ad

ad

AHADI YA NDOTONI - 12



ILIPOISHIA;
Baada ya kumaliza kuswali alirudi kwenye kochi na kumuuliza Lakashina:
“Mbona uswali?”
“Sina udhu,” alijibu kwa mkato.
“Una muda gani huswali?”
“Hata sikumbuki.”

“Mmh! Umekuwa mbuzi usiyekumbuka ulipotoka?”
“Wewe fanya kile kilichokuleta sihitaji vitu vingine visivyonihusu, kwanza dini yenyewe ngumu sina uhuru wa maisha.”
“Mmh! Kweli eeh.”

“Habari ndiyo hiyo, sema tu kila bwana anayenifuata ni Muislamu, bila hivyo ningerudia jina langu la Jeska.”
“Asante, nipe pete yangu,” Lakasina alinyoosha mkono kuomba pete yake.
Lakasina bila kusita aliivua pete ya ndoa na kumkabidhi Lakashi, Lakashi aliipokea: SASA ENDELEA...

“Asante, kuanzia leo upo huru kuolewa na mwanaume yeyote, ila utanitafuta na hutanipata tena.”
“Maisha yangu namtegemea Mungu si kiumbe kinachomtegemea Mungu kama mimi.”
“Asante.”

Baada ya kusema vile Lakashi alishika kwenye paji la uso na ghafla alitoweka kwenye kiti. Lakashina aliamini kwa kauli ya Lakashi alikuwa na nafasi ya kumjulisha Abdul Diabi kuwa yupo tayari kuolewa. Alichukua simu yake na kupiga kwa Abdul, baada ya kuita upande wa pili ulipokea.
“Haloo.”

“Haloo nazungumza na Abdul.”
“Hapana mimi ni mdogo wake.”
“Naomba kuongea naye.”
“Samahani Abdul amefariki ghafla sasa hivi hivi tupo katika harakati za kupeleka maiti yake hospitali kwa uchunguzi.”
“Ooh! Nimekwisha,” Lakashina alipiga kelele ya mshtuko alianguka chini na kupoteza fahamu.

***
Alipozinduka alijikuta amelala kwenye kitanda kilichoonesha sehemu ile ni hospitali. Taratibu alirudisha kumbukumbu alitokewa na kitu gani mara ya mwisho. Bado hakuamini alichokiwaza kweli kimetokea. Aliamini huenda ilikuwa ndoto na wala si kitu cha kweli.

Akiwa katikati ya dimbwi la mawazo aliingia msichana mmoja aliyekuwa katika vazi la uuguzi, alimsogelea kwenye kitanda chake na kumsalimia kwa lugha ya Kiswahili ambayo Dubai ilikuwa ikitumika sana kutokana na watu wengi wenye asili ya Kiarabu kutokea visiwani Zanzibar kuwa pale.

“Pole dada.”
“Asante.”
“Unaendeleaje?”
“Namshukuru Mungu, hata sijui nililetwa katika hali gani?”

“Mmh! Kwa kweli Mungu mkubwa, ulikuwa kwenye hali mbaya sana ila kuna kaka mmoja alifanya kazi ya ziada baada ya madaktari kukosa ufumbuzi.”
“Ufumbuzi wa nini?”

“Ulipoletwa hapa ulikuwa umeng’ata ulimi na macho kukutoka pima. Mganga mkuu alijitahidi kufanya anachokijua lakini hali haikubadilika. Lakini yule kaka ambaye amedai yeye ni msamaria mwema, aliwasaidia wafanyakazi wa hoteli uliyofikia kukuleta hapa.

“Baada ya kukuleta aliwaruhusu wafanyakazi waondoke na yeye kusema atakaa hapa mpaka mwisho kuhakikisha hali yako inarudi kawaida. Wakati wakiendelea kukufanyia huduma yeye alikuwa nje ya chumba cha matibabu. Ilichukua zaidi ya saa mbili bila kupatikana ufumbuzi, wakati mganga mkuu anatoka ndani ya chumba, yule kaka alimuuliza kinachoendelea. Mganga aliyekuwa akivuja jasho alimueleza kuwa hali yako bado ni mbaya hakuna mabadiliko yoyote.

Ajabu yule bwana aliyeonekana ni mtu wa ajabu kutokana na roho yake ya huruma, aliomba wampe nafasi na yeye ajaribu kutoa anacho kifahamu. Japo kwa sheria za kazi si rahisi kumuamini mtu asiye mfanyakazi wala kujua uwezo wake. Lakini kwa vile walikosa ufumbuzi walimruhusu.

Baada ya kumruhusu nao walikuwa pembeni yake waone anataka kufanya nini, aliomba mafuta ya nazi ambayo alinunuliwa kwenye maduka ya nje ya hospitali. Baada ya kuletwa aliomba yapashwe moto. Baada ya kupashwa, aliyachukua na kujipaka kisha alianza kukuchua taratibu. Kuanzia kifuani kwenda shingoni na kichwani. Ajabu ulimi ulirudi ndani na macho yalifumba , madaktari walishangaa sana.

Hakutaka kuendelea kuwepo pale kwa vile alikuwa na shughuli zake aliomba ruhusa, mganga mkuu alimruhusu baada ya vipimo vyote kuonesha unaendelea vizuri. Pia alikulipia fedha za matibabu na kuomba tusikupe dawa yoyote ukiamka urudi hotelini kwako ujiandae na safari.
“Eti ni kweli Abdul amefariki?” Lakashina alijikuta akiulizwa swali lisilomuhusu muuguzi.

“Mmh! Kweli nimekumbuka kabla ya kuondoka alinieleza jambo moja, kama ukiamka nikueleze.”
“Jambo gani?”
“Amesema kuwa kifo cha mumeo mtarajiwa Abdul akihusiani na mumeo wa zamani, ni amri ya Mungu.”
“Amejuaje?”
“Kwa kweli sikuwaza kumuuliza swali kama hilo, kwa vile sikuelewa anamaanisha nini.”
“Huyo mtu yukoje?”
“Mmh! Dada swali gumu lakini kama sikosei ana asili ya Kiarabu amevalia panjabi nyeupe na makubazi.”

“Mmh! Anaitwa nani?”
”Japo hakunitajia jina, lakini kutokana na jinsi alivyoonesha moyo wa huruma na upendo ilibidi nimuulize jina lake.”
“Alikujibu?”
“Ndiyo.”

“Anaitwa nani?”
“Lakashi.”
“Lakashiii?” Jina lile lilimshtua Lakashina.
“Ndiyo anaitwa Lakashi, kwani vipi, una mfahamu?”
“Kama ni yeye namfahamu.”

“Lakini mbona yeye anaonesha hakufahamu.”
“Mmh! Tuachane na hayo, kwa hiyo Abdul amefariki?”
“Kutokana na maelezo yake, amefariki.”
“Mungu wangu, haya sasa maisha gani nitakuwa mtu gani, kama Abdul amefariki lazima yeye anahusika tu.”

“Dada sikuelewi, una maana gani kusema yule kaka kamuua Abdul?”
Swali lile lilimshtua Lakashina na kukumbuka siri ile haikutakiwa watu waijue.
“Basi dada tuachane na hayo, naweza kuondoka?”
“Ngoja nikamwite daktari.”

Muuguzi alitoka nje ya chumba na kumuacha Lakashina akishindwa kuelewa Lakashi anataka nini kwake ikiwa wamekwisha achana. Lakini msaada wake nao ulimchanganya akili kwa kujitolea kuyaokoa maisha yake baada ya ugonjwa wake kuwashinda wataalamu wa utabibu.

Akiwa katikati ya mawazo mganga mkuu aliingia, baada ya kumfanyia vipimo vya mwisho alimruhusu kurudi hotelini kwake. Lakashina baada ya kutoka hospitali ili kupata uhakika alikwenda hadi katika duka alilokuwa akiuza Abdul. Alikuta limefungwa, alipouliza alipewa taarifa kuwa Abdul amefariki na atazikwa siku ile ile.

Hakuwa na jinsi zaidi ya kuondoka siku ile ile kurudi Tanzania, alipofika Tanzania alikuwa kama mgonjwa kutokana na matukio ya mfululizo ya vifo vya wanaume waliomtaka kimapenzi. Kutokana na kauli ya Lakashi aliyomueleza ya kukubali kuhusika na kifo cha Sadat lakini alikataa ahusiki na kifo cha Abdul. Alijua kauli ile ilikuwa ya kujikosha tu lakini kifo cha Abdul yeye ndiye mhusika.

Lakashina aliapa kuanzia kifo cha Abdul hatakuwa na uhusiano na mwanaume yeyote. Aliamua kuishi maisha ya kawaida si yale ya kujitunza kila wakati kuvaa nguo zinazouziba mwili wote. Aliyakumbuka maisha ya kihawara aliyokuwa akiishi na mzee Ezekiel, baba Edna enzi ya uhai wake.

Alianza kunywa pombe kuvaa mavazi ya nusu uchi hata kwenda sehemu za starehe.Vile vile jina lake alibadili na kujiita la zamani la Jeska, hakutaka tena kuitwa Lakashina kila aliyemwita jina hilo alikosana naye. Jeska kama alivyopenda kuitwa vile, kwa hasira vitu vyote alivyokatazwa na Lakashi alivifanya kwa fujo, huku akipuuza kauli yake ya kuwa akifanya kinyume kwa aliyomkataza yatamkuta makubwa. Aliingiza nyama ya nguruwe na pombe nyumbani kwake na kula na rafiki zake.

Aliogopa kuanzisha uhusiano na wanaume kuogopa kuwatoa kafara, aliamua kuelekeza mapenzi yake kwenye pombe akawa pombe na yeye, yeye na pombe. Muda mwingi baada ya kazi alikuwa akinywa pombe mpaka anapoteza uwezo wa kukumbuka. Watu wake wa karibu walimshangaa alivyobadilika, kutoka katika mavazi ya heshina na kuvaa ya nusu uchi huku akitumia kilevi muda mwingi.

Wiki moja akiwa kwenye kumbi za starehe alipigiwa simu na mlinzi wake kuwa nyumba yake inaungua. Alitoka ndani ya ukumbi akiwa amelewa na kuendesha gari kwa kasi ili kuwahi nyumbani. Baada ya mwendo mfupi gari lilisimama ghafla,  alipoangalia kwenye kioo kinachoonesha mita za gari ilimuonesha rejeta haina maji.

Alishangaa na kujiuliza kutokewa na hali ile, kwani magari yake alikuwa akiyatunza vizuri sana. Aliteremka baada ya joto la ndani ya gari kuzidi, alisogea pembeni huku pombe zikianza kumtoka. Alipotaka kufungua boneti gari lilikuwa la moto sana kitu ambacho kilikuwa kipya maishani mwake, gari kukaukiwa maji na kuunguza kama moto.

Akiwa bado anasikilizia maumivu ya mkono, sauti ya mtu ambaye hakumuona ilimueleza:
“Dada sogea mbali gari linalipuka sasa hivi.”
Alisogea mbali kidogo na gari haikuchukua muda gari lililipuka kama limepigwa na bomu. Alijikuta akizidi kuchanganyikiwa baada ya gari lake la thamani kuteketea huku akiliona. Akiwa bado anajifikiria afanye nini simu yake iliita tena:

“Dada upo wapi, nyumba yote inateketea,” ilikuwa sauti ya mlinzi aliyekuwa akilia.
“Mungu wangu mkosi gani huu! Umewapigia Faya?”
“Dada ni maajabu, watu wa Faya wamefika lakini ajabu ya Mungu wameshangaa maji waliojaza kutoka kama mate na tenki kuishiwa.”

“Mmh! Makubwa, huku na mimi gari lote limeteketea,” Jeska alisema kwa sauti ya kukata tamaa.
“Mungu wangu mkosi gani huu.”
“Kwa hiyo na magari yangu yote ?“
“Mama hakuna kilichobaki huu ni moto wa ajabu, sijawahi kuuona katika maisha yangu.”
“Na nyumba yangu?”

“Mama utafikiri hapakuwepo na nyumba yoyote”
“Mungu wangu nimekwisha Laka...nooo, Jeska miye.”
Mara simu nyingine iliingia ilikuwa ya mmoja wa wafanyakazi wake wa dukani.
“Dada upo wapi?”
“Nani Sakina?”

“Ndiyo dada, nimepigiwa simu kuwa duka lote limeteketea.”
“Atiii?”
“Yaani ninavyozungumza hivi nipo kwenye eneo la duka hakuna kilichobakia.”
Jeska nguvu zote zilimwisha, alianguka chini na kupoteza fahamu.

 ****
Alipozinduka alijikuta akiwa amelala juu ya kitanda cha hospitali, alijishangaa kujikuta akiwa na vazi la aibu la nusu uchi ambalo alitakiwa kulivaa kwenye kumbi za starehe tena akitoka ndani mwake na kuingia ndani ya gari siyo kutembea kwa miguu.
Baada ya kupata fahamu alipepesa macho na kuwaona watu wawili wakizungumza huku wamempa mgongo.  Mwanaume alionekana daktari kutokana na vazi lake la koti refu jeupe akiwa na muuguzi wa kike.

“Unasema huyu ndiye dada aliyekuwa akimiliki duka kubwa la nguo?” Daktari aliuliza.
“Ndiyo.”
“Si kweli?”
“Kwa nini?”
“Yule si anaitwa Lakashina, tena msichana aliyekuwa akijiheshimu kuna kipindi nilidhamiria kumuoa, lakini pete ya ndoa kidoleni kwake ndiyo iliyonifanya nisitishe zoezi langu. Lakini huyu mgonjwa si umesema anaitwa Jeska?”

“Ndiyo, nasikia aliachana na mumewe na kuamua kurudia dini yake na jina lake la zamani ikiwa pamoja na kutembea uchi kama unavyomuona, kunywa pombe na kufanya kila jambo la kumchukiza Mungu.”
“Labda alichanganyikiwa baada ya kuachwa!”
“Walaa, talaka kaitaka mwenyewe kwa vile alipata bwana mwingine.”
“Zubeda yote haya umeyajulia wapi?”

“Bosi, kaka aliyemleta hapa inaonekana anamfahamu vizuri.”
“Kivipi?”
“Baada ya kumleta alisema amemkuta dada huyu amelala barabarani akiwa amepoteza fahamu baada kutokewa na balaa la kuunguliwa moto vitu vyake.”
“Yeye alijuaje?”
“ Bosi, huo muda wa kumhoji kama polisi sikuwa nao isipokuwa msamaria mwema aliyemuokota na kumleta hapa alidai anamfahamu.”

“Alisema anaitwa nani?”
“Jeska.”
“Wewe huyu dada ulimfahamu kwa jina gani?”
“Lakashina.”
“Ulihoji kwa nini amwite Jeska badala ya Lakashina?”

“Kutokana na maelezo niliyokupa mwanzo kuwa baada ya kuachana na mume wake aliamua kurudia jina na dini yake ya zamani pia kurudia tabia zake chafu.”
“Mmh! Basi alikoelekea ni kubaya kuliko alikotoka, ona mavazi yake bila kuniambia, ningejua ni kahaba aliyeokotwa na wasamaria wema akijiuza kimwili.”
Muuguzi alipogeuka alimuona Jeska aliyekuwa akitokwa na machozi ya uchungu kwa kuilaumu nafsi yake kumshauri vibaya.

“Dokta naona kaamka.”
“Ooh! Vizuri.”
Daktari aligeuka na kusogea kitandani ambako Jeska alikuwa akiendelea kutokwa na machozi ya uchungu baada ya kupata ukweli wa kuunguliwa kwa mali zake zote nyumba, magari na duka.
“Pole sana,” daktari alimsemesha kwa sauti ya upole.
“Ni kweli vitu vyangu vimeungua?”
“Bado hatuna uhakika,” daktari alijibu.

“Hamna uhakika kivipi wakati nimesikia yote mliyokuwa mkizungumza?”
“Aliyozunguza ni msamaria mwema anayekufahamu, sikuweza kukubali mara moja mtu aliyekuokota njiani ajue kila kitu kilichokupata kuwa umeunguliwa sijui gari, gari lilionekana kweli limeungua, lakini nyumba na duka lako amejuaje?”
“Kwani aliyenileta alisema anaitwa nani?”

Itaendelea siku ya kesho.
Like: www.facebook.com/2jiachie
Web: www.2jiachie.com


No comments

Powered by Blogger.