ad

ad

NYUMA YA MACHOZI -19


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
“Mungu wangu! Amejua? Kwa nini tusimmalizie mbali?” “Tummalizie mbali nani?”
“Si Deus.”
“Kwa kosa gani?” “Si amejua.”
“Wala si hilo.”
“Picha ameziona?”
“Kilole hebu acha papala, yote unayouliza siyo.”
“Sasa nimekuweka kwenye wakati mgumu kivipi?”
SASA ENDELEA...
”Happy hanielewi kabisa, kila kukicha naitwa na familia yake naichenga, nikienda nitawaelezea nini wanielewe.”
“Kinape unakuwa kama siyo mwanaume, mwambie kuwa humtaki kwani mapenzi ni lazima.”
“Si rahisi kiasi hicho, kuvunjika kwa penzi kuna sababu huwezi kuzima chuma cha moto na maji baridi lazima kitapinda na Deus nitamwambia nini mtu niliyempeleka kwa wazazi wa Happy kumtambulisha kama kaka yangu?”
“Yote uliyataka wewe, kwa nini hukuniuliza kabla ya kwenda huko?”
”Kilole, wewe ni mke wa mtu na Happy ni mchumba wangu hivyo nilikuwa na haki ya kufanya vile.”
“Sasa Deus atakulazimishaje umpende Happy wakati humtaki?”
“Nitaanzia wapi ikiwa nilimweleza mengi juu ya mapenzi yangu ya dhati kwa Happy huku akiniahidi kusimamia harusi yangu. Kibaya zaidi Happy na wazazi wake watakuja hapa jioni ya leo ili kujua hatima ya ndoa.”
“Kwani wewe ulimjibu nini Happy?”
“Nilimueleza asubiri kidogo mzazi wangu mmoja alikuwa na matatizo.”
“Sasa yeye anataka nini na ulikwisha mweleza ukweli?”
“Anataka kwenda kumuona kwa vile anajua na yeye ni mzazi wake, pia muda wa kuwa naye umepungua si kama zamani. Kingine majibu yako ya mkato yamemshtua kitu ambacho kimemetia wasiwasi huenda tuna uhusiano wa kimapenzi.”
“Sasa akijua atafanya nini? Tena mweke wazi ili ajue hana chake.”
“Kilole acha kujisahau wewe ni mke wa mtu, kibaya kosa tunalifanya ndani ya kinywa cha simba. Hivi wakija hapa nitamwambia nini Deus na kwa vile huu ni mwisho wa wiki huenda akasema kesho tunakwenda kijijini. Siyo siri tabia ya Happy ilimvutia sana Deus na kusema atanipigania hata kwa fedha kuhakikisha namuoa, hivi niseme simtaki Happy nitaanzia wapi?”
“Kinape, Deus hawezi kukulazimisha kuoa mwanamke usiyempenda.”
“Unasema tu lakini kauli hiyo kwa mtu mwenye akili timamu hawezi kuitamka.”
“Kwa hiyo unamuogopa Deus?” “Ndiyo.”
“Kwa nini tusimpoteze?”
“Kilole acha papara nimekueleza tutajipanga.” “Nataka kukueleza kitu kimoja Deus ni kikwazo kwa nini mnamlea?”
“Tukifanya kwa pupa tutakosa mwana na maji ya moto.”
“Sasa tutafanyaje?”
“Nimekueleza niache niangalie tufanye nini?”
“Na kuhusu Happy najua ndiye anayeweza kuharibu kila kitu kama ataonekana kijijini?”
“Kwa kweli la Happy ndilo linalonichanganya nashindwa nifanye nini, nilipokutana naye leo nimechanganyikiwa jinsi alivyokonda kwa muda mfupi niliokuwa karibu yako na amenitishia nikimuacha lazima atajiua.” “Sasa akijiua wewe utapungukiwa nini, kwanza ndiyo itakuwa safi tunakuwa na nafasi ya kuishi wawili baada ya kumpoteza na Deus.”
“Siwezi kufanya hivyo, kama Happy atafariki basi nitakuwa na dhambi kubwa sana ambayo itakuwa kama tone la rangi nyekundu kwenye nguo nyeupe haitanitoka mpaka nitakapo ingia chini ya udongo.”
“Mmh! Sasa tutafanya nini?”
“Ndiyo maana nikasema umenipa mtihani mzito ambao sikuwahi kuusoma hata siku moja kwangu naona kiza. Kwa nini tusiachane na wazo kama hili?” ”Wazo gani?”
“Ukaniachana nioane na Happy na wewe unakie na Deus?”
“Kinape huwezi kunivisha kitanzi kisha uniweke juu ya donge la barafu likiyenyuka lazima nitakufa. Heri nife mimi kuliko kuendelea kuishi kwani naamini maisha yangu baada ya zile picha hayana thamani.
Kwa hiyo ulitaka kunidhalilisha ili ufurahi kwa vile nimeolewa na Deus kama kweli ulitaka niishi na Deus kwa nini ulinitendea unyama kama ule?”
“Happy..Ooh! Sorry Kilole mbona umekosa subira.”
“Nimekuelewa Kinape, tutazungumza kesho.”
Waliachana na Kilole alirudi chumbani akiwa amechanganyikiwa na kushindwa afanye nini juu ya picha mpya na habari za Happy.
Kilole baada ya kuachana na Kinape alirudi chumbani kwake na kujifungia kwa ndani, kila dakika iliyokuja mbele yake ilikuwa na maumivu makali yaliyomfanya akose jibu la haraka afanye nini. Kubakwa hakuona tatizo zaidi ya kusikia habari za Happy kupigania penzi lake ambalo ndilo lililomfikisha katika maumivu yale makali.
Alijiona mtu mmoja ambaye alikuwa akipigana na watu wengi bila msaada wa mtu mwingine, alijiuliza atawezaje kumdhibiti Happy kuhakikisha anampata Kinape mwanaume ambaye aliamini ndiye wa maisha yake.
Alichukua bahasha na kurudia kuangalia picha alizopigwa akibakwa na wanaume wawili kwa mpigo ambao hawakuonesha sura zao zaidi ya yeye peke yake.
Picha zile zilimchanganya sana na kuamini kama zitamfikia Kinape zitamweka katika mazingira magumu ambao utakuwa kama fimbo ya kumpigia ili kumuoa Happy.
Alipiga ngumi kwenye godoro kwa hasira baada ya kujiona yupo njia panda asijue aanze na kitu gani ili aweze kuyazima yote na mwisho wa siku awe na Kinape.
Akiwa katikati ya mawazo mlango uligongwa, alijua ni Kinape amekuja na wazo jipya, alikwenda hadi mlangoni na kufungua lakini alikuta ni mumewe ambaye alimchanulia tabasamu pana.
Kwa mshtuko aliufunga mlango haraka na kufunga na komeo, kwa haraka alichukua picha zake na kuzificha kisha alitoka hadi mlango ambako mumewe alikuwa bado amepigwa na butwaa.
“Ha! Kumbe ni mume wangu?” Alijifanya kushtuka.
“Unaniona sasa mwanzo ulifikiria nani?”
“Mmh! Hata sijui niseme nini, wakati unagonga mlango nilikuwa nimejinyoosha kitandani na kupitiwa na usingizi na kuota nimevamiwa na majambazi. Ulipogonga nilikuwa bado na usingizi nilipofungua na kukuona nilifikiri ni jambazi mpaka uliponiita na kuitambua sauti yako nisamehe mume wangu.”
“Kawaida, pole kwa ndoto mbaya.”
“Asante mume wangu.”
“Vipi mbona kama haupo sawa?”
“Mume wangu si nimekueleza naumwa, hata ndoto zangu zilikuwa za kutisha.” “Ooh! Pole sana.”
Kilole alijikuta akiangua kilio kilichomshtua mumewe.
“Vipi tena?” alimuuliza.
“Aah! Basi tu.”
“Basi tu nini! Au umezidiwa?”
“Walaa, hata sijiui nalia nini.”
”Niambie kama umezidiwa nikuwahishe hospitali, utalia bila kujua unalia nini?”
“Nimemeza dawa naomba kitu kimoja.”
“Kipi hicho mke wangu?”
“Uniache nipumzike nisiamshwe na mtu yeyote na mtoto alale kwa msichana wa kazi.”
“Hakuna tatizo mke wangu.” Deus hakutaka kumsumbua mkewe alifanya yote aliyoelekezwa, alitumia nafasi ile ya mkewe kutotaka usumbufu kuzungumza na rafiki yake juu ya mpango aliozungumza na Teddy na wauza unga wenzake.
Baada ya kuoga na kupata chakula cha usiku kilichopikwa na msichana wa kazi alikwenda chumba cha rafiki yake. Alimkuta amejipumzisha, alipomuona rafiki yake alimkaribisha kwa furaha.
“Ooh! Best karibu.”
“Naona umejipumzisha.” “Nifanye nini baada ya mihangaiko ya siku nzima.”
“Basi leo tulikuwa na kazi moja nzito ya kukamata gari lililokuwa na madawa kutokana na taarifa za watoa habari. Wenye gari waligoma kufungua mpaka walipokuja wakubwa zetu ambao waliliruhusu bila hata kuuliza. Lakini taarifa zilisema gari lile lina dawa za kulevya.”
“Basi hapo kuna rushwa imetembea kwa wakubwa.”
“Umeona eeh!”
“Ukweli ni huo unafikiri ndani ya gari kulikuwa na mzigo kiasi gani, ndiyo maana walikuwa wabishi kuwafungulia gari kwa vile kuna watu wanawategemea.” “Kitendo kile kimenivunja nguvu kweli, siwezi mkupote muda wangu kwa upuuzi kama ule.”
“Nawe kula sehemu yako.”
“Sasa kuna dili moja nimeingia leo si mchezo.”
“Mmh! Dili gani tena mzee?”
“Si nilikueleza yule mwanamke alisema atanikutanisha na wenzake?” “Eeh, ndiyo.”
”Basi leo mchana alinipigia simu na kunikutanisha nao.”
“Acha utani! Ehe ikawaje?”
“Tumekubaliana kuinza mwezi ujao kwa hiyo mpaka mwezi ukikatika nitakuwa nimetengeneza bilioni mbili.” “Acha utani!”
“Ukweli sasa hivi najiona nimekwisha uaga umasikini, kweli! Umefikia wapi mambo yako na Happy?”
Swali lilikuwa kama pigo zito moyoni mwa Kinape hakuwa na jibu la haraka, Deus hakujua rafiki yake anawaza nini baada ya kumuuliza na kukaa kimya. “Ni hivi nina fedha kidogo nitakupa ili kuhakikisha unakamilisha harusi yako.”
“Kiasi gani?”
“Milioni ishirini ambazo nitakupa sasa hivi ufanye maandalizi yako na shemeji, umekwisha mpeleka kwa wazazi kijijini?”
“Bado.”
“Unasubiri nini? Fanya hivi kesho kutwa hakikisha unakwenda na Happy kwa wazazi ili tupange nipango mingine. Utatumia gari langu sawa pia tafuta nyumba ya milioni hamsini ili nikununulie kwa siri ili shemeji yako asijue kitu.”
“Hakuna tatizo nimekuelewa mkuu.”
“Mbona kama upo mbali au umechoka?”
Deus alimuuliza Kinape aliyeonekana yupo mbali kimawazo. “Ni kweli leo nimefanya kazi kama mbwa, hapa nilipo natamani kulala tu si kitu kingine.”
“Basi pumzika tutaonana kesho.”
“Usiku mwema.”
“Na kwako pia.”
Deus alitoka na kwenda sebuleni kutafuta mkanda wa filamu ili kuvuta muda kabla ya kupanda kitandani huku akiwa anaisikia harufu ya utajiri. Alipiga mahesabu hata kama wataingiza mara moja kwa miezi miwili kwa mwaka aliziona bilioni kumi na mbili mbele yake.
Alijikuta akicheka peke yake huku akisema kwa sauti ya chini: “Kumbe utajiri hauna njia ndefu.”
Wakati akiwaza yale chumbani mkewe alikuwa akigaagaa kitandani kama nyoka aliyemwagiwa mafuta ya taa kutokana na kuwa na maswali yasiyo na majibu juu vitu vilivyopo mbele yake alijiuliza aanze na lipi la Jimmy au la Happy.
Alipanga usiku atoroke na kwenda kwa Jimmy kumbembeleza kwa njia yoyote ili tu amjue nani aliyemfanyia mchezo mchafu kama ule tena kujua picha za awali akifanya mapenzi na shemeji yake. Pamoja hakuwa na usingizi alitulia kitandani akisubiri mumewe akilala atumie nafasi hiyo kwenda kwa Jimmy.
Naye Kinape baada ya kutoka Deus alijikuta kwenye mtihani mzito wa kutoa uamuzi sahihi ambao hautaleta madhara kati ya Happy na Kilole. Lakini Happy kwake alikuwa muhimu kuliko Kilole ambaye tayari alikuwa mke wa mtu.
Swali ambalo kila kukicha lililokuwa likimla akili lilikuwa kuhusu picha alizopigwa akifanya mapenzi na Kilole nani aliyezipiga, alipata wazo la kumtafuta ili kupata ukweli wasiwasi wake huenda mtego ule ulipangwa na Deus.
Kingine kilichomkosesha raha kama picha zile zikivuja na kumfikia Deus angekuwa kwenye wakati gani. Wazo la kuua Deus au kumfanyia baya lolote alilipinga kwa nguvu zote japo hakuweza kumweleza ukweli Kilole. Taarifa za siku ya tatu kwenda kijijini kumtambulisha Happy zilizidi kumchanga kwa kujiuliza habari zile akimweleza Kilole atazipokea vipi.
Aliamua liwalo na lile lazima amweleze ukweli na hiyo kesho kutwa lazima ampeleke kijijini mengine yatakayotokea atakuwa tayari kukabiriana nayo. Alipuuza mkwara wa Kilole na kujilaza kuitafuta siku ya pili.
*****
Majira ya saa saba usiku baada ya kuona mumewe amelala na kukoroma, Kilole alijinyanyua kitandani na kumtazama mumewe aliyekuwa amepitiwa na usingizi hajitambui. Alinyanyuka taratibu kwa kunyata hadi pembeni ya kitanda na kuunyanyua mto aliokuwa amelalia mumewe taratibu na kutoa bastola ya mumewe.
Alikwenda hadi kwenye kabati na kuvaa kaptura na fulana, aliichomeka bastora kiunoni kisha alijifunga kanga zilizomziba mwili mzima na kutoka taratibu bila kumshtua mtu yeyote. Aliegesha mlango na kutoka kwa kunyata hadi nje ya geti na kuchepua mwendo kupitia barabara kubwa kuelekea kwa mpiga picha Jimmy ambako hapakuwa mbali sana na kwake.
Baada ya mwendo mfupi aliacha barabara ya rami na kuingia kwenye uchochoro ambao ungemfanya atokee nyuma ya nyumba anayoishi Jimmy pia ndipo palipokuwa na dirisha lake. Alishukuru Mungu muda wote hakupata kizuizi chochote alitembea kwa taadhari kubwa, shida yake kwenda kugonga dirisha la Jimmy ili azungumze naye na kutaka msaada wake. Alipokaribia alitembea kwa kunyata ili mtu wa ndani asijue nje ya nyumba kuna mtu anapita. Aliporikaribia dirisha la Jimmy alisikia sauti za watu wawili mwanaume na mwanamke.
Mwanaume alimtambua ni Jimmy lakini mwanamke hakujua ni nani, lakini alijua ni mwanamke wake japo Jimmy hakuwa ameoa. Alitulia akijifikiria amwite au afanyeje kwani wasiwasi wake huenda pakatokea tatizo kwa muda ule mwanamke wake akajua yeye ni hawala yake. Wakati akiwaza afanye nini, aliendelea kusikia mazungumzo yaliyokuwa yakizunguzwa ndani.
“Sasa mpenzi hiyo fedha utanipa lini?”
“Kuna dili moja litatiki muda si mrefu nitakupatia.”
“Kumbuka na mimi ninataka kuendesha gari.” “Nimekueleza nitakupatia hiyo fedha baada ya wiki kila kitu kitakuwa tayari.”
“Najua unanidanganya.”
“Mbona laki nane za kupangia nyumba nilikupa kisha laki nane zingine za kununulia sofa nimekupa nitashindwa vipi milioni nne?”
Kauli ile ilimshtua sana Kilole na kujiuliza Jimmy uwezo ya kutoa fedha kiasi kile ameutoa wapi, wakati maisha yake yalikuwa ya kubahatisha mpaka apige picha na muda mwingi alishinda kijiweni.
Wakati akijiuliza maswali yasiyo na majibu ndani mazungumzo yaliendelea.
“Ha..ha..lafu mpenzi siku hizi unafanya kazi gani maana fedha zimeibuka kama uyoga?”
Itaendelea

No comments

Powered by Blogger.