho yake ilimuuma zaidi, alikuwa mtoto mzuri mno kufa kwa Ukimwi!
Ilimuuma sana Belinda kujua kuwa hata mtoto wake hakuwa na maisha marefu mbele
yake, lakini Alicia hakuwa na taarifa na kilichokuwa kikiendelea aliendelea
kutabasamu huku akimpigapiga mama yake usoni.
Alipofika mjini Tabora aliteremka ndani ya basi, alihisi kukata
tamaa ya kila kitu! Hakuona sababu ya kurudi tena Tutuo, kijijini kwao Prosper alichofikiria wakati huo ni kurudi tena Dar es Salaam kwa baba yake na kujaribu
kumwomba msamaha! Lakini alipokumbuka jinsi baba yake alivyomfukuza kama mbwa roho iliingiwa wasiwasi na kujikuta
akisita kuchukua hatua hiyo.
“Kwa kweli baba asingekuwa na matatizo ningerudi Dar , acha tu
nirudi Tutuo!”
Baada ya kuwaza sana hatimaye mawazo yake yalimfikisha katika
hatua hiyo lakini alipokumbuka kuwa nyumba aliyofikia ingekuwa tayari imekwishabomolewa
na mwarabu aliyeinunua ili ajenge mashine, Belinda alikosa mahali pa kuelekea kwa sababu
hakuona mahali pengine popote pa kufikia kijijini Tutuo.
“ Lakini acha tu niende, Wanyamwezi ni watu wakarimu sana, nitaomba
kukaa kwa mtu yeyote au nitarudi tena kuomba kazi nyumbani kwa Mwarabu Mzee
Mohamed nafikiri safari hii atakubali kwa sababu sina mimba na sinuki kama
ilivyokuwa zamani!”
Belinda aliamua kurudi
kijijini na alichofanya ni kwenda stendi
ya basi ambako alipanda basi la kumpeleka kijijini Tutuo, njia nzima aliendelea
kulia alijua maisha yake yalikuwa yamefika mwisho! Alihisi hakuwa na maisha
tena mbele yake, binafsi hakujionea huruma sana aliyemtia simanzi zaidi alikuwa ni mtoto wake Alicia.
“Masikini Alicia anakufa kwa kosa lisilo lake akini kwanini hasa mtu
amuue mtoto asiye na hatia? Prosper alishindwa kuvumilia shida? Nasema sitaki kumwona tena
maishani mwangu!” Alisema kwa uchungu Belinda, hakujua alikuwa akiongea kwa
sauti kiasi kwamba watu wote ndani ya basi waligeuka kumwangalia.
*******************
Gerezani:
Baada ya kuachwa chumbani Prosper alinyanyuka kwa unyonge na
kutembea hadi chumba cha mahabusu na kwa
muda mrefu aliendelea kulia na hakuona tena sababu ya kuendelea kuishi,
alitamani kufa kukwepa aibu ya kuwaua mke na mtoto wake kwa Ukimwi lakini
alishindwa kuelewa ni kwa njia ngani angeweza kujitoa uhai akiwa ndani ya gereza.
Alilia usiku mzima hadi asubuhi, alijuta kwa yote aliyoyafanya na
alitamani sana kuonana tena na Belinda
ili apate kuongea naye na kumwomba msamaha! Alijua hilo lisingewezekana hata kidogo
kwani alikuwa na uhakika Belinda asingerudi
tena.
“Laiti ningejua nisingejiingiza katika mchezo huo mbaya, shida za gerezani zingeniua mbona watu
wengine wanaishi?” Aliwaza Prosper huku akilia.
Prosper alikuwa na watu wengi
sana wa kuwalaumu kuhusiana na suala hilo lakini watu waliopaswa kuzibeba
lawama zote hizo walikuwa ni mama na
dada zake kwa kitendo chao cha kumuua baba yake, bila wao kufanya hivyo Prosper
aliamini asingeingia gerezani katika
maisha yake!
“Ni wao ndio walilaumiwa niliingia gerezani kumwokoa mama na dada
zangu, mama mwenyewe amekwishakufa na hata hao dada zangu hakuna hata mmoja
anayefika hapa gerezani kunitembelea na
bado nyumba na kiwanja alichoacha baba
wameuza na kupotea, huu ni ukatili wa hali ya juu sana!” Aliendela kuwaza Prosper.
Baada ya siku hiyo Prosper hakuwaona tena Belinda na mtoto wake Alicia, kesi yake iliendelea katika mahakama kuu kanda ya
Tabora na miezi mitatu baada ya Belinda kuondoka kesi hiyo ilifikia hukumu yake, alionekana kuwa
na hatia mbele ya sheria baada ya yeye mwenyewe kukiri mauaji hayo ya baba yake mzazi mbele ya
jaji Mohamed Simbila na
kuhukumiwa kifo kwa kuchomwa
sindano ya sumu
Mahakama nzima ilipigwa na butwaa baada ya hukumu hiyo, Prosper hakuonyesha huzuni wala kulia badala yake alitabasamu kwa furaha baada ya
hukumu hiyo kutolewa.
“Una namna yoyote ya kujitetea?”
“Sitaki kujitetea Mhesimiwa
Jaji, hukumu yako ni sahihi na hii ndiyo niliyoisubiri ili iniepushe na kifo
cha mateso kilichopo mbele yangu!Nakushukuru sana mheshimiwa jaji na
ninakupongeza sana kwa hukumu hiyo
nzuri!” Alisema Prosper huku akicheka.
Bila kuchelewa maaskari walimpiga pingu mkononi na kumwondoa
mahakamani, jaji aliyemkuhumu alibaki na maswali mengi sana kichwani mwake,
alishafanya kazi ya kuhukumu watu kwa miaka
karibu ishirini na alishahukumu watu wengi kifo lakini hakuwahi hata siku moja kumhukumu
mtu kifo akicheka! Wengi walilia na kuomba kupunguziwa kifungo!
Siku iliyofuata Prosper ilitolewa amri Prosper
ahamishiwe gereza la Keko jijini Dar es Salaam ambako angepambana na kifo chake! Alipakiwa
ndani ya treni la abiria kutoka Mwanza kwa safari ya kwenda Dar es Salaam.
Prosper alilia lakini hakulia
sababu ya hukumu ya kifo aliyopewa ila
alilia kwa sababu alikuwa anapelekwa
kufa bila kuonana na mke na mtoto wake kwa mara ya mwisho, alikuwa
anakwenda kufa bila Belinda kufahamu ukweli juu yake! Pia alilia sababu yeye
alikuwa anakwenda kufa na kuwaacha mkewe na mwanae wakiteseka kwa ugonjwa wa
Ukimwi aliowaambukiza yeye.
*****************
Alicia, kijijini Tutuo:
Tayari alishazoea maisha ya nyumbani kwa mzee Mohamed, alifanya kazi
kwa nguvu zake zote ili aweze kumridhisha mama mwenye nyumba, alipewa chumba
kidogo ambacho alilala na mtoto wake kwa kutandika jamvi chini kila siku!
Ilikuwa ni kawaida yake siku
zote kudamka mapema na kufanya kazi zote
za ndani na ilipotimu sawa nne aliacha kazi hizo na kuanza kupasua kuni, baada ya kupasua kuni alianza kupika chakula
cha mchana na baadaye alianza shughuli za ufuaji wa nguo za kila mtu nyumbani.
Zilikuwa ni kazi ngumu lakini Belinda alizifanya ili aweze kuishi na
mtoto wake, katika miezi yote aliyokaa
nyumbani kwa mwarabu Mzee Mohamed hakuwahi kumkumbuka Prosper lakini asubuhi ya
siku hiyo akipasua kuni kumbukumbu za Prosper zilimsumbua kichwani, alitamani
sana kumwona na aliona uamuzi aliouchukua haukuwa wa
busara kwa sababu usingeweza kuubadilisha kitu chochote katika maisha yake kama ni virusi
alishavipata na ni lazima yeye na mtoto wake wangekufa.
“Ninaamini hivi sasa Prosper anahitaji msaada wangu kuliko wakati mwingine wowote katika maisha
yake!” Aliwaza Belinda huku akiendelea kupasua kuni.
Alimfikiria Prosper kwa muda mrefu hatimaye aliamua kuliweka shoka
pembeni na kuketi chini, mawazo juu ya Prosper yaliendelea kumiminika mwake.
“Hapana nakwenda gerezani!” Alisema Belinda na kulitupa shoka
pembeni, akambeba mtoto wake mgongoni na kwa kutumia khanga yake iliyochanika
alimfunga vizuri na kuondoka kuelekea ndani ambako alimkuta mke wa mzee Mohamed
na kumwomba ruhusa lakini hakuruhusiwa kuondoka.
“Belinda wewe hapana ondoka iko kazi nyingi leo!”
“Hapana mama ni lazima nikamwone Prosper nikishindwa leo ni mpaka wiki ijayo!”
“Hapana!” Mke wa mzee Mohamed alikataa katakata.
“Mama nimekwishasema naondoka,nitafanya kazi nikirudi!” Belinda
alisema na kunyanyuka.
“Wewe ondoka kwa nguvu eh! Pana rudi hapa!”
“Sawa mama!”
*****************
Alifika gerezani saa nne asubuhi, kitu cha kwanza alichofanya ni
kuomba kuitiwa Prosper.
“Dada yangu ulikuwa wapi siku zote hizi?”
“Nilikuwa safarini!” Belinda alidanganya!”
“Karibu sana!”
“Ahsante! Prosper yupo!”
“Prosper?” Askari magereza aliuliza.
“Ndiyo mbona unauliza kwa mshangao!”
“Amesafirishwa jana kwenda gereza la Keko Dar es Salaam, alihukumiwa kifo!
Belinda alichanganyikiwa na kwa kutumia basi alirudi hadi mjini
ambako alipanda basi jingine lililompeleka hadi
Tutuo. Hakukaribishwa tena
nyumbani kwa mzee Mohamed na kwa
sababu hakuwa tena na haja ya kufanya kazi aliomba mishahara yake na kuondoka
tena hadi stesheni ya treni mjini Tabora
ambako alipanda treni jioni ya siku hiyohiyo kurejea Dar es Salaam lengo lake
likiwa ni kuishi kabla Prosper hajanyongwa!
*******************
Treni iliingia Dar es Salaam saa saba mchana, Belinda aliona bado
muda ulimruhusu kwenda gerezani Keko kuonana na Prosper, hakutaka kabisa afe kabla hajaongea nae na
kumjulisha kuwa tayari alishamsamehe yote yaliyotokea.
Kutoka stesheni ya reli ya Dar es salaam hadi gereza la Keko ilikuwa kama nusu kilometa hivi, kwa
umbali huo mdogo Belinda hakuhitaji gari
alitumia njia ya mkato hadi kufika gerezani.
“Dada mwenye mtoto nikusaidie nini?” Askari magereza aliyekuwa
akilinda nje ya gereza alimuuliza
“Nimekuja hapa kumwona mume wangu!”
“Leo siyo siku ya kuwaona wafungwa njoo Jumamosi ama Jumapili
umesikia!”
“Sawa lakini……..!” Alisema Belinda huku akimsogelea askari.
“Lakini nini? Dada hiyo ni
sheria ya gereza!”
“Nilikuwa naomba kukuuliza kitu sababu sijui!”
“Kitu gani?”
Belinda alimsimulia askari huyo kila kitu juu ya Prosper na kwamba
alitaka kuhakikisha kama kweli alikuwepo
gerezani au la!
“Katokea gereza gani?”
“Isanga Tabora!”
“Nisubiri hapa niulizie!” Alisema askari huyo na kuingia hadi ndani
ya gereza na alipotoka alikuwa na jibu
la Belinda.
“Nasikitika hayupo!”
“Hayupo? Hayupo vipi wakati mimi Tabora wamenieleza amehamishiwa
gereza hili!”
“Amepelekwa gereza la Segerea sababu hapa hakuna nafasi ya wafungwa
kama yeye!”
“Ah! Sawa nashukuru sana kaka yangu!” Belinda alishukuru lakini
hakuwa tayari kusubiri hadi jumamosi ndio aonane na Prosper alihisi kufikia siku hiyo tayari
angekuwa amekwishayongwa!
“Na nitakwenda huko segerea
wakinizuia nitatumia hata hii pesa kidogo niliyonayo mpaka nimwone!”
Aliwaza Belinda.
Kutoka gerezani Keko hadi
kituo cha mabasi cha Shule ya Uhuru ambako mabasi ya Tabata na Segerea
yaliegeshwa ilimchukua dakika 30 na
kutoka shule ya Uhuru sababu ya ubovu wa
barabara ya Tabata ilimchukua saa
nzima hivyo alifika gerezani segerea saa
tisa na nusu ya jioni na kwenda moja kwa moja hadi mapokezi ambako alimkuta
askari magereza wa kike.
“Shikamoo dada!” Belinda aliamkia.
“Marahaba, nikusaidie nini mdogo wangu?”
‘Dada unavyoniona hivi ninatoka Tabora, huyu ni mwanangu nimekuja
hapa kumfuata mume wangu anaitwa Prosper, yeye
kahamishwa kutoka gereza la Isanga huko Tabora ni mfungwa aliyehukumiwa
kifo, nataka kumwona kabla ya kifo chake.
“Kwani vipi mbona unanieleza vitu vingi kwa wakati mmoja?” Askari
magereza aliuliza.
“Nisaidie dada, nisaidie mimi mwanamke mwenzio!” Aliendelea kusema
Belinda na baadaye kumsimulia askari huyo kila kitu kilichotokea katika maisha
yake na Prosper, askari alishindwa kujizuia na kujikuta akichukua kitambaa
chake na kujifuta machozi usoni mwake.
“Ni sawa nimehuzunishwa sana lakini sina jinsi ya kukusaidia kwa
sababu si rahisi kukuingiza gerezani
siku ya leo mdogo wangu,nenda uje Jumapili!”
“Dada tafadhali nisaidie!”
“Haiwezekani labda nimwite tu umwone kwa mbali lakini siwezi
kukuruhusu uingie ndani ya gereza, kwani unaitwa nani?”
“Naitwa Belinda!”
“Belinda nani?”
“Belinda Thomson Komba!”
“Thomson Komba yule mfanyabiashara?”
“Ndiyo!”
“Sawa wewe mbona una hali hiyo?”
“Maisha tu dada yangu!” Belinda alijibu huku akilia.
Post a Comment