Mama Lowassa afichua atakavyokuwa 'first lady'.
Mke
wa Edward Lowassa ambaye ni mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Regina Lowassa, amesema ana uhakika mumewe
atashinda katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu kutokana na muitikio
mkubwa anaoupata katika mikutano yake na pia kiu ya wazi ya wananchi
katika kufanya mabadiliko.
Kadhalika, ametaja vipaumbele vinne alivyojiwekea katika kumshauri
mumewe ili mwishowe aliongoze taifa kwa mafanikio makubwa katika kipindi
chake cha kuwa madarakani.
Mbali na Chadema, Lowassa anawakilisha pia muungano wa vyama vinne
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR-Mageuzi na
Chama cha Wananchi (CUF).
Mama Lowassa alielezea mambo hayo jijni Dar es Salaam jana katika
mkutano wake na wanawake walio katika Baraza la Wanawake wa Chadema(
Bawacha), Wilaya ya Kinondoni.
Akizungumza katika mkutano huo kuitikia shangwe zilizokuwa
zikimtaja Lowassa kama rais ajaye, Mama Lowassa alisema amejawa na imani
kuwa mumewe atashinda kwa sababu ameshuhudia mwenyewe muitikio wa
wananchi katika mikoa mbalimbali waliyopita katika harakati za kampeni
zinazoendelea nchini kote.
“Awali, nilikuwa ninafahamu kwamba Watanzania wengi wana matatizo.
Lakini baada ya kutembea zaidi katika kila pembe ya nchi, sasa nikiri
kugundua kwamba nilichokuwa nakifahamu juu ya matatizo ya Watanzania
kilikuwa kidogo sana kulinganisha na ukweli uliopo... sasa nimejionea,
ni matatizo makubwa na ndiyo maana wana kila sababu ya kuamua kufanya
mabadiliko,” alisema Mama Lowassa.
ATAKAVYOKUWA 'FIRST-LADY'
Akieleza zaidi, Mama Lowassa ambaye atakuwa 'first lady' kama
mumewe atashinda na kuwa rais baada ya Oktoba 25, mwaka huu, alisema
atajielekeza katika kushauri na kupigania vipaumbele vinne kwa ajili ya
wanawake nchini. Alivitaja vipaumbele vyake hivyo pindi atakapokuwa mke
wa rais kuwa ni katiba, elimu, afya na uchumi.
Akifafanua, Mama Lowassa alisema ataendeleza mapambano kuhakikisha
kuwa ukombozi wa mwanamke unapatikana kwa dhati kupitia Katiba ya nchi,
ambayo serikali itakayoundwa na Ukawa imeeleza wazi kuwa itaisimamia ili
iandikwe upya kwa maslahi ya Watanzania.
Alisema yeye kama Mke wa Rais mtarajiwa, atahakikisha elimu kwa
wanawake inapewa kipaumbele na kuingizwa kwenye katiba kwani huo ndiyo
ufunguo wa ukombozi wa kweli.
Akielezea kuhusu afya, alisema ni dhamira yake pia kuona eneo hilo
linaboreshwa kwani waathirika wakubwa wa huduma duni ya hospitali ni
pamoja na wanawake. Alizungumzia pia umuhimu wa kuwainua wanawake
kiuchumi ili hatimaye waondokane na umaskini.
Alisema hapendi kuona wanawake wanakuwa tegemezi na kwamba
atahakikisha mara zote anamshauri Rais ili kuhakikisha wanawake nao
wanajitegemea kiuchumi kwa kuhakikisha wanapata fursa za kujipatia
mikopo, elimu bora na afya bora tofauti na ilivyo sasa.
Aliwataka wanawake wajitokeze kwa wingi Oktoba 25 na kumpigia
Lowassa kura nyingi za ndiyo ili aingie madarakani na kuleta mabadiliko
kwa manufaa ya taifa.
Alisema mabadiliko na kuijenga Tanzania mpya yanawezekana, wala si
kwa kutumia gharama kubwa na nguvu kubwa isipokuwa kwa kuweka mikakati
mizuri, thabiti na kuitekeleza kwa vitendo.
“Ninaomba wanawake mniamini katika hili...kwa sasa siwezi kusema
mengi, ila ninanawahakikishia kuwa baada ya Lowassa kuchaguliwa,
nitarudi kwenu na tutapanga kwa pamoja mikakati zaidi ya kuishauri
serikali ya Ukawa katika kutimiza dhamira ya kuwakomboa wanawake na
Watanzania wote,” alisema.
Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha, Kunti Yusuph, alisema katika vipindi
vyote vya uchaguzi, wanawake wamekuwa wakirubuniwa na chama tawala kwa
vizawadi vidogo kama khanga na kisha kutelekezwa baada ya uchaguzi,
lakini sasa hawapaswi kukubali hali hiyo bali washiriki kwa dhati ya
kuleta mabadiliko ya kweli kupitia Ukawa.
CHANZO:
NIPASHE

Post a Comment