ad

ad

Nigeria na Burkina Faso zatinga nusu fainali

Nigeria na Burkina Faso zatinga nusu fainali; Ivory Coast na Togo zafungasha virago
Timu za taifa za Nigeria 'Super Eagles' na Burkina Faso zimefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya kombe la Mataifa ya Afrika inayoendelea kurindima nchini Afrika Kusini. Nigeria imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kuichabanga Ivory Coast kwa mabao 2-1. 

Ilikuwa Nigeria iliyoanza kuzifumania nyavu za Ivory Coast 'The Elephants' katika dakika ya 43 kwa bao lililofungwa na mshambuliaji Emanuel Emenike. Kipindi cha pili kilipoanza Ivory Coast walicharuka na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha lililopachikwa na mchezaji wa kiungo Cheikh Tiote katika dakika ya 50. Hata hivyo, Sunday Mba aliifanikiwa kumuangusha 'mnyama' na kumchinjia baharini katika dakika ya  78.
Nigeria itakwaruzana na Mali katika hatua ya nusu fainali siku ya Jumatano.

Mali ilifanikiwa kupata tiketi ya kucheza nusu fainali baada ya kuwatoa wenyeji, Afrika Kusini kwa mikwaju ya penalti baada muda wa kawaida na wa nyongeza kwa timu hizo  kufungana bao 1-1. Kwenye mikwaju ya penalti, Mali ilipachika mabao 3 na Afrika Kusini bao 1. Hivyo Mali ilisonga mbele kwa jumla ya mabao 4-2.

Katika mtanange mwengine wa robo fainali, Burkina Faso imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kuibwaga Togo kwenye mechi ngumu iliyotawaliwa na ubabe na wachezaji kurushiana madaruga. Kwenye mchezo huo, Burkina Faso imeweza kuinyoa Togo kwa bao 1-0. Hadi dakika ya 90 ya mchezo hakuna timu iliyoweza kutoboa nyavu za timu pinzani, na muda wa nyongeza wa dakika 30 ziliweza kuamua nani anasonga mbele. Jonathan Pitroipa aliipatia Burkina Faso bao pekee katika dakika ya 105 ya mchezo. Wachezaji sita wa Togo na wawili wa Burkina Faso walionyeshwa kadi za njano kwa kucheza rafu.
Kwa matokeo hayo, Burkina Faso itakwaruzana na Ghana siku ya Jumatano kwenye mchezo wa nusu fainali.
Ghana walifanikiwa kutinga nusu fainali baada ya kuifunga Cape Verde mabao 2-0 kwenye mchezo wa robo fainali.
Powered by Blogger.