Wiki tatu za Magufuli, Lowassa kuingia Ikulu
Wakati
zikiwa zimebaki siku 23 kuanzia leo kabla ya kupiga kura Oktoba 25,
wagombea urais wakiwamo Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
na Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
wanaonekana wakichuana vikali katika kampeni huku kambi ya kila mmoja
ikielekea kutumia mbinu za ziada kwa nia ya kujihakikishia kura nyingi
za kuwaingiza Ikulu.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe umebaini kuwa hadi sasa, Magufuli
na Lowassa wamekuwa wakibadili mbinu kila uchao kuelekea katika dakika
za lala salama za kampeni zilizoanza rasmi Agosti 22, huku maeneo makuu
yanayoangaliwa zaidi na kila kambi miongoni mwao ikiwa ni pamoja na
ufafanuzi wa ahadi wanazotoa, mbinu zao katika kusafiri kutyoka sehemu
moja hadi nyingine, maeneo ya kwenda kupiga kampeni na pia aina ya watu
wanaowatumia katika kampeni zao.
Wagombea hao wanaonekana kuchuana zaidi katika kampeni kutokana na
wingi wa watu wanaowaunga mkono karibu katika kila mikutano yao. Mbali
na Magufuli na Lowassa anayewakilisha pia ushirikiano wa vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR-Mageuzi na
Chama cha Wananchi (CUF), wengine wanaoendelea kupambana kwa nia ya
kuingia ikulu ili kuwa warithi wa Rais Jakaya Kikwete baada ya uchaguzi
ni Anna Mghwira (ACT-Wazalengo), Chifu Lutasola Yemba (ADC), Hashimu
Rungwe (Chaumma), Janken Kasambala (NRA), Maximilian Lyimo (TLP) na
Fahmy Dovutwa wa UPDP.
AHADI/ILANI
Katika mikutano yao ya mwanzoni mwa kampeni, Lowassa na Magufuli
waligusia vipaumbele vyao kadhaa pindi wakiingia madarakani, huku
wakihusianisha utekelezaji wake na ilani za vyama vyao.
Kati ya mengi aliyowaahidi Watanzania pindi akiingia Ikulu,
Magufuli alisema atahakikisha kuwa elimu inatolewa bure kuanzia madarasa
ya chini hadi kidato cha nne.
Alizungumzia pia malengo ya serikali yake katika kuhakikisha kuwa
huduma za afya zinazimarishwa, kwa kujenga zahanati katika kila kijiji,
kituo cha afya katika kila kata, hospitali katika kila wilaya na pia
hospitali ya rufaa katika kila mkoa. Pia aliutangazia umma juu ya
dhamira yake ya kuhakikisha kuwa kila kijiji nchini kinapata mgawo wa
Sh. milioni 50 zitakazotumika kusaidia harakati za maendeleo.
Wakati siku zikielekea ukingoni, Magufuli na timu yake wanaelekea
kupiga hatua moja mbele kwa kuhakikisha kuwa hatoi tu ahadi hizo, bali
pia anaeleza ni kwa namna gani yote anayoahidi yatafanyika. Kwa mfano,
ili kushughulikia tatizo la ajira, Magufuli amekuwa akisisitiza kuwa
serikali yake itahakikisha kuwa viwanda vinajengwa katika mikoa yote na
pia tozo zinazokwaza shughuli za kujikwamua kiuchumi kwa vijana na kina
mama zinasitishwa mara moja, baadhi zikiwa ni kwa waendesha bodaboda na
mamalishe.
Badala yake, Magufuli amekuwa akisisitiza kuwa serikali yake
itaongeza mapato maradufu kwa kuhakikisha kuwa mianya yote ya ufisadi
inazibwa, anaanzisha mahakama maalum ya kushughulikia mafisaidi na
kwamba, wafanyabiashara wakubwa wanalipa kodi kwa usahihi.
Lowassa na timu yake walianza kwa kutoa ahadi kuhusu utoaji wa
elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu, kutoa fursa kwa kila
mwananchi kuwamo katika mpango wa bima za afya, kutoa fursa za ajira
kwa vijana na pia kushughulikia kwa taratibu za kisheria kesi
zinazohusiana na ugaidi dhidi ya kina Sheikh Faridi.
Kama ilivyo kwa Magufuli, hivi sasa Lowassa na timu yake wamekuwa
wakienda mbali zaidi, wakieleza ni wapi fedha zitapatikana katika
kutekeleza ahadi ya elimu bure na pia juu ya kutoa fursa za ajira kwa
vijana.
Alipokuwa Mtwara, Lowassa alisema zipo fedha nyingi zinazopotea
kupitia ununuzi na uendeshaji wa magari ya kifahari kama ya Toyota Land
Cruiser maarufu ‘mashangingi’ na kwamba matumizi ya aina hiyo
yakidhibitiwa, elimu bure itawezekana.
Pia alizungumzia jinsi serikali yake itakavyofumua mikataba ya gesi
na mafuta ili inufaishe zaidi Watanzania. Kadhalika, kuanzisha benki
maalum za kuwakopesha madereva wa bodaboda. mama lishe na
wafanyabiashara ndogondogo (Wamachinga).
Kwa ufupi, wote wawili hivi sasa wamekuwa wakijikita zaidi katika kufafanua kwa kina ahadi wanazotoa karibu katika kila mkutano.
MATUMIZI YA CHOPA, MAGARI
Mwanzoni mwa kampeni, timu ya kampeni ya Magufuli ilitangaza kuwa
itatumia zaidi usafiri wa magari ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Hata hivyo, hivi sasa CCM wameanza pia kutumia helikopta (chopa)
kusafiri katika baadhi ya maeneo.
Timu ya Lowassa ilitangaza kuwa mgombea wao angetumia zaidi chopa
na hilo lilianza kushuhudiwa alipokuwa Sumbawanga. Hata hivyo, hivi sasa
Lowassa ameanza pia kutumia magari na mwishoni mwa wiki alitumia gari
kusafiri kutoka Tanga hadi jijini Dar es Salaam.
KIKOSI CHA KAMPENI
Kadri siku zinavyosonga mbele, timu za Lowassa na Magufuli zimekuwa
zikijiimarisha kwa kuongeza watu wa kuzungumza kwenye mikutano yao.
Mbali na kikosi chao cha watu 32, Magufuli ameongezewa nguvu katika
mikutano yake na hadi sasa, tayari ameonekan akiwa na mawaziri wakuu
wastaafu, Joseph Warioba na John Samuel Malecela.
MIKOA MUHIMU
Eneo jingine linaloonekana kuangaliwa kwa umakini katika mbinu za
CCM na Ukawa ni maeneo ya kukamilisha kampeni zao. Hadi sasa, ipo mikoa
kadhaa ambayo bado haijafikiwa kwa namna inayoonekana kuwa ni ya
kimkakati. Hadi sasa, baadhi ya mikoa yenye wapiga kura wengi bado
haijafikiwa kabisa na wagombea hao au imefikiwa na mmoja wao tu, baadhi
ikiwa ni Mwanza, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya na Zanzibar.
Vumbi linatarajiwa kutimka zaidi miongoni mwa wagombea hao katika mikoa ya kanda za kaskazini na Ziwa.
UKAWA, CCM WANENA
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya Uchaguzi ya CCM, January Makamba,
aliiambia Nipashe jana kuwa chama chake kimejipanga kumaliza kampeni kwa
nguvu zaidi katika wiki tatu zilizobaki, lengo likiwa ni kuwafikia
wananchi wengi zaidi.
Makamba alisema wataendelea kutumia usafiri wa gari kuwafikia
wapiga kura, lakini hawataacha kutumia chopa pale inapobidi na ndiyo
maana wapo makada wao wameshaanza kutumia usafiri huo (chopa) kuzunguka
mikoa yote nchini, akiwamo katibu mkuu wao, Abdulrahman Kinana.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rajabu Luhwavi, alisema usafiri wa
chopa ni muhimu katika kipindi hiki na wataendelea kuutumia ili kutimiza
malengo waliyojiwekea katika kampeni.
“Tutafanya kampeni za nguvu na kasi kwa kuzingatia mahitaji, na tutaongeza chopa ili kumfikia kila mwananchi,” alisema.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Chadema, Tumaini
Makene, alithibitisha kuwa chama chao kimejipanga upya katika wiki tatu
zilizobaki ili kuhakikisha kuwa Lowassa anaingia Ikulu baada ya uchaguzi
mkuu.
Aliitaja mbinu mojawapo kuwa ni kuigawa nchi katika kanda maalum
10 ambazo watakuwa wakizishambulia kimkakati ili kufanikisha ushindi.
Makene alifafanua kuwa licha ya kutumia chopa kama walivyodhamiria
kitambo ili kurahisisha usafiri na kupunguza gharama, pia wako tayari
kutumia usafiri wowote ule hivi sasa ukiwamo wa magari kama walivyofanya
wakati Lowassa akielekea Dar es Salaam kutoka Tanga na hata meli,
pikipiki na baiskeli ikibidi watatumia ili kuwafikia wapigakura wengi.
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John
Mnyika, alisema wamejiandaa pia kulinda kura zao dhidi ya hujuma zozote
zile na njia mojawapo ni kuwataka wananchi kutokwenda mbali zaidi ya
mita 200 kutoka vituo vya kupigia kura ili kuhakikisha kuwa hakuna wizi
unaofanyika dhidi ya kura zao.
“Tukimaliza kupiga kura hakuna kuondoka na kurudi nyumbani...
tutahakikisha tunakaa mita 200 kutoka vituoni jambo ambalo siyo kosa
kisheria kwani tukijidanganya kurudi nyumbani tutapigwa bao la mkono,”
alisema Mnyika.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), vituo 72,000
vitatumika nchini kote kwa ajili ya uchaguzi huo na mshindi wa nafasi ya
urais atatangazwa rasmi siku tatu baada ya kupigwa kwa kura.
*Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe na Richard Makore
CHANZO:
NIPASHE

Post a Comment