JINI LA DARAJA LA SALENDA - 14

ILIPOISHIA:
“Kweli Suzana umechanganyikiwa.”
“Unafikiri kidogo, mtu siku zinakatika hakuna dalili zozote za kurudi kwa mpenzi wangu.”
“Suzana kwa Mganga Njiwa Manga si nilikwenda kwa ajili ya kurudishiwa kizazi?”
“Ndiyo.”
“Basi majibu yametoka.”
“Ina maana wewe ni mjamzito?” SASA ENDELEA...
“Ndiyo maana yake.”
“Utani huo.”
“Kweli shoga nimeamini yule babu ni mganga kweli.”
“Kama ni hivyo basi hataki kunisaidia.”
“Amekataa vipi wakati kakueleza ukweli juu ya ramli yake ilivyomuongoza. Ingekuwa hawezi kitu angekwambia japokuwa hajawahi kushindwa matatizo ya majini.”
“Mmh! Kwa hiyo una uhakika kuwa Brighton atarudi bila kufanya dawa yoyote?”
“Kama amekueleza atarudi ujue atarudi, si alikwenda baharini na mbuzi wawili. Kama angekuwa hataki kukusaidia asingeona umuhimu wa kwenda kujisumbua baharini saa nane za usiku.”
“Mmh! Mimi nilijua labda ni njia ya kujitetea tu.”
“Suzana, kwa taarifa nilizozipata kutoka kwa mama, Njiwa Manga kazi ya uganga huu ni mwaka wa thelathini na siyo watu wa hapa tu nchini, kuna watu wanatoka mbali kwa ajili ya kufuata tiba zake. Si hivyo tu, ameshachukuliwa sana na watu wa mbali kwa ajili ya kwenda kufanya matibabu, kuna kipindi alikuwa akiondoka zaidi ya mwaka, kitu ambacho baadaye alikiona kuwa si kizuri kwa watu wengi hukosa huduma zake na kuamua kutosafiri.
“Si wewe hata mimi siku tulipokwenda baharini na hali iliyonitokea kisha kusema eti tayari kizazi changu kimerudi niliona ni uongo. Lakini hali iliyonitokea hivi karibuni na kufanya vipimo vyote na kujiona nina ujauzito nimekubaliana na mama kuwa, kweli mzee Njiwa Manga ni mganga wa kweli.
“Kwa hiyo shoga yangu nakuomba uvumilie kama amekuhakikishia uhai wa mpenzi wako ni mrefu ni kiasi cha kuvuta subira, nina uhakika alichosema kitakuwa kweli.”
“Mmh! Itabidi nikubali lakini moyo haunipi kabisa.”
“Sikuzuii kufikiria hivyo, lakini amini usiamini mzee Njiwa Manga ni mganga wa kweli.”
“Mmh! Haya,” Suzana alikubali kwa shingo upande.
“Basi shoga mguu ulikuwa wako kukujulisha mzee Njiwa Manga amefanya mambo, punguza mawazo kila alilosema mganga litatimia mimi naamini Brighton atarudi bila ya dawa kama alivyosema.”
“Kama alichokisema ni kweli nitampa zawadi kubwa.”
“Hata mimi najiandaa kumpelekea zawadi kubwa, sijui hata nimpelekee nini?”
“Utakachojaaliwa.”
“Shoga baadaye.”
“Sawa, wacha na mimi nianze kazi kidogo umeichangamsha akili yangu bila hivyo siku ya leo ingekuwa ngumu kwangu.”
“Najua hata mimi baada ya kuona mabadiliko ya mwili moyo wangu ndipo ulipofunguka.”
“Wacha na mimi nisubiri.”
Sharifa alirudi ofisini kwake na kumuacha Suzana akijiandaa kuanza kazi za siku ile.
****
Baada ya Balkis kupelekwa katika chumba cha giza, mfalme alionekana kuzidi kukasirika kwa kuona mtoto wake amemkosea adabu. Mkewe muda wote alikuwa ameinama bila kusema kitu, baada ya mwanaye kurudishwa chumba cha giza alimgeukia mumewe na kumuuliza kwa sauti ya ukali ambayo hakutakiwa kuitoa mbele ya mfalme.
“Sasa ulinituma kufanya nini na umefanya nini?”
“Kwanza punguza sauti yako ujue unaongea na nani?”
“Nazungumza na mume wangu na aliyepelekwa katika chumba cha giza ni mwanangu,” bado malkia Huleiya hakushusha sauti yake.
“Unabishana na mimi?” Mfalme aliuliza kwa sauti ya juu.
“Sibishani na wewe kwa vile anayeteseka ni mwanangu.”
“Lakini huoni kama amevunja sheria ya majini pia na wewe unanivunjia adabu kama mumeo na mfalme wako?”
“Nimekuvunjia adabu kivipi wakati nakueleza kitu cha kweli?”
“Kwa hiyo nivunje sheria kwa ajili ya mwanao?”
“Kwani unataka aolewe na jini mwenzake au atoroke?”
“Siwezi kuvunja sheria, majini wengine watanielewa vipi?”
“Kwani si ni wewe ndiye uliyeiweka sheria hii kwa roho mbaya yako baada ya majini wengi kuwa na uhusiano na wanadamu. Umemkataza mwanao asiolewe na mwanadamu, anakuomba umrudishe duniani mpenzi wake hutaki. Kuna faida gani kuwa mfalme wakati huna mapenzi hata na familia yako.”
“Kwa hiyo nawe unaungana na mwanao?”
“Ndiyo na pia nasema hivi, Soobaaa,” malkia Huleiya alimwita mkuu wa watwana msaidizi kwa sauti kubwa.
“Wa nini?” Mfalme Balami aliuliza.
“Naam Malkia mtukufu,” Soba aliitikia akiwa amesimama mbele ya malkia.
“Soba kamtoe haraka Balkis.”
Soba alibakia amesimama na kusita kutekeleza amri hiyo kwa kuhofia kupingana na mfalme.
Soba alibakia amesimama kama sanamu, malkia Huleiya alipaza sauti yake tena:
”Soooba hujanielewa, kamtoe haraka Balkis chumba cha giza.”
Bado Soba alibaki amesimama huku akisubiri mfalme ataamua nini baada ya mkewe kutoa amri ya kupingana na mumewe kwa mara ya kwanza. Siku zote alijua mwenye sauti ya mwisho ni mfalme, malkia sauti yake siku zote aliitoa kwa taratibu tena ya chini. Toka awe ndani ya jumba lile la kifalme hakuwahi kusikia amri kali ya malkia.
“Sooooba, unanidharau?” Alimuuliza huku akiteremka sehemu ya juu alipokuwa amesimama pembeni ya mumewe.
Soba bado alisimama kikakamavu kusubiri kauli ya mfalme aende au la, aliamini siku zote mke wa mfalme hakuwa na maamuzi tofauti na mumewe. Kitendo cha Soba kukataa kwenda kumtoa Balkis kilimuudhi sana malkia na kuona umevunjiwa heshima.
Pembeni yake kabla hajafika kwa Soba alichomoa upanga uliokuwa kiunoni kwa mmoja wa walinzi wa nyumba ya mfalme na kulipunga hewani usawa wa shingo ya Soba. Wengi walijua anamtisha ili akubali kumfuata Balkis chumba cha giza alipofungiwa na mumewe.
Soba naye aliendelea kusimama kikakamavu akisubiri kauli ya mfalme aliyekuwa amepata kigugumizi kwa kitendo cha mkewe kumvunjia heshima mbele ya wasaidizi wake na watwana.
Panga alilopunga hewani bila hiyana lilitua kwenye shingo ya Soba na kutenganisha kichwa ni mwili. Kitendo kile kilimtisha kila mmoja aliyekuwepo pale, hata mfalme hakuwahi kuona hasira nzito ya mkewe kama siku ile. Kila mtwana aliyekuwa pembeni yake aliingiwa na mchecheto wa kuhofia maisha yake.
Malkia Huleiya baada ya kuona mwili wa Soba ukianguka chini kama gunia na kichwa kikigaagaa chini, alishtuka kwa kuona ameua, alilitupa upanga chini kisha aliangua kilio na kukimbilia chumbani. Kila tukio lililotokea muda ule lilimshangaza kila mmoja.
Mfalme alijikuta amebaki amesimama kama sanamu asielewe kilichotokea ni kweli au alikuwa akiota. Ulikuwa mwaka wa sabini na tano toka amuoe mkewe aliyekuwa msikivu na mtulivu pia mnyenyekevu kwa mumewe muda wote. Malkia Huleiya siku zote alikuwa kiumbe mwenye huruma na kumkanya mumewe pale anapotumia nguvu bila kutumia muda wa kufikiri katika maamuzi yake ya kutoa adhabu kwa majini yanapofanya kosa.
Lakini siku ile kwa mara ya kwanza alifanya kitendo kilichomshtua kila mmoja aliyemfahamu. Hata adhabu anapotoa mfalme, yeye ndiye aliyesimama kutetea.
Lakini kitendo cha kutenganisha kichwa na kiwiliwili cha jini hakuwahi kukifanya zaidi ya mumewe ambaye kila alipokosewa adhabu yake kubwa ilikuwa kutenganisha kichwa na kiwiliwili.
Kitendo cha mkewe kumuua mtwana mkuu msaidizi aliyekuwa akitegemewa na mfalme baada ya Kulani kuwa kipofu kilimfadhaisha sana.
Alitoka sebuleni na kumfuata mkewe aliyekuwa amejitupa kitandani akilia kwa uchungu huku akijutia kitendo cha kumuua Soba.
Japo Soba alionesha jeuri lakini moyoni alijuta kwa uamuzi mzito alioutoa kwa kumtenganisha kichwa na mwili.
“Malkia wangu,” mfalme Balami alimwita mkewe kwa sauti ya upole.
“Nisamehe mume wangu, nimeshindwa kuzuia hasira zangu, yote ni kwa ajili ya mapenzi mazito kwa mwanetu wa pekee Balkis.”
“Najua mke wangu, lakini kitendo chako kimenifanya nijione nina mke mwenye maamuzi mazito.”
“Hapana sikutarajia kutoa uamuzi mzito kama ule, lakini yote umeyasababisha wewe.”
“Hapana mke wangu, ningejuaje uwezo wa maamuzi yako bila kufanya vile?”
“Si kwa kutoa roho ya kiumbe kisicho na hatia.”
“Ile imeonesha kumbe hata nikiondoka au nikifa hakuna mtu wa kukuchezea, kwa kitendo kile Balkis namtoa kwenye chumba cha giza pia kumrudisha duniani mchumba wake bila masharti.”
“Unasema kweli?” Malkia Huleiya alishtuka kusikia kauli ya mumewe.
“Kweli kabisa, hii itakuwa kama zawadi kwa ujasiri uliouonesha mbele yangu.”
“Asante mume wangu kwa uamuzi wako uliorudisha furaha yangu.”
“Si kurudisha furaha yangu tu bali kuendelea na msimamo huo huo ili kuongeza heshima ndani ya himaya yangu.”
Baada ya makubaliano alitumwa kibaraka kwenda kumtoa Balkis kwenye chumba cha giza lakini aligoma kutoka kama hawatamuachia Brighton. Waliamuliwa kwenda kuwatoa wote, walifanya hivyo na Balkis alikubali kutoka ndani ya chumba cha giza.
Pia alitoa masharti kuwa, kabla ya kuzungumza lolote wahakikishe Brighton anatolewa chini ya maji na kurudishwa duniani. Kwa vile uamuzi ulikuwa amepitishwa ombi lake halikupingwa na baba yake. Lakini kabla ya kurudishwa duniani Brighton alipewa masharti na mfalme kuwa siku atakayoitoa siri ya majini ndiyo siku ya mwisho ya uhai wake.
Baada ya kukubaliana na masharti, Brighton alisindikizwa na watwana kumi baada ya kumfikisha pembeni mwa bahari walimlaza pembeni. Ubaridi wa alfajiri na maji vilimfanya Brighton ashtuke na kujikuta amelala ufukweni, miguu ikiwa majini na mwili nchi kavu. Baada ya kunyanyuka alipokuwa amesimama kwa mshtuko. Aliifahamu sehemu ile ilikuwa ni eneo la daraja ya Salenda.
Baada ya kujinyanyua alipokuwa amekaa, alitembea kuelekea barabarani ili apate lifti ya kumrudisha kwake.
Je, kurudi kwa Brighton ndiyo mwisho wa Balkis kuchukua wanaume wa kibinadamu?
Post a Comment