ad

ad

JINI LA DARAJA LA SALENDA - 11


Ilipoishia:
“Bila ya hivyo hawezi kutoka?” Sharifa aliuliza.
“Inategemea na uamuzi wa mfalme wa bahari kumtoa.”
Sasa endelea:

“Hawezi kumuua?” Suzana aliuliza kwa sauti ya kukata tamaa.
“Hawezi, nina imani atatoka tu, kinachotakiwa ni kuvuta subira.”
“Mmh! Na mimi tatizo langu?” Sharifa aliuliza.

“Wewe tatizo lako limepata bahati moja kubwa ambayo sawa na bahati ya mtende.”
“Bahati gani?” Sharifa aliuliza huku akijiweka sawa.
“Kitendo cha kufungiwa Balkis katika chumba cha giza, kimewawezesha kuja huku bila ya matatizo.
“Una maana gani?” Sharifa aliuliza.

“ Majini ni viumbe wasiokubali kuona wanavurugiwa mipango yao, Balkis kama angekuwa hajafungiwa lazima angeizuia safari yenu.”
“Angeizuia kivipi?”
“Mngekutana na vitu vya ajabu njiani hata kupinduka na gari lenu.”
“Si tungekufa?”

“Msingekufa, mngeumia tu ili msiweze kumfuatilia.”
“Na bahati nyingine?”
“Bahati nyingine wakati wa kufanya dawa ya kurudisha kizazi chako hakutakuwa na upinzani wowote. Wala kazi yako haitahitaji vitu vingi vya kufanya na itaanza leo saa sita za usiku baharini.”
“Kama angekuwepo?”

“Mmh! Pangechimbika, waganga wengi wamepoteza maisha kwa ajili ya kutaka kuvuruga mipango ya majini. Pia tungehitaji vitu vya gharama ili kumdhibiti hapo kazi ingetakiwa kufanyika saa nane za usiku baharini katika maji ya shingo.”
“Mmh! Sasa akitoka si ataweza kutuua?”

“Balkis ni jini lenye huruma sana, katika maisha yake hapendi kufanya vitu vibaya, hata kuolewa ilikuwa ni shinikizo la wazazi wake tu ambao walimlazimisha kutafuta vizazi vya wanawake ili aweze kupata tiba ya matatizo yake ya kushindwa kupata ujauzito.

“Mwanzoni alikataa katakata lakini aliahidiwa kupewa zawadi kubwa kama atapata mtoto hasa wa kiume. Alikubali kuifanya kazi ile kwa shingo upande, lakini moyoni mwake hakupenda hata siku moja kutenda kitendo chochote kibaya kwa wanadamu, siku zote aliwaza kuishi duniani na kuolewa na binadamu.

“Hata kazi  ya kutoa vizazi ilimchukua muda mrefu sana, kitu kilichowafanya wazazi wake kumleta duniani moja kwa moja ili aweze kupata vizazi hivyo kwa muda mfupi, bila kujua Balkis hakupenda kuifanya kazi ile.

“Siku Suzana alipoona sherehe ya ajabu juu ya bahari, hiyo ndiyo ilikuwa siku rasmi ya kuja duniani kwa Balkis kusaka vizazi vya wanawake na kuvipeleka baharini. Aliandaliwa jini mwingine ambaye kazi yake ilikuwa ni kuvipokea vizazi hivyo juu ya bahari katika eneo lile la Daraja la Salenda na kuvipeleka kwenye stoo chini ya bahari.

“Lakini ilikuwa tofauti na walivyotegemea wazazi wake, tangu Balkis alipofika rasmi duniani kwa kazi hiyo, kwa siku moja alipeleka vizazi vinne tu na chako kikiwa kimojawapo.
Kazi aliyotumwa alisahau baada ya kuvutiwa na uzuri wa mchumba wa Suzana na kujikuta akianzisha uhusiano wa siri bila mwenzako kujua.

“Katika harakati za kuhakikisha anamdhibiti mchumba wako, muda mwingi aliutumia kuhakikisha anamchukua jumla badala ya kuifanya kazi aliyotumwa.
“Aliweza kuwagonganisha kwa kuziua nguvu za kiume za mchumba wako na usiku ulipoingia alizirudisha ili afaidi yeye.

“Hali ile ndiyo iliyowasukuma kutafuta suruhu ya tatizo lenu, alipoona mmeanza kupata mwanga aliwachanganyeni kwa kuzirudisha kitu kilichokufanya uone kama hakuna tatizo.Balkis alipofanikiwa kumnasa mchumba wako kwenye mtego wake, hakupanga kuondoka naye mapema.
“Mngeendelea kushea mapenzi bila wewe kujua mpaka angeshika ujauzito.
“Kosa alilolifanya mchumba wako ni kwenda kinyume na yale aliyokuwa akielekezwa na Balkis.

“Kubabaika kwake kulipelekea wewe kuingia wasiwasi na kutamka neno lililomchukiza Balkis na kukupulizia hewa iliyokupoteza fahamu.
Hali ile ilimfanya Balkis aone mpango wake umeharibika mapema, ili asiweze kumpoteza mpenzi wako aliamua kuondoka naye kwenda chini ya bahari.

“Kutokana na huruma yake aliamini kama ataolewa na binadamu atakuwa ameokoa tatizo la wanawake kutolewa vizazi.  Lakini ilikuwa tofauti na walivyotegemea wazazi wake ambao wao  walimtuma kuishi duniani ili kufanikisha kupatikana kwa vizazi vingi vya mwanamke vitakavyomuwezesha kupata dawa ya kushika ujauzito ili aolewe na jini mwenzake.

“Walishangaa kumuona akiwa na mwanaume wa kibinadamu na kumtambulisha kwao kama ni mume wake. Kitendo kile kiliwaudhi sana, naye hakutaka kukubali.Baada ya mvutano Balkis na mchumba wako waliwekwa kwenye chumba cha giza.”
“Sasa kama unasema wazazi wake hawakukubali wataweza kumtoa salama Brighton?” Suzana aliuliza.

“Hapa inaonesha maisha yake yapo zaidi ya hapo, Kwa hiyo hawezi kuuawa.”
“Kama umeona anaweza kuendelea kuishi, itakuwa wapi duniani au kuendelea kufungwa kwenye chumba cha kiza?” Suzana alikuwa na shauku kutaka kujua hatma ya mchumba wake.
“Kwa kweli haioneshi ataishi wapi ila kuna maisha marefu ya mchumba wako.”
“Vipi kuhusu kazi yangu ya kurudisha kizazi kuna vitu vinatakiwa kwenda kununua?” Sharifa aliuliza. 

“Anatakiwa njiwa mwekundu tu, kwenye mabanda yangu anapatikana.”
“Na mimi kumpata mchumba wangu utanisaidiaje?”
Mganga aliingia kwenye gari, Suzana aliliendesha mpaka nyumbani kwa mganga, walipofika walimteremsha Sharifa ambaye alitembea kwa tabu. Walipomfikisha sebuleni walimlaza kwenye mkeka na kumsuburi mganga aliyekuwa amemshika njiwa aliyekuwa tayari ameshamchinja  tangu baharini.

Mganga alimwomba mkewe awape nguo za kujifunga wateja wale kutokana na nguo zao kulowana na maji ya bahari walipokuwa wakimtoa Sharifa kwenye maji. Baada ya kubadili nguo alimpa mkewe yule njiwa na kumweleza amnyonyoe na kumchemsha. Mkewe alimchukua na kuondoka naye na kuwaacha kina Suzana sebuleni.

Majira ya saa kumi za usiku mganga alimwamsha Sharifa  na kumpa dawa ya njiwa aliyechemshwa kwa ajili ya kumla akiwa katika sufuria ile ile aliyochemshiwa.
“Mle njiwa wote na unywe na supu yake,” mganga alimwambia Sharifa ambaye bado mwili wake ulikuwa hauna nguvu.

Sharifa alianza kumla njiwa  na kunywa supu yake kwa shida kwa vile alichemshwa bila kuwekwa chumvi, alipomuona kama anamshindwa kutokana na kutokuwa na kiungo hicho aliuliza.

“Mbona hana chumvi?”
“Huyo hawekwi chumvi, jitahidi umle vivyo hivyo, tena una bahati njiwa ni mdogo, watu wanakula kuku mzima bila chumvi.”

Sharifa hakuongeza neno alimuinamia njiwa wake na kuendelea kumla taratibu mpaka alipommaliza, wakati huo Suzana na mama yake walikuwa wakikoroma. Baada ya kumaliza kumla njiwa aliruhusiwa kuendelea kulala na wenzake ambao walikuwa hawajitambui kwa usingizi.

Wote waliamshwa alfajiri kwa ajili ya tiba ya mwisho ya kuoga maji ya bomba yaliyochanganywa na yale ya baharini. Baada ya kuoga waliingia kwenye chumba cha mganga kwa ajili ya mazungumzo ya mwisho kabla ya kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Wote walikaa kwenye mkeka baada ya mganga kutulia kwa muda huku akipitia maelezo kwenye karatasi nyeupe iliyoandikwa kwa wino mwekundu kisha alisema kwa sauti ya chini:
“Nina imani kazi yetu imekwenda vizuri sana tofauti na nilivyofikiria, shughuli kama hii niliifanya siku za nyuma kwa muda wa wiki nzima, tena nikiwa na majeraha mengi kutokana na kushindana na jini.”

“Unataka kuniambia nimepona?” Sharifa aliuliza.
“Umepona.”
“Kwa hiyo nina uwezo wa kushika mimba?”
“Bila shaka.”

“Nashukuru sana mzee wangu,” Sharifa alinyanyuka kwa lengo la kumpigia magoti.
“Hapana mama kaa tu, wakushukuriwa ni Mungu yeye ndiye mwenye kukubali au kukataa maombi yetu.”

“Ina maana kama Balkis angekuwa hakufungwa kazi isingeisha leo?” Suzana aliuliza.
“Kazi ya kushindana na majini ni ngumu msione imekwenda kirahisi kiasi kile, kama Balkis angekuwa hajafungwa vita ingekuwa kubwa asingekubali tuchukue kizazi katika stoo yake. Lazima ingetakiwa niwe na vijana wangu wa kazi na katika  kumdhibiti wangetakiwa mbuzi wekundu wawili, shuka nyekundu mbili na vitu vingine vingi.”

“Kutokana na kauli za mganga wa awali kuwa matatizo mengi ya tumbo yanatokana na jini Balkis kuchukua vizazi vya wanawake, lakini mbona ni wanawake wengi wana matatizo tofauti na idadi ya vizazi vilivyoko kwenye stoo ya Balkis?” Sharifa aliuliza.

“Kama nilivyowaeleza majini wanaishi kama wanadam, jinsi matatizo yetu yanavyofanana basi na ya majini huwa ni vivyo hivyo. Majini wengi wenye matatizo ya kukosa uzazi hutumwa duniani kuifanya kazi kama ya Balkis, hivyo vita si vyake peke yake ni kwa majini wengi.”

“Mungu wangu sasa tutapona vipi?” Suzana aliuliza.
“Kupona inategemea na wewe kuonana na watu wenye uwezo kama sisi au kusimama katika imani yako.”
“Kusimama kwenye imani una maana gani?” Sharifa aliuliza.

“Kila anayesimama katika imani humtanguliza Mwenyezi Mungu mbele kwa kila jambo, kabla ya kulala huomba ulinzi wake na baada ya kuamka humshukuru kwa kumvusha usiku salama, kisha humuomba tena amlinde na mchana wote.”
“Mbona tunafanya hivyo?” Alisema Suzana.

“Unaweza kuwa unafanya kutimiza wajibu wa maombi lakini imani yako si kamili, siku zote imani husimama kwa matendo siyo kwa maneno.”
“Unataka kuniambia aliyesimama kwa imani ya matendo mema hawezi kupatwa na tatizo hili?’

“Litaingilia vipi wakati Mungu ndiye mlinzi wake, hata hao majini wanamuogopa na kumuabudu yeye.”
“Kutokana na maelezo yako sasa hivi nimepona kabisa?” Sharifa aliuliza.
“Umepona na wala haitakutokea tena.”
“Kwa mfano Balkis akitoka gerezani,  akijua nimerudishiwa kizazi changu si litakuwa tatizo?”

“Tatizo litabakia kwake, wewe utakuwa salama kuanzia asubuhi hii.”
“Ile hali ya tumbo kuvurugika nilipokuwa pale baharini ilitokana na nini?”
“Kizazi chako kilikuwa kikirudi sehemu yake.”

“Baba tunashukuru kwa msaada wako,” mama Sharifa alisema kwa niaba ya mwanaye.
Nini kiliendelea?
“Jamani nimewaeleza wa kumshukuru ni Mungu bila yeye kukubali kisingetendeka kitu.”
“Hata hivyo baba pamoja na Mungu kukubali lakini wangapi wameshindwa wewe umeweza?”
“Ni kweli lakini inabakia pale pale kwa uweza wake.”
“Pamoja na uweza wake, lazima na wewe tukushukuru.”

“Haya mama asante, nina imani kazi yetu imekwisha ila kuna kombe la kunywa na kuoga kwa siku tatu.”
 Baada ya Sharifa kupewa kombe, waliruhusiwa kuondoka lakini kabla Suzana naye alitaka kujua hatima ya mpenzi wake katika chumba cha giza.

“Sasa na mimi itakuwaje?”
“Binti nimekueleza tatizo lako linahitaji muda zaidi, si la kukurupuka, we nenda halafu uje baada ya siku tatu nitakuwa nimeshapata jibu.”
“Nimekuelewa.”
“Haya nakutakieni safari njema.”
Waliagana na kuingia ndani ya gari na kurudi jijini Dar. 

CHINI YA BAHARI
Mtikisiko mkubwa katika stoo ya kutunzia vizazi vya wanawake ulimtisha mtwana mmoja aliyekuwa akilinda. Alitoka mbio hadi kwa mkuu wao Kulani kumuelezea kilichotokea.
“Umesikia nini?”

“Chumba chote kilikuwa kikitetemeka kama kinataka kubomoka kwa muda mrefu.”
“Kwa nini hukuja kunieleza?”
“Nilishindwa kuondoka kwa vile hapakuwa na wa kulinda hapa.”
“Baada ya kutulia umeona nini?”
“Sijaona kitu lakini mtikisiko ulikuwa mkubwa sana.”
“Mmh! Ngoja.”

Kulani alisema huku akiondoka na kwenda moja kwa moja kwa Mfalme Barami Hudirud, baba mzazi wa jini Balkis. Alipofika alipiga magoti mbele ya mfalme.
“Naam mtwana wangu mtiifu unasemaje?”
“Mfalme kuna tatizo.”

“Tatizo gani mtwana wangu mtiifu?”
“Mtukufu mfalme, chumba cha siri kumetokea na kitu kisicho cha kawaida.”
“Kitu gani hicho mtwana wangu mtiifu?”
“Mtukufu mfalme kumetokea mtikisiko ndani ya chumba cha siri, ambao si wa kawaida.”
“Mmh! Kuna tatizo, mama Balkis,” alimwita mkewe.
“Naam laaziz wangu.”

”Katika chumba cha kuhifadhia vizazi kumetokea mtikisiko usio wa kawaida sijajua kuna tatizo gani?”
“Mmh! Hata mimi ulinishtua lakini sikutaka kuuliza.”
“Basi nenda kaangalie kuna usalama kweli?”
“Sawa.” 

Malkia Huleiya aliongozana na Kulani hadi chenye chumba cha siri, alipofika alifungua mlango wa chumba cha kuhifadhia vizazi. Aliingia ndani ya chumba na kushangaa kukuta kasha la dhahabu la kuhifadhia vizazi limefunguka, nje ya kasha alishtuka kuona damu.
“Ooh! Tayari walimwengu wameanza matatizo yao, kwa hali hii sijui kama mwanangu ataolewa,” Malkia Huleiya alisema kwa masikitiko.
“Kwani vipi malkia?”

“Naomba mtoke nje,” Malkia Huleiya mama wa Balkis alisema bila kuwaangalia.
Kulani na mlinzi wa chumba kile walitoka nje na kumuacha peke yake, chini ya kasha sehemu iliyokuwa wazi kulikuwa na matone ya damu ambayo ilikuwa bado mbichi. Alipoishika ile damu iliganda kidoleni, dalili ile ilimjulisha moja kwa moja kuwa kizazi kimerudi kwa mwenyewe.

Alivihesabu vilivyobaki na kugundua kilichotoka ni kimoja, alifunga kasha na kurudisha sehemu yake kisha alifunga chumba na kurudi kutoa taarifa kwa mumewe.
Uso wake ulionesha huzuni, kitu kilichomtisha mumewe ambaye alitaka kujua kulikoni.
“Vipi mahabuba wangu?”

“Mambo yameharibika.”
“Kivipi?”
“Mpango wetu umeingia kwenye mtihani wa kwanza.”
“Mtihani upi?”

“Kizazi kimoja kimechukuliwa.”
 “Tufanye haraka kabla hakijarudishwa kwa mwenyewe tumtume  Kulani akaifanye kazi hii kabla hakujapambazuka.”
“Tumechelewa tayari kimesharudishwa kwa mwenyewe.”
“Umejuaje?”

“Damu ya sehemu kilipotoka nilipoigusa imeganda kidoleni.”
“Ooh! Nani anataka kuchezea himaya yangu? Lazima nimkomeshe,” Mfalme Barami Hudirud alisema kwa hasira.
“Hebu kaniletee damu ya sehemu iliyotoka kizazi ili nimjue ni nani?”

Kazi imeanza, Mganga Njiwa Manga kaichokoza himaya ya Jini Bahari. N-ini kitatokea? Kuyajua yote tukutane Siku yakesho.

No comments

Powered by Blogger.