ad

ad

Ferguson agoma kumpumzisha Van Persie.

MANCHESTER, ENGLAND
HAPUMZISHWI kamwe! Ndivyo ambavyo Sir Alex Ferguson anavyosema kuhusu kukauka kwa mabao ya mshambuliaji wake, Robin Van Persie, ambaye inadaiwa amechoka kutokana na kucheza mechi nyingi mfululizo.

Nyota huyo aliyenunuliwa kwa pauni 25 milioni kutoka Arsenal Agosti mwaka jana, ameshindwa kufunga bao lolote katika mechi tisa zilizopita huku akinyang anywa bao lake dhidi ya Sunderland ambalo limeingizwa katika orodha ya mabao ya kujifunga.

Mapema wiki hii, Ferguson, alikiri kwamba staa huyo wa Kidachi mwenye umri wa miaka 29 ameanza kuchoka baada ya kuanza maisha ya Old Trafford kwa kiwango cha ajili ya juu. Hata hivyo kocha huyo amesema kamwe hatampumzisha.

"Robin hahitaji kupumzika. Nina uhakika na hilo. Ni kijana imara na ana nguvu sana. Mabao yatarudi tena kwake, washambuliaji wote huwa kuna vipindi wanakaukiwa mabao. Ni sehemu ya kuwa mshambuliaji," alisema.

"Wakati nikiwa mshambuliaji sikuwa nakaukiwa mabao, lakini inabidi upitie kipindi hicho na usipoteze kujiamini kwako. Baba yangu aliniambia siku zote hakikisha unauweka mpira wavuni ukiwa maeneo ya lango.

"Kama kipa akiokoa unaweza kusema bonge la kipa. Lakini kama ukijaribu kufanya mbwembwe akaudaka lazima utakosolewe."

Bao ambalo Van Persie alionekana kama amefunga dhidi ya Sunderland limehesabiwa kuwa la kujifunga kwa beki, Titus Bramble na hivyo inamfanya Van Persie asiwe amefunga tangu Februari 10 mwaka huu.

Hata hivyo, Ferguson ameligeuzia macho pambano la keshokutwa Jumatatu dhidi ya wapinzani wao Manchester City huku akipiga mkwara kuwa hawatapoteza pambano hilo.

"Ni mechi kubwa kwa City, watataka kuja kutuabisha.

Naweza kuelewa changamoto inayowakabili, hata na sisi tutakuwa na changamoto hiyo hiyo. Lakini tupo nyumbani na kila mtu anajionea jinsi tunavyocheza vizuri kila siku," alisema.
Powered by Blogger.