KAJALA:NILIKAA DAWATI MOJA NA WATOTO WA RAIS JK
Kwa kuanzia, tunaye nyota wa filamu za hapa nyumbani, Kajala Masanja, ambaye kabla ya kujiingiza kwenye sanaa hiyo aliwahi kuishi kinyumba na mmiliki wa studio ya Bongo Records, Paul Matheas, maarufu kama P.Funk na kujaaliwa kupata mtoto mmoja aitwaye Paula.
Katika safu hii, Kajala ambaye amewahi kukutwa na misukosuko lukuki ikiwemo kuhukumiwa kifungo jela, anaelezea mambo mengi kuhusiana na maisha yake ambayo hakuwahi kuyaelezea kokote kule au katika chombo chochote cha habari.
“Nilizaliwa mwaka 1983 katika familia ya mzee Masanja na walijaaliwa kuwa na watoto wawili tu, mimi na mdogo wangu, Dorice. Sisi tuna tofauti kubwa sana ya umri kati yetu kwa vile tulipishana sana kuzaliwa. Wakati nikizaliwa, wazazi wangu ambao wote ni askari polisi, walikuwa wakifanya kazi na kuishi kituo cha Oysterbay jijini Dar es Salaam.
“Baada ya kuandikishwa Shule ya Msingi Mbuyuni, siku ya kwanza
niliyotakiwa kwenda niliamka asubuhi na mapema na dada aliyekuwa
akinilea alinivalisha nguo za shule na kunitaka sasa kusubiri chai kabla
ya kunipeleka shuleni.
“Wakati dada akiipua chai ili animiminie kwenye kikombe, kwa bahati
mbaya ilinimwagikia mapajani na kuniunguza sehemu kubwa ya mapaja yangu.
Ikabidi wazazi wangu wafuatwe kituoni hasa kwa kuwa hakukuwa mbali na
nyumbani, ambao walifika na kunipeleka hospitalini. Ndoto ya kusoma
ikaishia hapohapo!
“Nilipofika hospitali, walinipa dawa na kila siku nilikuwa nikienda
kuosha kidonda, hamu ya shule ikaniishia, nikawa mtu wa kulala tu, maana
hata kutembea nilikuwa siwezi, kwani nilipohitaji kutembea nilibebwa na
kufanyiwa kila kitu hadi nilipopata nafuu.
“Hali yangu iliendelea kuimarika hadi nilipopona kabisa na kuanza
kwenda shuleni, ambako nilikutana na watoto wenzangu ambao tukajikuta
tukijenga urafiki. Nilikuwa mpole mno, sikuwa mtu wa kuongea kabisa na
mara nyingi watoto wenzangu wakorofi walipenda sana kunichokoza.
“Wakati huo nikisoma, mwalimu wangu wa darasa alikuwa Mama Salma
Kikwete ambaye sasa ni first lady na nilikaa dawati moja na watoto wa
Rais Kikwete, Ridhiwan na Miraji na kwa kweli walikuwa ni marafiki zangu
wakubwa sana.
“Nakumbuka nilipofika darasa la sita, kuna msichana mmoja alipanga
kunipiga yeye na marafiki zake kwa madai kuwa mimi nimemchukulia mchumba
wake, maana kipindi hicho ni wadogo na kutokana na upole wangu
niliwaambia mimi sijafanya hivyo wakaniambia kesho yake lazima wanipige,
maana enzi hizo tukitaka kupigana, lazima iwe Ijumaa.
“Siku hiyo ilipofika, mama alikuja kuniamsha asubuhi kwa ajili ya
kwenda shuleni, nikajifanya nimebanwa na tumbo, siwezi kuamka wala
kutembea, akanitafutia dawa na kunipa ninywe kisha akaniambia nilale.
Nilishukuru sana kwani siku hiyo niliepuka kipigo.
“Ilipofika Jumatatu nikaendelea na mambo yangu kama kawaida wala
hawakunisemesha tena, lakini nilikuwa muoga sana, nilijua wakati wowote
wanaweza kunivizia na kunipiga, lakini haikutokea ingawa hata mimi
rafiki zangu walikuwa wamejipanga kwa ajili ya kujibu mashambulizi.
“Niliendelea kusoma shuleni hapo kwa amani mpaka nilipomaliza darasa
la saba. Wakati huo nilikuwa na rafiki yangu mmoja wa kiume ambaye kila
siku jioni alikuwa akipita nyumbani. Baba yangu akamshtukia, siku moja
alichukua manati yake aliyokuwa akiitumia kuwapigia kunguru, alipopita
akampiga nayo!
“Kufuatia kitendo hicho, rafiki yangu yule hakupita tena nyumbani na
akatokea kunichukia sana kwa ajili ya kitendo alichofanyiwa, wakati wa
kuanza sekondari ulipofika, nilipelekwa Songea katika shule ya masista
kwa hofu kuwa nikisoma mjini nitaharibika kimaadili.
“Nilipoanza masomo shuleni hapo, nilikuwa mpweke sana maana sikuwahi
kukaa mbali na wazazi wangu, halafu kulikuwa na baridi sana kitendo
kilichosababisha nisiwe naoga kabisa na kujikuta nikipata ukurutu kwa
uoga wa kuoga maji ya baridi.”

Post a Comment