Tukaishangilie kwa nguvu Azam FC leo.
Azam FC inaingia Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni
kupambana na Barrack Young Controllers ya Liberia katika mchezo wa
marudiano Kombe la Shirikisho.
Wawakilishi hao pekee wa Tanzania katika michunao ya Klabu Afrika, wanaingiwa uwanjani wakiwa na faida ya mabao mawili iliyopata ugenini katika mchezo wa kwanza, Liberia.
Hivyo basi, ili kusonga mbali hatua ya 32 bora, Azam wanahitaji sare ya aina yoyote katika mtanange huo unaotarajiwa kuanza jioni saa 10. Katika mchezo wa kwanza, Azam ilishinda mabao 2-1.
Azam ilifanikiwa kusonga mbele baada ya kushinda mchezo wa kwanza dhidi ya Al Nasri ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 8-1, baada ya kushinda mabao 3-1, Dar es Salaam na kisha kushinda 5-0 kwenye mechi ya marudiano ugenini Juba.
Pamoja na kumbukumbu hiyo nzuri ya ushindi wa
ugenini, bado Azam wana kazi kubwa ya kufanya kuweza kuitoa nje ya
mashindano timu hiyo ya Liberia ambayo hakuna shaka imepania kulipa
kisasi.
Ndiyo maana tunawaomba mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi kuishangilia Azam, huku pia suala la uzalendo likipewa kipaumbele kikubwa.
Mara nyingi mashabiki wa soka nchini wamekuwa na kasumba ya kushangilia timu ngeni hasa kwenye mashindano ambayo timu za Simba na Yanga zimekuwa zikishiriki. Utamaduni huu siyo tu kwamba umekuwa ukilitia aibu taifa, pia umechangia kuzivunja moyo timu za nyumbani na kiasi cha kuonekana kama vile zinacheza ugenini na siyo kwenye viwanja vyao vya nyumbani.
Imezunguzwa sana athari za vitendo vya kukosa uzalendo, na leo tunarudia tena kuwataka mashabiki wa soka kijitokeza kwa wingi kuishangia Azam ili iweze kukamilisha vizuri safari ya ushindi.
Tunatarajia Watanzania wengi watajitokeza uwanjani kesho kuishangilia Azam na kuiongezea nguvu kwa sababu inawakilisha nchi kimataifa baada ya wawakilishi wengine Simba kutolewa raundi ya kwanza kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
Tukijitokeza kwa wingi katika mechi dhidi hii,
maana yake tunawatia nguvu vijana wetu wa
Azam kucheza kwa moyo na ari ya kujituma kupata ushindi kwenye uwanja wa nyumbani.
Azam kucheza kwa moyo na ari ya kujituma kupata ushindi kwenye uwanja wa nyumbani.
Kwa upande wa wawakilishi hao, tunaamini
watahakikisha wanalipigania taifa letu leo kwa hali na mali, kwa kucheza
kitimu, kujituma, kutengeneza nafasi nyingi za ushindi.
Wachezaji wa Azam wakiwa umakini na watulivu
uwanjani kwenye mchezo wa leo, hapana shaka kwamba wataandika ushindi
mnono kama ilivyofanya dhidi ya timu ya Al Nasri ya Sudan Kusini.
Wachezaji watakaochaguliwa kuvaa jezi kwenye mchezo huo, ni
lazima waone sifa na kucheza kwa kujituma siyo kwa faida ya Azam, bali
ya Watanzania wote wapenda michezo.
Tunasema hivyo kwa sababu tunafahamu wapinzani wa
Azam pamoja na kupoteza mchezo wa kwanza wakiwa nyumbani, lakini bado
siyo timu ya kubeza hata kidogo.
Kama ambavyo wenyewe wamesema kuwa wamekuja kulipa
kisasi, ndivyo Azam wanatakiwa kuichukulia kauli hiyo kwa tahadhari
kubwa ili kuepuka kufanya makosa yanayoweza kuwapa ushindi wapinzani
wao.
Azam wasiingie uwanjani na kujiona kama vile
tayari wameshashinda mchezo huo, bali wajione wana deni la kushinda
mabao mengi zaidi.
Tunaitakia Azam FC kila la kheri.

Post a Comment