ad

ad

Blati Touré Aachana na Pyramids, Atua Rasmi Al Ahli SC ya Libya

 


Kiungo wa kimataifa wa Burkina Faso, Blati Touré, ameaga rasmi klabu ya Pyramids FC baada ya kukamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Al Ahli SC ya Libya kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu.

Pyramids imethibitisha kuondoka kwa nyota huyo kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao yake ya kijamii, ikimpongeza na kumshukuru kwa mchango wake mkubwa alioutoa katika kipindi chote alichoitumikia klabu hiyo.

“Tunamshukuru Blati Touré kwa kujitoa kwake na utumishi wake wa miaka yote akiwa sehemu ya familia ya Pyramids, na tunamtakia kila la heri katika hatua mpya ya maisha yake ya soka,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Touré amekuwa mmoja wa viungo tegemeo ndani ya kikosi cha Pyramids, akijulikana kwa uwezo wake wa kulinda safu ya ulinzi, kupora mipira na kuanzisha mashambulizi kutokea katikati ya uwanja.

Kwa upande mwingine, Al Ahli SC ya Libya pia imetangaza rasmi usajili wake, ikimkaribisha kama sehemu ya mpango wa kuimarisha kikosi chao kuelekea mashindano yajayo ya ndani na kimataifa.

Nyota huyo wa zamani wa AFC Eskilstuna ya Sweden alijiunga na Pyramids mnamo Januari 2022, ambapo alicheza michezo kadhaa muhimu na kusaidia timu hiyo kufikia mafanikio mbalimbali katika ligi na mashindano ya bara Afrika.

Uhamisho wake unaonekana kuwa hatua mpya ya changamoto katika safari yake ya soka, huku mashabiki wa Al Ahli wakitarajia kuona uzoefu na ubora wake ukiongeza nguvu katika safu ya kiungo.

Kwa Touré, huu ni ukurasa mpya – lakini kwa Pyramids, ni mwisho wa enzi ya kiungo aliyekuwa mhimili muhimu wa timu.

No comments

Powered by Blogger.