Sumatra: Ulevi unasababisha ajali kwa 76%
MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra)
imebaini kuwa asilimia 76 ya ajali za barabarani zinasababishwa na
matatizo ya kibinadamu, ukiwemo ulevi na uzembe wa madereva.
Takwimu hizo ni kwa mujibu wa utafiti walioufanya mwaka 2007 katika
kutafuta chanzo cha ajali nyingi za barabarani ambazo zimekuwa
zikitokea mara kwa mara.
Pamoja na matatizo hayo, pia utafiti huo ulibaini uchakavu na ubovu
wa magari kuwa unachangia kwa asilimia 16 na ubovu wa barabara ni
asilimia 8.
Kaimu Mkurugenzi wa Sumatra, Ahmed Kilima alitoa takwimu hizo wakati
wa hafla fupi ya mamlaka hiyo kukabidhi kwa Jeshi la Polisi vifaa vya
kupima ulevi kwa madereva 2,000 wa vyombo vya usafiri.
Alisema kuwa vifaa hivyo si vya muda mrefu, lakini wako mbioni
kutafuta vya kudumu ili kupunguza ajali za barabarani zinazotokana na
ulevi.
Kilima alisema vifaa hivyo vitawasaidia kuwakamata madereva kabla
ajali hazijatokea, kwani wengi wamekuwa wakinywa pombe kwenye chupa za
maji na kusingizia kuwa ni maji.
Alisema kuwa vifaa hivyo vimegharimu sh milioni 12, lakini kwao
hawajali gharama za ununuzi bali wanachotaka ni kuhakikisha Watanzania
wako salama.
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema alisema kuwa anaamini
vifaa hivyo vitafanya vizuri katika kupunguza ajali za barabarani kama
walivyofanya vizuri na kamera walizopewa na Sumatra miaka ya nyuma.
Alisema kuwa vifaa hivyo vimesaidia kujibu moja ya malengo ya Jeshi
la Polisi ambalo ni kukinga ajali isitokee na vile vile kusaidia
kudhibiti uhalifu.
IGP Mwema alisema kuwa katika kuhakikisha usalama barabarani jeshi
hilo litashirikiana na Sumatra kuziwekea namba pikipiki za abiria
maarufu kama bodaboda, zitakazozitambulisha mikoa zinakotoa huduma kama
ilivyo kwenye gari ndogo (teksi).

Post a Comment