SI KITU BILA PENZI LAKO -01
NYEMO CHILONGANI
Hali ya hewa tayari ilianza kubadilika, jua kali lililokuwa likiwaka kipindi kichache kilichopita likapotea na mawingu mazito kutanda angani. Kila mtu alionekana kuogopa kwani kwa jinsi mawingu yale yalivyokusanyika angani, kila mmoja akahisi kwamba mvua kunbwa ingenyesha.
Wale waliokuwa mashambani mwao, wakaanza kuondoka, waliokuwa njiani, wakaanza kukimbia kuelekea makwao na hata wale waliotaka kutoka katika nyumba zao, waliva makoti makubwa kwa kuamini kwamba uwepo wa mawingu hayo angani ungesababisha mvua kubwa kunyesha.
Mbali na mawingu hayo mazito, upepo mkali ukaanza kuvuma, watu wakaogopa zaidi kwa kuona kwamba mvua ambayo ingetarajia kunyesha kipindi kichache kijacho ingekuwa mvua kubwa ambayo haikuwahi kutokea katika mkoa mzima wa Shinyanga.
Wakati hali ya hewa ikibadilika, katika uwanja wa mpira wa Makao uliokuwa katika Kijiji cha Chibe mkoani Shinyanga, Mchungaji wa Kanisa la Praise And Worship la jijini Dar es Salaam, Emmanuel Zakayo alisimama katika jukwaa la uwanja huo na kuhubiri neno la Mungu.
Watu walikuwa kimya wakimwangalia, mahubiri aliyokuwa akiyatoa katika mkutano huo yaliwatia nguvu watu wote waliokuwa wakimsikiliza, wengine waliumizwa na kujikuta wakibubujikwa na machozi.
“Mungu anakupenda, hawezi kukuacha ukiteseka milele, hakukuumba uje kuteseka duniani, kila unalopitia ni jaribu lako ambalo Yeye atakushika mkono katika njia zote ngumu unazopitia,” alisema mchungaji Zakayo.
Wakati mahubiri yakiendelea, mvua kubwa ikaanza kunyesha, hakukuwa na mtu aliyediriki kuondoka uwanjani hapo, wote walisimama na kuendelea kumsikiliza. Mvua haikuwa kitu kwao hasa katika kipindi kama hicho, walikuwa tayari kulowa lakini si kuondoka uwanjani hapo.
Miongoni mwa watu waliokusanyika katika mkutano huo alikuwa mzee Innocent. Mzee huyu alikuwa mtu masikini, asiyekuwa na kitu chochote kile. Muda wote machozi yalikuwa yakimtoka, aliumizwa na maneno ya mchungaji na wakati mwingine alihisi kama alikuwa akiambiwa yeye.
Mavazi yake tu yalionyesha kwamba alikuwa mtu masikini, nguo zake zilichanikachanika, alikuwa mchafu, nywele zake zilikuwa timutimu. Mzee Innocent hakuwa peke yake, aliambatana na familia yake, mke wake, Anna na mtoto wake Patrick.
Hata nao ukiwaangalia, hawakutofautiana na mzee huyo, mavazi yao yalichoka na walionekana ni jinsi gani walipigwa na maisha ya kimasikini. Mkewe, Anna alionekana kuumizwa zaidi na maneno ya mchungaji, machozi yalikuwa yakitiririka kila wakati mashavuni mwake.
“Mungu anaposema kwamba atasimama pamoja nawe, hadanganyi, Mungu si binadamu mpaka aseme uongo. Wewe kama mwanadamu, weka tumaini lako kwake kwani yeye mwenyewe amesema na alaaniwe amtegemeaye mwanadamu. Mganga hatoweza kukusaidia, msaada wako pekee upo kwa Mungu aliye hai,” alisema mchungaji huyo.
Mahubiri yaliendelea mpaka ilipofika saa kumi na mbili kamili, mchungaji akahwaita watu wanaotaka kufanyiwa maombezi na kwenda mbele. Mzee Innocent na familia yake walikuwa miongoni mwa watu hao, walipofanyiwa maombezi, wakataka kuzungumza na mchungaji.
“Kijiji kizima kimetutenga, wanatuita wachawi kwa sababu ya macho yetu, mchungaji, tunaomba utuombee, watatuua,” alisema mzee Innocent.
“Mungu ndiye mwenye uwezo wa kuumba na kuua, Mungu anaposema hufi, hautokufa hata binadamu afanye nini,” alisema mchungaji Zakayo na kuwataka wapige magoti, hapohapo akaanza kuwafanyia maombezi na kisha kuwaruhusu kuondoka.
*****
Hali ilikuwa inatisha mkoani Shinyanga hasa katika vijiji mbalimbali. Watu wengi walikuwa wakiuawa kila siku kutokana na imani za kishirikina. Wanakijiji wenye hasira walivamia katika nyumba za wanakijiji wengine na kuwaua kwa mapanga na hata kuzichoma moto nyumba zao.
Idadi kubwa ya watu waliokuwa wakiuawa ilikuwa ikiongezeka kiasi kwamba serikali ikaamua kuweka ulinzi wa kutosha katika vijiji mbalimbali. Hiyo haikusaidia, hiyo haikusimamisha mauaji hayo, mara kwa mara taarifa za watu kuuawa kwa kuhisiwa kwamba ni wachawi ziliendelea kuripotiwa kitu kilichowafanya watu wengine kuhisi kama huko Shinyanga ilikuwa jehanamu au uwanja wa machinjio.
Familia ya mzee Innocent ilikuwa familia pekee iliyokuwa imetengwa katika Kijiji cha Chibe. Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alilisogelea eneo la nyumba yao, macho yao mekundu ndiyo yaliyowafanya watu kuona kwamba watu hao walikuwa wachawi.
Ingawa walikuwa wakielekea katika kanisa la kijiji cha Beda lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyewaamini, kila siku watu waliwaona kuwa wachawi ambao walikuwa wakitumia dini kama mwamvuli wa kufunika maovu ambayo walikuwa wakiyafanya.
Hawakushirikishwa katika kikao chochote kijijini hapo, na kama ilitokea wakashiriki, basi kila mtu alikuwa akiondoka na kuwaacha peke yao. Maisha yakawa magumu, hawakuwa na raha hata kidogo, masengenyo ndiyo ambayo walikuwa wamezoea kuyasikia kutoka kwa wanakijiji wenzao.
Roho za chuki zilikuwa zikizidi kuongezeka juu yao. Walikuwa wakichukiwa na wanakijiji wenzao kuliko mtu yeyote yule. Maisha yao yalikuwa ya shida sana kiasi ambacho mara kwa mara walijiona kuwa na kila hali ya kuomba msaada lakini hawakufanya hivyo.
Hawakuona kama kulikuwa na mtu angekuwa tayari kuwasaidia kwa msaada wa aina yoyote ile. Walikaa peke yao, hawakutaka shida zao kuwatangazia watu wengine. Kila siku walizidi kumwomba Mungu ili abadilishe kila kitu lakini hakukuwa na kitu chochote kilichobadilika.
Kila kona walikuwa wakiitwa wachawi huku wakizomewa. Waliumia lakini hakukuwa na njia yoyote ya kuepuka maneno hayo. Kumtegemea Mungu na kumwombea Patrick afanikiwe maishani mwake ndiyo kitu walichofanya kila siku maishani mwao.
“Mtoto mchawi anapita,” sauti ya mwanafunzi mmoja wa kike ilisikika akiwaambia wenzake katika kipindi ambacho Patrick alikuwa akipita karibu yao.
Patrick akaumia mno. Akageuka nyuma na kuwaangalia wasichana wale, wote walikaa kimya. Alipogeuka na kuendelea kupiga hatua, sauti ya vicheko vya zikaanza kusikika tena kutoka kwa wasichana wale. Patick akashindwa kuvumilia, akapiga hatua za haraka haraka kuelekea nyuma ya darasa alilokuwa akisoma na kuanza kulia.
Shuleni hakuwa na raha hata kidogo, kila siku alikuwa mtu wa majonzi tu. Hakukuwa na mwanafunzi aliyekuwa akiongea naye shuleni. Katika darasa alilokuwa akisoma, hakukuwa na mwanafunzi yeyote aliyekuwa akikaa pamoja naye.
Kutengwa kwake hakukuwa kwa wanafunzi tu, bali hata walimu walikuwa wakimtenga. Darasani hakuwa akichaguliwa kujibu swali lolote hata kama alinyoosha mkono, madaftari yake hayakukusanywa wala kusahishwa. Hakukuwa na aliyempenda Patrick, alionekana chukizo mbele yao kutokana na imani ya kishirikina ambayo ilikuwa imejengeka katika vichwa vyao juu ya familia yake.
Kila siku Patrick alikuwa mtu wa kusoma tu kwa kuamini kwamba hapo ndipo yalipokuwa maisha aliyoyatamani kila siku. Hakupenda kabisa wazazi wake waendelee kuishi katika nyumba ya udongo kama waliyokuwa wakiishi, alitamani asome kwa bidii, apate fedha na kuwatengenezea wazazi wake nyumba nzuri iliyokuwa na bati pamoja na umeme.
Mitihani ya kumaliza elimu ya msingi tayari ilikuwa imemalizika na katika kipindi hicho wanafunzi wote wa vijiji vya karibu na kijiji cha Beda ambacho hakikuwa mbali sana na kijiji chao cha Chibe walikuwa wamekusanyika katika ukumbi mmoja mkubwa uliotengenezwa kwa udongo wa mfinyanzi kwa ajili ya kusherehekea mahafali yao.
Wanafunzi zaidi ya elfu mbili walikuwa wamekusanyika wakicheza muziki ambao ulikuwa ukisikika ukumbini hapo. Ingawa kila mwanafunzi alikuwa na furaha mahali hapo, Patrick alionekana kuwa tofauti kabisa. Alikuwa amekaa pembeni huku akichorachora chini.
Wanafunzi aliomaliza pamoja nao, hawakutaka kabisa kumsogelea, kila mmoja alimuogopa. Kadiri muda ulivyozidi kwenda na ndivyo hali ilivyozidi kubadilika, jua likazama na hatimaye kwa mbali kigiza kuanza kunyemelea.
Bado Patrick alikuwa amekaa katika jiwe lililokuwa pembeni, mara akashtuka baada ya kuona mtu akiwa amesimama mbele yake. Akaanza kuyapandisha macho yake juu, akakutana na uso wa msichana ambaye hakuamini kama angeweza kukutana naye katika maisha yake.
Akabaki akimwangalia msichana huyo, machoni mwake alikuwa mgeni kabisa, na alijua fika kwamba msichana huyo alikuwa mwanafunzi kutoka katika shule nyingine ambazo zilikuwa zimekusanyika mahali yapo kwa ajili ya kusherehekea mahafali ya kumaliza darasa la saba.
Patrick akauhisi moyo wake kufa ganzi, damu ikaanza kuzunguka kwa kasi ya ajabu katika mishipa yake hali iliyopelekea moyo wake kudunda kwa kasi huku kijasho chembamba kuanza kumtoka kwa mbali.
“Naomba tukacheze muziki,” msichana huyo, mwenye sura iliyojaa tabasamu alimwambia Patrick ambaye alibaki akimshangaa tu.
*****
Bi Anna alionekana kuwa na hofu kubwa moyoni mwake, muda ulikuwa umekwenda sana lakini mtoto wake mpendwa, Patrick hakuwa amerudi nyumbani. Mapigo yake ya moyo yalikuwa juu na muda mwingi alitoka nje na kuangalia huku na kule kuona kama Patrick alikuwa akirudi lakini hakuweza kumuona.
Hofu yake ilikuwa juu kwa sababu ya mauaji yaliyokuwa yakiendelea kutokea katika vijiji mbalimbali. Alichohisi ni kwamba mtoto wake alikuwa ameuawa na wanakijiji ambao hawakuwa wakiwawapenda kitu kilichomfanya machozi kuanza kumbubujika mashavuni mwake.
Mumewe aliligundua hilo, alimwangalia mke wake kwa macho yaliyojaa huruma nyingi, hakupenda kumuona mke wake akiwa katika hali hiyo, alimpenda na alitamani kumuona akiwa na furaha siku zote za maisha yake.
“Vipi tena mke wangu?” mzee Innocent alimuuliza mkewe, Bi Anna.
“Patrick mpenzi.”
“Patrick! Amefanya nini?”
“Hajarudi mpaka sasa. Nina wasiwasi mpenzi,” Bi Anna alisema huku akionekana dhahiri kuwa na wasiwasi.
“Wasiwasi wa nini tena?”
“Wanaweza wakawa wamemuua. Hebu fikiria, saa mbili usiku sasa bado hajarudi. Watakuwa wamemuua mwanangu. Ni bora ...” alisema lakini hata kabla hajamalizia sentensi yake akaanza kulia.
Moyo wake ulikuwa umeumia mno, tayari aliona kuwa Patrick alikuwa ameuawa. Amani yote iliyokuwa moyoni mwake ikapotea kabisa. Akaanza kulia kama mtu aliyekuwa akiomboleza. Mzee Innocent akawa na kazi kubwa ya kuanza kumbembeleza. Hakuna kitu kilichosaidia, bado Bi Anna alikuwa akiendelea kulia.
“Kulia hakutasaidia mke wangu. Patrick bado ni mzima, inatubidi tuanze kumuomba Mungu amlinde huko alipo,” alisema mzee Innocent.
Akamuinua na kumshika mikono. Hawakuwa na tumaini lolote katika maisha yao zaidi ya kuanza kumkabidhi Patrick mikononi mwa Mungu ili amlinde. Sala ilikuwa ikiendelea zaidi na zaidi. Bado walikuwa wakimwamini Mungu kwamba alikuwa na uweza mkubwa wa kumlinda kule alikokuwa na kumnusuru na mauti yoyote iliyokuwa imepangwa.
Huku wakiwa katikati ya sala, wakapigwa na mshtuko mara baada ya kuona vitu kama maji vikiwa vimewamwagikia. Kwa kutumia mwanga hafifu wa koroboi, wakaanza kuviangalia vimiminiko vile kwa makini, wakavinusa na kugundua kwamba ni mafuta ya petroli.
“Mungu wangu! Petroli,” mzee Innocent alimwambia mkewe huku petroli ile ikizidi kumwagiwa katika nyumba ile.
Minong’ono ya watu ikaanza kusikika kutoka nje ya nyumba ile hali ambayo ilionekana kuwatia wasiwasi. Huku akionekana kujiamini, mzee Innocent akaufungua mlango na kuchungulia nje, akashtukia akipigwa na kitu kizito usoni kilichomfanya kuangukia ndani huku damu zikianza kumtoka usoni.
Bi Anna alichanganyikiwa, hata kabla hajajua ni kitu gani alichotakiwa kukifanya, akashtuka alipoona nyumba hiyo ya nyasi ikianza kuteketezwa kwa moto. Bi Anna akabaki akilia huku akimuinua mumewe, tayari waliuona mwisho wa maisha yao ukiwa umekaribia, sala zote ambazo walikuwa wakisali katika kipindi cha nyuma, wakaonekana kusahau.
“Inuka mume wangu ...tunakufa mume wangu...” Bi Anna alimwambia mumewe huku akilia.
Vicheko na sauti za kushangilia zikaanza kusikika nje ya nyumba yao huku moto ukiendelea kuiteketeza nyumba ile. Mzee Innocent akainuka huku akianza kuyumbayumba kama mtu aliyelewa. Akamwangalia mkewe, akajiweka sawa na kurudiwa na hali yake ya kawaida.
“Tunakufa mume wangu... tusali sala ya mwisho... wamekuja kutuua...” Bi Anna alimwambia mumewe huku akimshika mikono miwili.
“Hata kama tutakufa... naamini tutakwenda Mbinguni kupumzika,” mzee Innocent alimwambia mkewe, Bi Anna.
“Lakini vipi kuhusu mtoto wetu Patrick?” Bi Anna alimuuliza mumewe.
Taswira ya sura ya Patrick ikaanza kujijenga kichwani mwa mzee Innocent. Ni kweli aliuona mwisho wao kufikia tamati, lakini hakujua kama wangeuawa kwa wakati huo Patrick angebaki katika maisha gani duniani. Akajiona akipata nguvu, alitamani kutoka nje na kupambana na watu ambao walikuwa wamekuja kumvamia nyumbani kwake.
“Ni lazima nipambane nao...nitapambana nao kwa ajili ya Patrick,” alisema mzee Innocent na kutoka nje kwa lengo la kupambana na watu hao.
Bi Anna akabaki ndani akiwa anatetemeka, mara akaanza kusikia sauti ya mumewe ikilia kutoka nje, akatamani atoke nje na kumsaidia mumewe lakini kila alipotaka kufanya hivyo, aliogopa. Sauti ya mumewe iliendelea kusikika ikiomba msaada, lakini baada ya sekunde chache, sauti ile ikakatika na wala haikusikika tena. Bi Anna hakujua afanye nini, nyumba bado ilikuwa ikiendelea kuteteketea kwa moto.
“Bado mkewe na mtoto wake... tuingieni ndani na wao tuwaue,” sauti ya mwanaume mmoja ilisikika, Bi Anna akazidi kutetemeka kwa hofu.
Huu ni mwanzo wa hadithi yetu hii nzuri na ndefu.
Kuna mengi utajifunza, kuna mengi yatakuhuzunisha na kukufurahisha.
Hadithi itakayokutia nguvu ya kusonga mbele.
Hadithi ambayo itakuonyesha kwamba hata ukiwa masikini, bado Mungu anaweza kukuinua.
Huu ni mwanzo tu, ushirikiano wenu wa Share, Like, Comments kwa maoni ndiyo utaifanya simulizi hii kutoka katika siku
Post a Comment