MABAO 500 YA CRISTIANO RONALDO, HATA WEWE YANAKUHUSU

Na Saleh Ally
MSHAMBULIAJI
nyota duniani, Cristiano Ronaldo, amefikisha mabao 500 aliyoyafunga
akiwa na timu tatu pamoja na timu yake ya taifa.
Ronaldo amefikisha mabao 500 katika kipindi ambacho ametimiza miaka 30, jambo ambalo si dogo au si la kuliacha lipite tu.
Hakika Ronaldo ambaye amekuwa mwanasoka bora duniani mara mbili, ana kipaji cha juu kabisa.
Mabao
hayo na mfano utaona amefikisha mabao 323 sawa na gwiji wa Real Madrid,
Raul Gonzalez si jambo dogo. Sasa ana nafasi ya kuwa gwiji kwa kufunga
mabao mengi zaidi.
Tayari
Ronaldo ana rekodi ya wastani wa juu zaidi katika ufungaji kwenye Ligi
Kuu Hispania ‘La Liga’. Ana wastani wa 1.05 ya mabao. Maana yake
amefunga bao katika kila mechi kama mabao yake yatagawanywa.

Mafanikio ya mabao 500 tangu alipofunga bao lake la kwanza akiichezea Sporting Lisbon ya Ureno Oktoba 7, 2002.
Ndani
ya miaka 13, Ronaldo ameweza kufunga mabao hayo 500 tena akicheza
katika timu kubwa tatu ambazo hakika zinakuwa na ushindani wa juu na
wachezaji wake hupambana na upinzani wa juu kabisa.
Ameshinda
kila kombe kwa ngazi ya klabu akiwa na Manchester United na Real Madrid
ambazo ni moja ya timu kubwa tatu zaidi duniani.

Wakati
anatua Real Madrid, msimu wa kwanza aliweza kuweka wastani wa mabao 20
kwa msimu. Baada ya hapo akapanda kwenda hadi mabao 53, kitu ambacho si
mzaha hata kidogo.
Msimu
wake wa kwanza na Madrid ambao ulikuwa ule wa 2009/10, alifunga mabao
21, uliofuata wa 2010/11 akatandika kimiani mabao 50.
Msimu
wa 2011/12, akafunga mabao 66, msimu wa 2012/13 akashuka kwa kufunga
mabao 51, ule wa 2013/14 akafunga mabao 56 na 2014/15 akafunga mabao 66.
Angalia
ushindani wa La Liga au michuano ya Ulaya, lakini huyu mtu ana uwezo wa
kufunga hadi mabao 50 kwa zaidi ya misimu miwili au mitatu anafanya
hivyo.

Katika
hali ya kawaida unaamini kweli ni kipaji pekee? Ndiyo maana nikaamua
kukumbusha kwamba mafanikio ya watu hawa hayapatikani ukiwa umelala na
kufumba macho.
Lazima
kujituma, lazima kujipambanua na kuamini mtafutaji hachoki. Historia ya
Ronaldo inajielezea, kwa kuwa wazazi wake walikuwa ni watu wa maisha ya
chini kabisa.
Baba
yake alikuwa ni mtunza bustani tu huko kwao katika Kisiwa cha Madeira,
Ureno. Ronaldo alionyesha anataka kufanikiwa na utaona wakati akiwa
Manchester United wachezaji wengi walimshangaa kwamba anaishi vipi,
kweli anaweza kula raha na maisha yake. Kwamba hakuwa akijipa nafasi ya
kula maisha?

Maana
alikuwa akifika mazoezini saa moja au mbili kabla ya wenzake, aliondoka
mazoezini saa moja baada ya wenzake. Muda wote aliokuwa pale aliendelea
kujifua zaidi.
Hata
walipokwenda gym, yeye ndiye alibaki muda mwingi zaidi ya wengine. Kuna
wakati hadi Kocha Sir Alex Ferguson aliwahi kumuonya kufanya hivyo,
kwamba apunguze mazoezi.
Wakati
anatokea Manchester United kwenda Madrid, wengi walichambua na kusema
angefunikwa kabisa na Lionel Messi na kupotea. Lakini leo amebaki pekee
anayechuana vikali na mshambuliaji huyo wa Barcelona mwenye kipaji cha
juu kabisa.

Ronaldo
si mashine, ni binadamu kama wewe lakini ameamua kuishi tofauti,
ameamua kutaka kufanikiwa. Amepania kutimiza ndoto zake bila ya
kusikiliza maneno mengi ya pembeni ambayo hukatisha tamaa.
Hii
inakuhusu wewe mchezaji wa soka wa Tanzania katika daraja lolote,
achana na woga na kusikiliza sana maneno ya watu hasa yale
yanayosisitiza ‘hauwezi’.
Unaweza
zaidi ya wanavyofikiri, unaweza kufika zaidi ya ulipo. Lakini usifumbe
macho ukalala. Hauwezi kuwa kama Ronaldo, lakini unaweza kupata
mafanikio ya juu yanayoweza kuwashangaza wengi kama Mreno huyo
anavyoshangaza kwa mabao yake hayo 500.
Kwa
Tanzania hata kufunga mabao 50 kwa misimu minne nayo ni shida kubwa.
Bado wewe unaweza kuwa wa kwanza kama utaachana na woga, kukubali
kukatishwa tamaa.
Ronaldo si mashine, ni binadamu lakini anafanikiwa. Lakini lazima ukubali kuumia zaidi na kujituma zaidi ili kufikia mafanikio.
Usiyaache
mafanikio yake ya mabao 500 yapite tu kama kitu cha kukushangaza,
badala yake yafanyie kazi siku nyingine yakusaidie hata katika maisha ya
kawaida. Panga ndoto, iote ukipambana na mwisho ufanikiwe.
BAO LA KWANZA AKIWA….
SPORTING LISBON
Oktoba 7, 2002 vs Real Betis.
MAN UNITED
Novemba Mosi, 2003 vs Portsmouth.
REAL MADRID
Agosti 29, 2009 vs Deportivo.
TIMU YA TAIFA URENO
Juni 12, 2004 vs Ugiriki.
MABAO:
NDANI YA BOKSI: 417
NJE YA BOKSI: 83
PENALTI: 81
ADHABU: 45
ALIFUNGAJE?
Mguu wa Kulia: 326
Mguu wa kushoto: 89
Kichwa: 83
TIMU ALIZOZIFUNGA LA LIGA:
Sevila-21, Getafe-18, Barcelona-15, Atletico Madrid-15, Malaga-14
WALIOMPA ‘ASISTI’ NYINGI:
Karim Benzema 31, Mesut Ozil 28, Angel di Maria 20, Gareth Bale 15, Ryan Giggs 16, Gonzalo Higuain 15.
SOURCE: CHAMPIONI
Post a Comment