NEC yatoa mwongozo utangazaji matokeo urais
Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imetoa mwongozo ikisema kuwa matokeo ya
udiwani, ubunge na urais yanayobandikwa kwenye vituo mbalimbali nchini
ni ruksa kutangazwa na vyombo vya habari, lakini havina mamlaka ya
kumtangaza mshindi wa nafasi yoyote.
Kamishna wa Nec, Prof. Amon Chaligha, alitoa mwongozo huo wakati
akijibu maswali ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari waliotaka
kujua kama vyombo vyao vitaruhusiwa kutangaza matokeo ya urais kadiri
yatakavyokuwa yakipokelewa kutoka kwenye vituo mbalimbali nchini.
Alisema awali, matokeo ya urais yalikuwa hayabandikwi wala mawakala
kusomewa, lakini sasa imeamuliwa yasomwe, yabandikwe na kila mmoja
kupewa nakala kwa lengo la kuongeza uwazi.
“Matokeo ya vituo yanaruhusiwa kujumlishwa na kutangazwa...
waandishi wa habari wanaweza kutangaza matokeo ya vituo, lakini siyo
kutangaza mshindi,” alisema Profesa Chaligha na kuongeza:
“Tunafanya hivi ili kuondoa hisia mbaya na kuziba mianya ya kuibwa
kwa kura au kubadilishwa matokeo. Tume haina matokeo yake kama
inavyosemwa, bali ni yale yatokanayo na kura zinazopigwa na wananchi,”
alisema.
“Tangazeni matokeo, lakini msiandike huyu ni mshindi kwa sababu hiyo si kazi yetu,” alisema.
Kwa mujibu wa kifungu cha 80 cha sheria ya Tume ya Taifa ya
Uchaguzi sura ya 343 na kifungu cha 81 cha sheria ya uchaguzi ya
serikali za mitaa, sura ya 292, Nec ndiyo yenye mamlaka kisheria
kujumlisha na kutangaza matokeo ya uchaguzi wa rais.
Wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo husika ndiyo wenye mamlaka
kisheria kujumlisha na kutangaza matokeo ya uchaguzi ya ubunge na
wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ndiyo wenye mamlaka ya kujumlisha na
kutangaza matokeo ya udiwani.
JAJI LUBUVA ATOA NENO
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva, alivitaka vyombo vya habari
kuzingatia maadili ya kazi yao kwa kuendelea kuandika ukweli bila
kuegemea upande wowote.
“Tunaomba mtumie kalamu zenu kuelimisha wapigakura wajitokeze kushiriki uchaguzi mkuu,” alisema.
Kamishna wa Nec, Jaji mstaafu John Mkwawa, pia alifafanua juu ya
wapigakura ambao walirekebisha taarifa zao, lakini hadi siku ya uchaguzi
majina yakakosekana katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, akisema
kuwa kitakachotumika kuwaruhusu kupiga kura ni hekima na burasa ya
msimamizi wa kituo baada ya kujiridhisha na kitambulisho
kitakachoonyeshwa na mpigakura.
Mkurugenzi wa Nec, Ramadhani Kailima, alisema hadi kufikia Oktoba
15, vifaa vyote vya uchaguzi vitakuwa vimeshawasili katika majimbo yote
nchini isipokuwa karatasi za kupigia kura ambazo alisema zitawasili
baadaye.
CHANZO:
NIPASHE

Post a Comment