ad

ad

Singidani (A Story From My Heart) - 10



 

MACHO ya mshangao yalimtoka. Woga ukamjaa moyoni mwake. Alibaki akiingalia ile simu bila kuipokea. Mara simu ikakatika. Hapo sasa akapata nafasi ya kuangalia simu yake vizuri.
Alikuta meseji nne, zote zilitoka kwa Laura. Alipoifungua ya kwanza tu, simu ikaanza kuita tena. Chris akazidi kuogopa. Akili yake ilimtuma kwamba, huenda aliyekuwa akipiga alikuwa ni mume wa Laura au walikuwa pamoja na alilazimishwa kufanya hivyo ili aingie mtegoni.
Hakuwa tayari!
Simu ilipokatika, mara moja akaanza kusoma ile meseji. Maneno aliyoyasoma yalimchanganya sana. Hakuamini alichokiona. Meseji ile iliandikwa: “Kwa muda mfupi sana umeuteka moyo wangu, tafadhali Chris usinitese. Mbona hujanitafuta wakati tulikubaliana tukutane klabu?”
Inawezekana vipi mwanamke ambaye aliambiwa ni mke wa mtu ampigie simu usiku ule tena akimwambia kuwa anatakiwa kwenda kukutana naye klabu? Jambo hilo lilimchanganya sana kichwa chake.
Akaendelea kusoma nyingine mfululizo: “Baba vipi jamani? Mbona kimya? Acha kunitesa.”
“Chris nimekuwa tayari kukukabidhi moyo wangu wote kwako, mbona sasa huonyeshi kuwa upo tayari?”
“Sikia, tayari mimi nipo klabu hapa, kama huji niambie nirudi zangu hosteli nikapumzike. Nimekuja hapa kwa ajili yako Chris.”
Meseji ya mwisho ndiyo iliyomchanganya zaidi. Anamwambia anataka kwenda hosteli? Ni hosteli gani wakati alishaambiwa kuwa ni mke wa mtu?
Kwa hakika usingizi wote ulipotea. Pamoja na yote hayo, alijua alikuwa mtegoni na kama angejibu chochote angeweza kukamatwa mara moja. Kwa mtu mkubwa kama mkuu wa kituo cha polisi, maana yake ni kwamba, kama angeamua kumfanyia chochote kwa kosa la kutembea na mke wake, angeweza!
Wazo moja la haraka likamvamia kichwani mwake; alitakiwa kuvunja kabisa line yake. Hakutakiwa kupatikana tena kwa namba ile. Hilo ndilo wazo lililomwingia kwa kasi sana. Hakutaka kufikiria sana kuhusu hilo.
Akavunja ile line na kuitupilia mbali!
“Shiiit! Tuone sasa, watanipata wapi! Kwanza mimi sijafumaniwa. Najua wakiamua kunitafuta watanipata, lakini natakiwa kuwa mjanja sana kwenye eneo hilo. Hawawezi kunikamata asilani.”
Hasira ilimjaa moyoni. Alishindwa kuelewa ni kwa nini Laura aliamua kumdanganya kuwa hajaolewa wakati alikuwa mke wa mtu, tena wa askari kabisa. Jambo hilo lilimuumiza sana.
Akajilazimisha kulala.
***
Nani asiyemjua Dk. Chris, msanii wa filamu za Kibongo? Kila kona alijulikana. Hilo lilimaanisha kuwa, kama polisi mkoani Singida wangeamua kumtafuta kwa dhati kabisa, wangemkamata mapema sana asubuhi hiyo.
Chris alilijua hilo. Mara baada ya kuamka, alikwenda moja kwa moja mapokezi na kumuomba mhudumu akamnunulie kofia ya kapero. Yule mhudumu hakuwa na maswali mengi, alichukua fedha kwa Chris kisha akaenda kununua kofia na kumpelekea.
Chris akaichukua na kuivaa baada ya kujiandaa kikamilifu. Alitoka nje ya gesti hiyo na kutembea kwa mwendo wenye tahadhari zote. Taratibu akiwa ameuficha uso wake kwa kapero, alikodi teksi na kumtaka dereva ampeleke stendi kuu ya mabasi mkoani Singida, Misuna.
Dakika tano tu zilitosha kumfikisha kituoni hapo. Alishuka na kumlipa dereva kisha akatembea hadi katika ofisi za basi la Beffe, linalofanya safari zake kutoka mjini kwenda wilayani Mkalama kupitia Iguguno na Nduguti.
“Gari linaondoka saa ngapi?” Chris akamwuliza dada aliyekuwa akimkatia tiketi.
“Saa tano kamili, kwa sababu leo tunapita hadi Meatu.”
“Sawa, nipatie tiketi lakini kuna shughuli zangu nazifanya hapa mjini, sitapandia hapa. Mtanikuta kwenye mizani huo muda.”
“Tafadhali usije kulalamika umeachwa, saa tano juu ya alama uwe pale, sisi tutakukuta hapo.”
“Haina shida dada.”
Chris akalipa kisha akaondoka zake na kwenda kuchukua teksi nyingine iliyompeleka Kibaoni, ambapo ndipo gesti iliyokuwa na begi lake na vitu vyake vingine. Gari liliingia eneo hilo na kuegesha mbele ya geti.
“Naomba ukaniitie mhudumu tafadhali,” Chris akamwomba yule dereva ambaye alitii.
Sekunde chache sana, Mwanjaa alitokea, akakutana na swali kutoka kwa Chris: “Vipi, jamaa walirudi tena jana?”
Chris alisubiria jibu la Mwanjaa akiwa mwenye wasiwasi mwingi sana. Bado hakuijua hatma yake.
Itaendelea wiki ijayo.
Powered by Blogger.