ad

ad

Yanga Kutinga Robo Fainali, Kocha wa Al Ahly, Jess Thorup Awapania AS FAR

 

Kocha Mkuu wa Al Ahly, Jess Thorup, amesema hajafurahishwa na namna timu yake ilivyocheza katika mchezo wao wa hivi karibuni licha ya kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali, akisisitiza kuwa kiwango walichoonesha hakilingani na hadhi ya klabu hiyo kubwa ya Afrika.

Thorup amesema kufuzu ni jambo muhimu, lakini kwa upande wake bado anaamini kikosi chake kina uwezo mkubwa zaidi wa kufanya vizuri uwanjani.

“Sijaridhishwa na tulivyocheza leo… ni vile tumefuzu robo ambacho ndio ilikuwa muhimu,” alisema Thorup.

Kocha huyo ameweka wazi kuwa sasa macho yote yanaelekezwa kwenye mchezo ujao dhidi ya AS FAR, akieleza kuwa huo ni mtihani mwingine mkubwa ambao wanapaswa kuutumia kuthibitisha ubora wao na dhamira ya kweli ya kutwaa ubingwa.

Kwa mujibu wa Thorup, Al Ahly haitarajii matokeo ya kawaida bali wanahitaji ushindi wa wazi ili kuongoza kundi na kujiweka kwenye nafasi nzuri zaidi hatua zinazofuata.

“Jumapili tunacheza dhidi ya AS FAR na tutatakiwa kuonesha tupo serious na mashindano. Tunatakiwa kuamua tuongoze kundi na si vinginevyo,” aliongeza.

Ameongeza kuwa wachezaji wake wanapaswa kuingia uwanjani wakiwa na njaa ya ushindi na ari ya kupambana kwa dakika zote 90, akisisitiza kuwa hakuna nafasi ya kuridhika.

“Tutalazimisha kushinda na itatakiwa iwe hivyo… ni lazima tushinde.”

Kauli hiyo inaonesha wazi presha na matarajio makubwa yaliyopo ndani ya kikosi cha Al Ahly, timu ambayo imezoeleka kufanya makubwa katika mashindano ya kimataifa.

Mashabiki sasa wanasubiri kuona kama kauli ya kocha wao itageuka motisha kwa wachezaji na kuzaa matokeo chanya watakapovaana na AS FAR kwenye pambano lijalo.

No comments

Powered by Blogger.