NYUMA YA MACHOZI - 20

MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
Kauli ile ilimshtua sana Kilole na kujiuliza Jimmy uwezo ya kutoa fedha kiasi kile ameutoa wapi, wakati maisha yake yalikuwa ya kubahatisha mpaka apige picha na muda mwingi alishinda kijiweni.
Wakati akijiuliza maswali yasiyo na majibu ndani mazungumzo yaliendelea.
“Ha..ha..lafu mpenzi siku hizi unafanya kazi gani maana fedha zimeibuka kama uyoga?”
SASA ENDELEA...
“Maisha kama kalata ukijua kuzichanga kila kitu kina kwenda kilivyopangwa.”
“Au unauza dawa za kulevywa?” “Kwani dia tatizo lako nini?”
“Naogopa nisije kukupoteza wakati nakuhitaji.” “Ungekuwa unanihitaji ungeridhika na nilivyokupa.”
“Sawa, hata kama unauza unga kuwa makini.”
Kilole alijikuta akijawa na maswali juu ya maneno ya Jimmy kuonesha ndani ya wiki ile atampatia yule mwanamke milioni tatu. Pia siku ile alimpa milioni moja na laki sita. Akili ya haraka aliamini fedha hizo huenda ndipo aliziombwa azitoe ili azipate picha zake.
Alikubaliana na wazo lake la awali kuwa Jimmy ndiye mhusika mkuu wa mipango yote. Wakati akiwaza vile alisikia simu ya Jimmy ikiita, alimsikia Jimmy akimwambia mwanamke wake.
“Samahani nakuja.” “Unakwenda wapi?”
“Sipendi maswali ya kijinga nimekueleza nakuja,” Jimmy alijibu kwa ukali.
“Najua na wanawake zako tu, “ alimsikia mwanamke akilia wivu.
“Wewe si unataka gari sasa kwa nini unapenda kufuatilia mambo yangu?”
“Sawa, basi nenda.”
Kilole alisikia mlango ukifunguliwa kuonesha Jimmy alikuwa akitoka nje kusikiliza simu. Kilole akiwa ametulia pembeni ya ukuta kwenye choo cha nyumba ya jirani.
Alisikia sauti za viatu zikielekea nyuma ya nyumba, kwa haraka alijificha nyuma ya choo. Jimmy bila kujua kuna mtu alisimama pembeni ya choo na kupiga simu iliyopokelewa upande wa pili.
“Sema Rich mbona usiku?”
“Aisee nina tatizo kubwa ya fedha,” kutokana na utulivu wa hali ya hewa Kilole alisikia mtu aliyekuwa akizungumza upande wa pili.
“Shida gani mzee, si leo nimekupatia mgao wa milioni?” “Ni kweli, si unajua nyumba za uswahili baada ya leo kununua sofa nimepandishiwa kodi ghafla na kutakiwa nilipe mwaka mzima na fedha yake anataka kesho. Sasa sijui utanisaidia vipi naomba basi unikope milioni ili kesho kama tukilipwa ile fedha nitakurudishia.”
“Sikiliza Rich leo nimempa shemeji yako milioni mbili kwa ajili ya sofa na kulipia nyumba, kwa sasa sina kitu ila jitahidi kumtisha yule mwanamke ili tupate hiyo fedha ikiwezekana hata kesho saa tano asubuhi.”
“Okay, nitajaribu kumsomesha.”
“Atakuelewa tu, jitahidi kesho tuzipate zote milioni kumi sawa?”
“Sawa nimekuelewa.”
“Basi usiku mwema, unajua umenitisha sana, wasiwasi wangu yule mwanamke kujua kama ni mimi ndiye namchezea mchezo huu.” “Walaa, nawe usiku mwema.”
Baada ya kukata simu Jimmy alirudi ndani na kumuacha Kilole akiwa amepata kitu ambacho mwanzo alikidhania lakini siku ile ukweli ulijulikana. Aliona hakuna haja ya kuendelea kuwa pale. Aliondoka na kurudi nyumbani huku moyo ukimuuma kwa kitendo alichotendewa na Jimmy.
Alifika kwake na kuingia ndani bila mtu yeyote kujua kama alitoka, alipanda kitandani na kujilaza. Kutokana na kutingwa na mawazo muda mwingi alifikiria jinsi ya kumuadabisha Jimmy. Moyoni aliapa kabla ya kuwapa hizo milioni kumi lazima wote wawe wamelamba udongo.
****
Teddy mwanamke hatari muuza unga baada ya kumaliza kuuza mzigo wake alimuaga Deus na kumweleza kila kitu kitakavyoendelea atamjulisha. Muda wote alikuwa na maswali juu ya mtu aliyemchoma katika kitengo cha madawa ya kilevya.
Alijiuliza nani aliyekuwa akijua kuondoka kwake zaidi ya mdogo wa marehemu mumewe ambaye alinyongwa China baada ya kukamatwa na madawa ya kulevya. Tokea kifo cha mumewe mdogo wa mumewe alikuwa akimfuatilia na kumtaka kimapenzi. Lakini hakuwa tayari kutembea na familia moja kwa vile alikuwa na uamuzi wa kumchagua nani awe mpenzi wake. Muda mwingi kulikuwepo na kutoelewana kwa shemeji yake kulazimisha mapenzi na yeye kumkatalia. Mwanzoni alifanya kazi na mumewe ya uuzaji wa madawa na ndiye aliyemfundisha kuifanya kazi ile. Baada ya kifo cha mumewe alimshirikisha mdogo wa mumewe ambaye baada ya kupata fedha alianza nyodo na kuendelea kumtaka kimapenzi huku akimuahidi kumfanyia kitu kibaya kama ataendelee kumtolea nje.
Teddy bado hakutishwa na vitisho vya shemeji yake ambaye bado aliendelea kufanya naye kazi ya kusambaza dawa za kulevya kila kona ya dunia. Hata siku ya kuondoka mara ya mwisho aliyekuwa akijua safari ile ni yeye na washirika ambao wote walikula kiapo cha kuficha siri ya kazi yao na kuwa tayari kumsaidia mwenzao kwa gharama yoyote anapopatwa na tatizo. Wazo lake lilimpekeka huenda ni shemeji yake ndiye aliyefanya mchezo ule ili kumkomoa baada ya kumkataa kimapenzi.
Aliapa kumfanyia kitu kibaya kama ni yeye na adhabu yake ilikuwa ni kifo kwa vile nia yake ilikuwa ni kumpoteza. Teddy alipofika Italia alikwenda moja kwa moja kwenye nyumba aliyokuwa akiishi pamoja na shemeji yake.
Mara zote alipokuwa akisafiri na kurudi alikuwa akiwasiliana naye hata kumpokea, lakini siku ile alirudi kimya kimya. Alipofika nyumbani kwake aliingia ndani bila hodi, shemeji yake aliyekuwa na rafiki zake wakinywa na kujiachia na wanawake na muziki mkubwa alipomuona alishtuka sana.
“Ha! Teddy wewe si ulikamatwa?” “Wapi?” “Si..si.nilisikia umeshikwa Tanzania?” “Nani aliyekuambia?”
“Au alinidanganya?” “Nani mbona sikuelewi nani amekwambia mimi nimeshikwa?”
“Au umetoa rushwa?” “Ili?” Teddy alimuuliza huku akimtazama usoni kutafuta ukweli. “Tu..tu..achane na hayo, na..na mbona umekuja bila taarifa.” “Tatizo nini? kwa nini umegeuza nyumba yangu club?”
“Kwani tatizo nini?” “Mose unanitafuta huwezi kuigeuza nyumba yangu kama kilabu cha pombe ya kienyeji zinazouzwa Afrika.”
“Oya washikaji tutimke mambo yamekwisha haribika.”
“Sasa sherehe tunaihamishia wapi?” Mwanamke mmoja aliyekuwa amelewa sana na kuvaa nusu uchi aliuliza.
“Oya Rose, hii tunakwenda kuimalizia club Royal clasic.”
“Sasa kuna faida gani ya kupoteza muda, na huyu nani?” “Shemeji yangu.”
“Si ulisema umenyongwa au kafufuka?”
“Sitaki maswali hebu tuondokeni.”
Mose aliondoka na washikaji wake waliokuwa wamelewa na kwenda kumalizia starehe zao club.
Teddy alianza kufanya usafi ili kuirudisha nyumba katika hali nzuri. Macho yake yaliona simu kwenye kochi, aliacha kufanya usafi kuichukua simu ile na kuanza kuipekea kwenye sehemu ya ujumbe.
Jicho lake lilikutana na ujumbe ulioonesha shemeji yake alimtumia mtu aje kwenye sherehe ya kupotezwa kwake. Ilisomeka: yule fala nimemmaliza njoo tusherehekee njoo na demu wako. Palepale alipata picha kuwa shemeji yake ndiye aliyemtengenezea mtego ule. Aliapa kummaliza na kutoroka Italia na kwenda kuishi nchi yoyote kutokana na uwezo ya kifedha.
*****
Siku ya pili Kilole aliwahi kuamka ili aweze kuzungumza na Kinape kuwa asiondoke ili wazungumze. Kama kawaida Kinape alijichelewesha kwenda kazini. Baada ya Deus kuondoka alimfuata chumbani kwake ili apate muafaka wa jambo walilozungumza jana yake. “Mhu! Umefikia wapi?” Kilole alimuuliza Kinape.
“Kuhusu nini?” “Kuhusu huyo mwanamke wako.”
“Kwa kweli bado sijapata jibu, tena jana Deus ndio kaniachanganya zaidi.”
“Kivipi?”
“Amesema kesho niende na Happy kijijini.”
“Eti nini?” Kilole alishtuka kusikia habari zile.
“Mumeo kasema kesho niende na gari kanipa ili kuhakikisha sina cha kujitetea.”
“Wewe ulimjibu nini?”
“We unafikiri ningemjibu nini?”
“Si ungemwambia umebadili umamuzi kuwa hutamuoa tena Happy.”
“Ningeanzia wapi wakati kila siku nimekuwa nikiomba msaada wake kufanikisha ndoa yangu.” “Mmh! Kumbuka akiishafika kijijini mimi sina changu.”
“Lakini kwa nini tulazimishe mambo wakati yamekwisha onesha vikwazo?” “Kinape hunielezi lolote nikakuelewa, nimejitoa kwako sitarudi nyuma.”
“Sasa nitafanyaje maana leo jioni happy na mama yake watakuja kujua hatima ya uchumba wetu.”
“Lakini kwa nini tusimfutilie mbali Deus, huoni anatuwekea kivingu?”
“ Ni haraka sana kufanya mambo hayo, kuna kitu kimoja kizuri tukifanya haraka tutakipoteza.”
“Kitu gani?”
“Mwezi ujao kuna bilioni kama mbili hivi zinaingia kwa hiyo tukizipata tutakuwa na uwezo wa kuishi nchi yoyote tuitakayo.”
“Lakini kumbuka kila siku unaongeza siku mwisho wake picha zitamfikia na kuharibu kila kitu.” “Kilole tutakuwa wajinga kuziacha hizo bilioni mbili za bure.” “Tutazitoa wapi?”
Kinape alimueleza yote aliyoelezwa na Deus juu ya mpango wa kuhongwa na wauza dawa za kulevya. “Nimekuelewa.”
Alimkubalia ili kumaliza mazungumzo lakini moyoni alipanga wiki ile lazima afanye kitu ambacho kitakuwa simulizi midomoni mwa watu. Baada ya Kinape kuondoka kwenda kazini, Kilole alijikuta akizidi kuchanganyikiwa na kujiuliza aanze na nani kati wa watu wote watatu, mumewe, Jimmy na Happy mchumba wa Kinape.
Aliamini mtu wa kuanza naye alifaa kuwa Happy kwa kumzima usiku wa siku ile ili kuzuia safari ya kwenda kijiji, kisha Jimmy na mwisho alipanga kummaliza mumewe. Mpango ule aliufanya kwa siri ili mtu yeyote asijue kwa kuamini kama angemshirikisha Kinape angemuharibia kila kitu.
Wazo alilopata la kummaliza mumewe aliona anahitaji msaada wa mtu, na mtu wa karibu alikuwa Jimmy. Aliamini msaada wake ulikuwa muhimu lakini mwisho wa yote na yeye angemmalizia mbali. Baada ya kukubaliana na mawazo yake aliamua kumpigia simu Jimmy ili mpaka jioni mpango wake wa kummaliza mumewe ukamilike ibakie kuutekeleza. Baada ya kupiga simu ya Jimmy iliita upande wa pili na kupokelewa. “Haloo.” “Haloo Jimmy.” “Ndiyo sister.” “Samahani Jimmy nina shida na wewe.”
“Shida gani?” Sauti ya upande wa pili ilionesha kushtuka.
“Nitakueleza tukionana, sema tuonane wapi.”
“Njoo nyumbani kwangu.”
“Sawa nakuja.” “Nitakuwa nyumbani baada ya nusu saa.”
“Hakuna tatizo nitafika kwa muda huo.” Dakika tano baada ya kumaliza mazungumzo na Jimmy, simu ya Kilole iliita alipoitazama ilikuwa namba ngeni. Aliipokea. “Haloo.”
“Eeh! Umefikia wapi?”
“Kuhusu nini?” Japo sauti iliijua alijifanya kuuliza. “Hiyo milioni kumi ipo tayari?”
“Kesho itakuwa tayari.”
“Sihitaji kesho nataka leo.” “Okay, hakuna tatizo jioni ya leo nitatimiza kila kitu.”
“Na ufanye hivyo, kinyume na kauli yako kila kitu hadharani.”
“Wala usihofu, itanibidi nichukue fedha ya ujenzi wa nyumba nitazirudisha kesho.”
“Nakutakia siku njema.”
“Na wewe pia.”
Kilole baada ya kukata simu alishusha pumzi ndefu na kujikuta akili yake ikifanya kazi kama kompyuta kwa kupata jibu. Ilionesha muda alioweka Jimmy ulikuwa ni kuwasiliana na jamaa yake ili kutaka kujua fedha yao.
Alicheka kwa uchungu na kuamini siku ile mpaka inakatika itabaki kumbukumbu akilini mwake. Alikwenda kujiandaa kisha alitoka hadi kwenye mashine ya kuchukulia fedha na kuchukua milioni ishirini ambazo aliamini zingemsaidia kuifanya kazi yake vizuri.
Baada ya kuziweka vizuri fedha zake aliingia kwenye gari na kwenda moja kwa moja kwa Jimmy. Alimkuta Jimmy yupo nyumbani, kwa vile chumba alikuwa akikijua alikwenda kugonga mlango.
“Karibu,” Jimmy alitoka akiwa kifua wazi.
“Ooh! Sister karibu.”
"Asante nimekaribia,” Kilole alijibu huku akiingia ndani.
Ndani ya chumba cha Jimmy hakukuta mabadiliko makubwa zaidi ya tivii ya flati na friji ndogo. Alikaa kwenye kochi wakati huo Jimmy alikuwa akielekea chumbani kuchukua fulana. Macho ya Kilole yaliona kitu kilichomshtua, kiuoni kwa Jimmy kulikuwa na mchoro ambao ulifanana na mchoro aliouona kwenye kiuno cha mtu wa kwenye picha ya watu waliombaka.
Moja kwa moja ushahidi wake ulikamilika alijua Jimmy ni mmoja ya watu waliombaka, alijilaumu kwa kuondoka bila siraha ambayo ingemsaidia kumaliza kazi kwani ushahidi wa kutosha kuwa Jimmy ndiye mbaya wake ulikuwa umetimia. Lakini bado aliamini Jimmy alikuwa kiungo muhimu wa kufanikisha mpango wake kabambe utakaomuwezesha kutimiza lengo lake.
Itaendelea
Post a Comment