JINI LA DARAJA LA SALENDA - 13

ILIPOISHIA: Baada ya kiumbe kile kilichojigeuza mtu kukaribia kwake, kilijigeuza umbile lililotoka nalo chini ya maji. Ajabu kilipotaka kuingia kwenye himaya yake aliona moto ukiwaka kuzunguka eneo lake, ghafla kiumbe kile kilitoka mbio hadi baharini na kuchota maji kisha kilirudi kuzima moto.
Kiliendelea kuzima moto mpaka kunapambazuka, kila kilichoendelea alikiona mpaka kupambana na jini lile. Hapo ndipo alipogundua jini lile lilitoka wapi, alicheka na kuona kinga aliyonayo ndiyo iliyomsaidia bila hivyo angekufa vibaya.
Taratibu moshi ulipungua na hali ya ndani ilirudi kawaida, mganga aliendelea kuweka tena ubani uliotoa moshi wa kawaida bila kuwepo na kitu kisicho cha kawaida. Alimtuma msaidizi wake kuwaita wagonjwa.
SASA ENDELEA...
CHINI YA BAHARI
Malkia Huleiya, mama mzazi wa Balkis alikwenda hadi chumba cha giza na kuomba Balkis atolewe, baada ya kutolewa alimpeleka kuoga na kukaa naye kwenye pwani ambayo huitumia kupumzika familia ya kifalme. Muda wote Balkis alikuwa akibubujikwa na machozi.
Baada ya kukaa kimya kwa muda malkia Huleiya alimwita mwanaye.
“Balkis”
“Abee mama.”
“Najua utatuona sisi wazazi wako makatili lakini unajua kabisa ubaya wa wanadamu na pia ni aibu jini kutoka katika ukoo wa kifalme kuzaa na mwanadamu.”
“Mama kabla ya kuzungumza lolote naomba mumtoe mpenzi wangu na kama hamtaki awe huku naomba mumrudishe duniani.”
“Hakuna tatizo.’ Alitumwa mtu kwenda kumtoa Brighton kwenye chumba cha giza na kumpa maji ya kuoga kisha kuwekwa kwenye chumba kizuri. Baada ya hatua zile mazungumzo yaliendelea.
“Nina imani imefurahi?” Mama yake alimuuliza.
“Siwezi kufurahi kwa vile sijatimiza dhamira yangu.”
“Ipi?”
“Ya kuolewa na mwanadamu.”
“Hilo ndilo baba yako hataki kusikia.”
“Lakini kumbuka tunachokifanya hakimpendezi Mwenyezi Mungu.”
“Kipi hicho.”
“Cha kuwafanya wanawake matasa.”
“Ni kweli, lakini tunafanya hivyo kwa ajili yako.”
“Kama unaona kufanya vile ni dhambi kwa nini msiniache na mpenzi wangu aliyekuwa tayari kukaa huku hata watoto wangezaliwa wangekuwa wetu.”
“Mwanangu hujui vita ya wanadamu ni kubwa, huwezi kuamini kizazi kimoja kimechukuliwa. Kama kizazi kimechukuliwa je, mwanadamu watakubali aishi huku?”
“Mwanadamu kanipenda mwenyewe wala sikumlazimisha.”
“Lakini si ana mchumba wake?”
“ Alimkana mbele yangu na kuwa tayari kunioa.”
“Kwa sababu hakujua kuwa wewe ni jini.”
“Hata alipojua alikubali ndiyo maana nimekuja kuishi nae huku.”
“Lakini kumbuka baba yako alikuwa akikutegemea sana, ulichokifanya kimemchanganya sana.”
“Lakini mama tatizo nini, kutafuta vizazi vya wanawake na kuzaa bila vita na wanadamu kipi bora, ona kama ulivyoniambia mkuu wa watwana Kulani kawa kipofu, kwa nini tusiachane na vita na wanadamu ili hamu ya mtoto apatikane bila kupata madhara zaidi.”
“Uamuzi wako umemuweka baba yako katika wakati mgumu, kumbuka anakupenda kuliko kitu chochote, hakuota hata siku moja utamkosea heshima.”
“Ni kweli najua baba ananipenda lakini alitakiwa kunisikiliza kuliko kuchukua maamuzi mazito, ona katumia nguvu nyingi matokeo yake Kulani kawa kipofu.”
“Balkis mwanangu hakuna jini anayekubali kushindwa na mwanadamu.”
“Ni kweli lakini kuna wanadamu nao huamini kabisa majini hawawawezi, kama wameweza kuchukua kizazi kimoja wanashindwa nini kuvichukua vyote?”
“Balkis mwanangu kama ungekwenda kwa kitu tulichokutuma, nina imani kazi yako ingekuwa nyepesi sana kuliko ulichokifanya cha kuanzisha uhusiano na mwanadamu.
“Kitendo kile kilituchanganya sana hasa baba yako, hata kuzungumza na wewe alishindwa na kunituma mimi. Anaamini hata matatizo ya Kulani chanzo ni wewe.”
“Chanzo ni mimi kwa vipi? Wakati niliwakataza tuachane na vita na wanadamu lakini mkawa wabishi.”
“Balkis mwanangu naomba uifanye kazi tuliyokutuma, tunaamini wewe ni mtoto mwenye heshima na usikivu. Nakuomba chonde chonde mwanangu msikilize baba yako.”
“Mamaa kwa nini msinikubalie, kwani kuna ubaya gani?”
“Kumbuka baba yako ni mfalme wa majini, ni aibu kwa mwanaye kuolewa na mwanadamu, ndiyo maana alikutuma kutafuta kizazi cha mwanamke ili kuhakikisha unapata tiba na kuolewa na jini mwenzako.”
“Kwa hiyo nimrudishe Brighton duniani?”
“Ikiwezekana.”
“Mbona unasema ikiwezekana.”
“Lazima tumuulize baba yako ataamua nini juu ya mwanadamu aliyejua siri yetu.”
“Sasa naona unataka kuharibu mazungumzo, mmenikataza kuolewa na mwanadamu basi nimrudishe kwao.”
“Lakini si atakuwa amejua siri yetu?”
“Sasa mnataka kumfanya nini?”
“Sijajua mpaka tupate maelekezo ya baba yako.”
“Sikiliza kama nimekubaliana na uamuzi wenu wa kuachana na mwanadamu ili niendelee na kazi yangu ya kutafuta vizazi vya wanawake, naomba kwenye suala la kurudi kwao mpenzi wangu msiniingilie.”
“Lakini kumbuka mwanangu chini ya bahari hii mwenye sauti ya mwisho ni baba yako.”
“Hata awe na sauti gani uamuzi wowote tofauti na kumrudisha duniani hatutaelewana.”
“Mbona umefika mbali, ngoja nimpelekee taarifa hizi, atafurahi sana kusikia kuwa umekubali kurudi dunia kutafuta vizazi vya wanawake. Pia nitamueleza suala la mpenzi wako la kurudishwa duniani. Siamini kama atakuwa na maamuzi mazito ya kukuumiza.”
“Mmh! Haya basi naomba nafasi ya kuzungumza na Brighton.”
“Mmh! Basi ataletwa huku ili baba yako asijue chochote.”
Baada ya kusema vile, Huleiya aliondoka na kumuacha Balkis akiwa amejilaza kwenye kiti cha uvivu. Japo moyo ulimuuma kumuacha Brighton mwanaume aliyeamini ndiye mume wa maisha yake. Bado hakuamini kama anaweza kutoa siri za majini. Lakini aliamini hakuwa akijua lolote katika siri za chini ya bahari kutokana na kufikia kwenye chumba cha giza.
Baada ya muda Brighton alifikishwa bustanini na kukutana na Balkis, baada ya kukutana Balkis alimueleza hali halisi na yeye kuwa tayari kumrudisha duniani. Kwa upande wake Brighton alijikuta akizama kwenye dimbwi la mahaba ya Balkis na kumuomba atafute njia yoyote ili asirudishwe duniani.
“Mpenzi kwa nini usimbembeleze baba yako ili tuishi pamoja?”
“Hilo ndilo lilikuwa lengo langu lakini limeleta mtafaruku mkubwa ndani ya familia. Kwa hiyo nakuomba ukubali kurudi duniani ila sitakuwa mbali nawe.”
“Mmh! Sawa lakini nitalikosa penzi lako.”
“Ni kweli, lakini lazima nikubaliane na matakwa ya wazazi wangu.”
“Sawa, sina jinsi,” Brighton alikubali kwa shingo upande.
Malkia Huleiya baada ya kuzungumza na mwanaye alipeleka taarifa ya kikao kwa mumewe mfalme Barami. Alipofika alimkuta akimsubiri kwa hamu.
“Karibu malkia wangu.”
“Asante mfalme wangu.”
“Mh, nijuze yaliyojiri huko?”
“Mmh! Namshukuru Mungu yamekwenda vizuri.”
“Kakubali?”
“Ndiyo.”
“Ooh! Afadhali.”
“Lakini..”
“Lakini nini tena malkia wangu?” Mfalme alishtuka.
“Kuhusu yule mpenzi wake.”
“Ana nini?”
“Anataka arudishwe duniani.”
“Ina maana hajui sheria yetu mwanadamu anayejua siri zetu huwa harudi tena duniani?”
“Hapo ndipo penye tatizo.”
“Tatizo gani?”
“Mwanao anataka amrudishe duniani.”
“Haiwezekani.”
“Amesema iwe isiwe lazima tumrudishe duniani.”
“Yeye ni nani anayetaka kutulazimisha tufanye anavyotaka, siwezi kuwa na sauti mbili katika himaya yangu ya chini ya bahari.”
“Lakini mume wangu..”
“Hakuna cha lakini, aendelee na kazi ya kutafuta vizazi tena tutampangia kwa siku moja alete vingapi ili awahishe kutimiza lengo la kuolewa tuondokane na adha hizi.”
“Mume wangu si vyema kila wakati kutumia nguvu, ifike wakati mwingine uwe unawasikiliza walio chini yako.”
“Siwezi, nasema kauli yangu ni ya mwisho na maamuzi yangu yaheshimiwe,” mfalme alikuwa mkali.
“Mume wangu hii itakuwa vita nyingine, kwa jinsi nilivyomsikiliza mwanao hawezi kukubali hili.”
“Nitakachomsikiliza ni kumuacha hai, lakini si kumrudisha duniani.”
“Mwanao amesema kwa hili hamtaelewana.”
“Hebu kamlete hapa,” mfalme alisema kwa hasira.
Alitumwa kijakazi kumfuata bustanini, Balkis alifika mbele ya baba yake kusikiliza kile alichoitiwa.
“Abee mtukufu mfalme,” Balkis aliitikia akiwa amesimama mbele ya baba yake.
“Kwanza nimefurahi kusikia umeweza kubadili uamuzi wako ila umeniudhi kwa kunilazimisha nifanye utakavyo.”
“Baba kukulazimisha kitu gani?”
“Kuhusu kumrudisha mwanadamu duniani.”
“Sasa tatizo liko wapi? Mmemkataa asinioe sasa si nimrudishe nilipomtoa.”
“Ina maana hujui sheria za majini, kama mwanadamu atajua siri zetu?”
“Nazijua lakini huyu nimemleta miye hakujileta mwenyewe, wala hakuletwa kwa lipizo.”
“Sheria za huku mwanadamu yeyote atakayeingia huwa hatoki salama, lakini kwa heshima yako hatutamuua bali ataishi huku milele.”
“Kwa hilo baba sitakubali hata kwa kukatwa kichwa, ni mimi ndiye niliyemlazimisha kuja huku iweje mumshikilie?”
“Hiyo ndiyo sheria ya huku kamwe haibadiliki.”
“Nasema kwa hili itabadilika.”
“Tunabisha?”
“Hatubishani ukweli ndiyo huo, ikifanywa kinyume nikiondoka hapa sitarudi tena.”
“Sooba,” alimwita mtwana msaidizi wa Kulani kwa sauti ya juu.
“Rabeka mtukufu mfalme,” Sooba aliitika na kusimama imara mbele ya mfalme.
“Mpeleke huyu kwenye chumba cha giza.”
Balkis alichukuliwa tena na kurudishwa kwenye chumba cha giza
Baada ya mwezi mmoja na nusu kupita, Suzana akiwa ofisini kwake, muda mfupi baada ya kuingia alijikuta akiwa na mawazo mengi. Hiyo ilikuwa ni kutokana na maneno ya Mganga Njiwa Manga alipokwenda kwake jana yake kufuatilia suala la kurudi mchumba wake Brighton, aliyekuwa chini ya bahari katika chumba cha giza.
Majibu ya mganga yalimkatisha tamaa tofauti na alivyofikiria kupatiwa matibabu kama ya Sharifa ya kuingizwa ndani ya maji ya bahari usiku wa manane. Alishangaa kuambiwa baada ya kukutana naye na kuchukua vitabu vyake vya uganga na kuvisoma kwa muda. Alipomgeukia alimueleza:
“Kazi yako inanichanganya sana, mpenzi wako bado yupo chumba cha giza, inaonesha alitolewa na kurudishwa tena, kuna utata mkubwa juu ya hatima ya mumeo kutolewa chini ya bahari kurudishwa duniani.”
“Mungu wangu! Si atauawa?” Suzana aliuliza.
“Hawezi kuuawa, inaonesha uhai wake bado mrefu.”
“Sasa itakuwaje ikiwa kila siku mambo yanazidi kuwa mabaya kwake, huoni kama maisha yake yapo hatarini?”
“Ni kweli yapo hatarini lakini..”
“Lakini nini mganga? Naomba msaada wako wa kumtoa huko.”
“Nilikueleza toka siku ya kwanza kuwa ni vigumu kumtoa kwenye chumba cha giza kwani kila nikimtafuta haonekani. Kuna siku mchana nikiwa katika shughuli zangu nilikiona kivuli cha mchumba’ako, ilionesha ametolewa chumba cha giza lakini usiku nilipotaka kuifanya kazi ile sikumuona.
“Kitendo kile kilinichanganya sana, hasa baada ya kuwa nimefika baharini na mbuzi wangu wawili, mweupe na mwekundu. Nilijikuta nikimtafuta tena lakini sikuweza kumuona. Niliamua kurudi nyumbani ili kuangalia upya, wasiwasi wangu nilidhani labda amekwisharudi duniani.
“Nilimtafuta kila kona ya dunia mpaka chini ya udongo sikumuona, kila nilipomtafuta ilionesha bado yu hai, lakini alikuwa haonekani zaidi ya kiza kinene. Baada ya kuhangaika sana niliweza kukiona kivuli chake kwa taabu sana kikionesha yupo kwenye chumba cha giza.
“Lakini kila nilivyojaribu kumvuta hakuonekana, huwezi kuamini kazi yako nimeifanya kwa muda mrefu bila mafanikio kuliko kazi nyingi nilizowahi kufanya. Wakati nikiendelea kuhangaika kutafuta nilishangaa kuona taarifa ikinionesha kuwa mumeo atatoka chini ya bahari bila kutumia dawa yoyote.”
“Sasa atatokaje ikiwa bado ameshikiliwa na majini?”
“Mara zote huongozwa na maandiko ya vitabu vya uganga ili niweze kumtibu mgonjwa, siwezi kukurupuka ndiyo maana dawa zangu huwa sibahatishi.”
“Hakuna njia nyingine ya kunisaidia?”
“Siwezi kukudanganya ila nakuhakikishia mpenzi wako atarudi bila dawa yoyote.”
Suzana alikubali kwa shingo upande kwa kuamini sifa za mganga yule kuwa hashindwi na kitu ni za uongo. Aliona ni ajabu Brighton kurudi bila dawa yoyote. Baada ya kuondoka na kurudi nyumbani aliondoa tumaini la kurudi kwa mpenzi wake.
Akiwa bado ofisini, katikati ya mawazo ya kukumbuka maelezo ya mganga yaliyomkatisha tamaa, baada ya kuonekana ameshindwa kumrudisha mpenzi wake na kuweka visingizio lukuki. Alishtushwa na sauti ya Sharifa aliyeingia ofisini kwake bila kumuona kutokana na kuzama kwenye dimbwi la mawazo.
“Suzana vipi shoga mbona unaonekana upo mbali, una tatizo gani?”
“Ooh! Shoga karibu.”
“Mbona hivyo, una tatizo gani maana nimeingia bila wewe kuniona?”
“Sharifa ina maana huyajui matatizo yangu?”
“Nayajua lakini leo umekuwa tofauti na siku zote.”
“Ni kweli.”
“Tatizo nini?”
Suzana alimtonya Sharifa aliyoelezwa jana yake na Mganga Njiwa Manga alipofuatilia kumrudisha duniani mpenzi wake. Kutokana na majibu yake juu ya mganga, ilionesha kabisa hakukuwa na uwezekano wa kurudishwa kwa mchumba wake.
“Nina imani mzee yule si mganga, wala hana lolote! Anafanya kazi kwa kubahatisha, iweje aweze kumuona ashindwe kumrudisha? Kisa, oooh, nilimuona mchana usiku akapotea, mwongo mkubwa hana lolote yule,” Suzana alilalamika.
“Lakini si alikueleza atarudi, tena kizuri hakukudanganya, au ulitaka akudanganye ili achukue fedha zako?”
“Kuna mtu gani anaweza kutoka kwa majini bila dawa au maombi?”
“Muamini yule babu, analokueleza ndilo linalokuwa.”
“Kipi cha kunifanya nimuamini zaidi ya sifa za kusikia?”
“Basi shoga mguu huu ni wako.”
“Una maana gani?”
“Mambo yamejibu.”
“Mambo gani?”
“Kazi ya mzee Njiwa Manga.”
“Kazi gani?”
“Kweli Suzana umechanganyikiwa.”
“Unafikiri kidogo, mtu siku zinakatika hakuna dalili zozote za kurudi kwa mpenzi wangu.”
“Suzana kwa mganga Njiwa Manga si nilikwenda kwa ajili ya kurudishiwa kizazi?”
“Ndiyo.”
“Basi majibu yametoka.”
“Ina maana wewe ni mjamzito?”
Itaendelea wiki ijayo Jumatatu.
Post a Comment