SIMBA MKIENDELEA HIVI, MTAJICHANGANYA WENYEWE NA TIMU YENU ITASHINDWA KUFIKIA MALENGO
Na Saleh Ally
KAWAIDA ninapenda sana kuweka kumbukumbu ya mambo mengi kwa ajili ya matumizi ya baadaye au sehemu ya elimu tu.
Hivi
karibuni, nilimfanyia mahojiano mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan
Dalali ambaye alizungumza mambo mengi sana, ninaamini ilikuwa makala
nzuri iliyowanufaisha wasomaji wa gazeti hili.
Kwa
kuwa ilikuwa ni siku chache baada ya Simba Day, mzee Dalali pia
alizungumzia mambo kadhaa kuhusiana na kikosi cha Simba ambacho siku ya
tamasha hilo kiliitandika AFC Leopards ya Kenya kwa mabao 4-0.
Ushindi
wa Simba uliamsha mwamko wa matumaini mapya miongoni mwa mashabiki wake
ambao walichoshwa na timu yao kutofanya vizuri kwa miaka minne
mfululizo, inamaliza ligi bila ya kombe hata moja au kupata nafasi ya
kushiriki michuano ya kimataifa katika miwili ya mwisho chini ya uongozi
wa Ismail Aden Rage na miwili ya mwanzo ya Evans Aveva.
Sasa
wanachotaka ni mafanikio na kweli wana hamu ya mafanikio, lakini mzee
Dalali aliwaeleza kwamba katika soka, siku zinatofautiana.
Kwanza
aliwakumbusha kutokuwa na matumaini kupita kiasi, kuachana na kuamini
kwamba kwa ushindi wa siku ile au katika mechi za kirafiki, basi Simba
haifungiki tena.
Baada
ya sare ya Simba dhidi ya JKT Ruvu juzi Jumamosi, maana yake sasa
kikosi hicho kina pointi nne baada ya mechi mbili. Jambo ambalo
Wanasimba wengi wanaonekana kutofurahishwa nalo na wengine walianza
kulaumu mitandaoni, baadhi wakimtupia lawama kocha au benchi la ufundi,
mara hivi mara vile, ilimradi kila mmoja anajua sana.
Hii
ikanifanya nikumbuke kauli ya mzee Dalali, kwamba Simba ni timu na kila
siku haiwezi kushinda. Laudit Mavugo ni binadamu, hawezi kucheza kwa
kiwango cha juu kila siku. Itafikia siku atakosea au kucheza katika
kiwango cha chini, hali kadhalika kikosi kizima cha Simba.
Sasa
tayari imetokea, alichokieleza mzee Dalali wiki chache zilizopita
kimeanza kutokea. Tayari baadhi ya mashabiki wa Simba, wameanza kusukuma
lawama ambazo ninaamini kabisa hazina msingi na wasipoangalia
watajichanganya.
Kwani
Simba, wanaamini wana ubora upi hadi kupata pointi moja waone si saizi
yao au wamepunjwa sana? Wana kipi hasa cha kuona hakuna kama wao au wao
kupata sare na JKT ni kama dhambi!
Simba
ndiyo kwanza imeanza ligi, haijapoteza hata mechi moja katika mbili na
ina pointi nne. Ina kocha mpya na wachezaji wapya rundo. Unapozungumzia
kocha mpya maana yake ni mabadiliko ya mfumo na kuunganisha kikosi.
Lazima
kila mmoja ajue, mechi za kirafiki ni tofauti na ligi. Hata uchezaji
wake au maandalizi na mipango kwa makocha inakuwa tofauti. Kwa Wanasimba
waliokwenda uwanjani au kushuhudia kwenye runinga, waliona kikosi chao
kilicheza vizuri na walikuwa na matatizo mawili, matatu.
Kung’ang’ania
mpira bila sababu kwa wachezaji, umaliziaji na pia wachezaji kuonekana
kama wana presha kubwa hali inayopoteza utulivu wao.
Nimeliona
hili tatizo kwa Yanga kwa kipindi kirefu. Huenda baada ya kuwatokea,
walishindwa kulirekebisha kutokana na presha kuendelea kuwa kubwa kutoka
kwa mashabiki au kwingineko.
Simba
wanalazimika kujipanga na kuwa makini sana na hilo, la sivyo
litawaangusha na watacheza mechi nyingi wakishambulia sana lakini mwisho
wataishia kwenye sare au kufungwa wao na sifa yao itakuwa ni soka safi
la kushambulia sana bila matunda baada ya dakika 90.
Ushauri
wangu ni kwa mashabiki kuachana na kubeba presha za kishabiki na
kuziingiza kwenye kikosi chao, hali inayoweza kusababisha timu hiyo
kujawa na hofu na baada ya hapo kuzidisha kukosea au kuteremsha utendaji
wa wachezaji.
Kwa
wachezaji wa Simba nao wanapaswa kutoingia sana mitandaoni na kuonekana
wanajali au kufuatilia kila kinachosemwa, mwisho watajiangusha na
kujijaza presha zaidi.
Mzee
Dalali aliliona hilo mapema kwa kuwa anajua soka, leo na jana ni
tofauti. Vema wengine wakajifunza kupitia jicho hilo la mzee Dalali.

Post a Comment