She is too young to die (4)
Gilbert anamruhusu mke wake
mjamzito Salome kwenda kijijini kwao
huko Kahunda Sengerema kuwaona wazazi wake kabla hajajifungua! Akiwa
huko, mvua kubwa zinanyesha yakiwa
yamebaki masaa machache tu kabla hajaondoka kurejea Dar es Salaam ambako yeye
na mume wake wanaishi maisha ya kifahari, Gilbert akiwa Mkurugenzi wa kampuni
yake binafsi iliyojishuhusisha na masuala ya kompyuta, WorldCom Ltd.
Madaraja yote yamevunjika na kuna
mafuriko ya kutisha, kifupi eneo lote la Kahunda limekuwa kisiwa na hakuna
mawasiliano kati ya Salome na Gilbert jambo ambalo limefanya achanganyikiwe
kabisa hasa kwa sababu anafahamu siku za mke wake kujifungua zimefika!
Akitafakari nini cha kufanya anapata ujumbe wa
polisi kwamba mke wake yu katika hali mbaya, anavuja damu nyingi kabla
ya wakati na huko aliko hana jinsi ya kutoka.
Jambo hili linamfanya Gilbert
afikie uamuzi wa kukodisha helkopta ambayo
anaruka nayo kutoka Dar es Salaam
hadi Mwanza na baadaye kuelekea maeneo
hayo, alichokishuhudia akiwa angani kilimsikitisha! Maeneo yote yalikuwa
yamejaa maji, nyumba nyingi zilikuwa zimebakiza mapaa tu juu, akaamini mke wake alikuwa kwenye matatizo
makubwa! Moyoni mwake akajuta ni kwanini
alimruhusu Salome aende kwao.
Upande wa pili Salome anachukuliwa
katika gari la kukodi kwenda wilayani Sengerema ambako kuna hospitali
kubwa, hali yake ni mbaya lakini walipofika kijiji la Bilulumo walikuta daraja
kubwa limevunjika, hakuna mahali pa
kupita! Je, nini kitaendelea? SONGA
NAYO…
“Vipi baba?” Mama yake Salome
aliyekuwemo ndani ya gari akibubujikwa na machozi bila kutoa sauti alimuuliza
dereva.
“Mama hapa hatuwezi kupita!”
“Tutafanyaje mwanangu, kweli Salome
afie hapa?”
“Sina jinsi mama!”
“Gari yako haiwezi kupita kwenye maji?”
“Haiwezekani, itavutwa na sote
tutakufa! Nashauri tumtegemee Mungu”
Mama
alinyanyuka mahali alipokuwa ameketi ndani ya gari na kushuka chini
ambako watu wote walimshuhudia akipiga magoti
na kuanza kusali huku akilia na machozi yake kuchukuliwa na matone ya mvua yaliyokuwa
yakidondoka mashavuni mwake! Alionekana kabisa kukata tamaa ya mwanae
kupona, nusu saa baadaye aliponyanyuka
uso wake ulikuwa umejaa tabasamu,
akapandisha tena kwenye gari na kumgusa Salome usoni, mwili wake wote
ulikuwa wa baridi na damu ziliendelea kutiririka na kuchafua
sakafu ya gari.
“Pole mama!” dereva aliongea.
“Katika hili napaswa kumwamini Mungu,
kwa imani mwanangu Salome atapona! Mungu
ninayemwabudu ana nguvu, uwezo wangu umekomea hapa, lakini ninapokomea mimi ndipo yeye anapoanzia!”
aliongea mama huyo uso wake ukiwa umekunjuka kuliko alivyokuwa kabla hajasali.
Baada ya kusema maneno hayo mama huyo alilala kando ya mtoto wake na
kumkumbatia akitarajia muujiza wa Mungu utokee. Akili yake ikamrudisha nyumbani, akamkumbuka mumewe na namna
alivyoondoka usiku kwa lengo la kwenda nyumbani kwa mkunga mama Mataluma lakini
hakurejea tena! Hakuwa na jibu juu ya kitu gani kingempata lakini alikuwa na
uhakika kutoka moyoni mwake lazima alipatwa na jambo baya, alikuwa baba mzuri mno kukimbia tatizo la
mtoto wake.
“Najua yuko tayari kufa kwa sababu ya
mtu anayempenda, iweje leo amkimbie
Salome? Atakuwa amepata tatizo kubwa” aliwaza akiwa amemkumbatia mwanae.
***
“Hapa kuna mwinuko kidogo, tunaweza
kutua kwenye huu uwanja!”
“Wewe tu, nakutegemea wewe rubani,
ninachotaka mimi ni kumpata mke wangu!”
“Haya tulia, nashuka sasa. Umefunga
mkanda?”
“Hapana!” aliitikia Gilbert
“Funga haraka!” Rubani aliamuru.
Gilbert alipotekeleza hilo, Rubani
kwa taratibu alianza kuishusha
helkopta chini na kuikaribia ardhi, hatimaye ikatua kwenye uwanja ulionekana
kuwa wa shule. Kilikuwa ni kitu kigeni
sana kwa helkopta kutua katika maeneo hayo, jambo lililofanya wanakijiji waanze
kukimbia kutoka sehemu mbalimbali kuelekea uwanjani kwenda kuishangaa, ndani ya
dakika kumi na tano tu tayari ilishazungukwa na wananchi wakiishangilia na wengine kusogea karibu
kuigusa.
“Habari
yako ndugu yangu?” Gilbert alimsalimia mzee mmoja aliyekuwa jirani yake.
“Nzuri tu habari za leo?”
“Salama!”
“Poleni na mafuriko!”
“Ahsante bwana, vipi mmetuletea misaada?”
“Hapana, mimi naitwa Gilbert, natokea Dar es Salaam,
mwenzangu?”
“Naitwa Mwalimu Mchele, ndiye mkuu wa
shule hii! Wewe Gilbert gani? Uliyemuoa Salome?”
“Unamfahamu?”
“Ah! Kuna mtu asiyemfahamu Salome
huku?”
“Basi huyo ndiye mke wangu, nimemfuata!”
“Nilisikia yuko kijijini kwao Kasheka,
atakuwa hajaondoka kweli?”
“Ilikuwa tayari awe amekwishaondoka
lakini mvua zikamfungia huku, bahati mbaya sana hivi sasa anaumwa na yuko katika hatari ya kufa kwa
sababu ya kuvuja damu nyingi! Naomba unisadie kufika kijijini kwao!”
“Hakuna shida, twendeni tu!”
“Ni umbali gani kutoka hapa?”
“Kilometa ishirini na tano hivi!”
“Tunaweza kupata baiskeli?”
“Kwani hii helkopta yenu haiwezi kuruka
na kutua kijijini kwao?”
“Hakuna sehemu ya kutua, kote kumejaa
maji!”
“Basi twendeni kwa miguu maana baiskeli
nina uhakika haitatusaidia chochote, barabara ni mbovu mno, tutafika tumeibeba”
“Sawa! Hata kama ni kukimbia tutafanya
hivyo!”
Mwalimu Mchele na kwenda nyumbani kwake kuaga na wakaondoka hadi kijiji cha Bupandwa ambako
pia walikuta daraja limejaa maji,
wakavushwa kwa mtumbwi hadi upande wa pili wakaendelea kwa miguu, sehemu zenye maji mengi wakivushwa mpaka
wakaingia kijiji cha Kasheka wakiwa wamepita
njia ya mkato iliyokatisha katika
kijiji cha Chamanyete. Wakiwa kijijini kwao
na Salome walinyoosha moja kwa moja nyumbani kwao, njiani wakakutana na watu wengi waliobeba
maiti wakiongoza kwenda njia waliyokuwa wakienda wao.
“Poleni wazee!” Gilbert aliwaambia
baada ya kusalimiana na baadhi yao.
“Ahsante, mzee wetu bwana hapa kijijini
jana usiku alichukuliwa na maji ya mvua hadi mtoni ambako alizidi kuvutwa mpaka
ziwani, akafa!”
“Aisee, bahati mbaya kwa kweli!”
mwalimu Mchele aliingilia kati.
“Tena bahati mbaya sana kwake, binti
yake mmoja anayeishi Dar es Salaam pia
ana hali mbaya kupita kiasi, usiku alianza kuvuja damu nyingi mzee akaondoka
nyumbani kwenda kumtafuta mkunga, ndipo alipokutana na kifo cha…” mwanakijiji
huyo hakumalizia sentensi yake, akashtuka
alipomwona Gilbert akiangua kilio.
“Masikini mzee……………………?”
“Unamfahamu?”
“Mkwe wangu, huyo binti yake uliyemtaja ndiye mke
wangu, mimi naitwa Gilbert!”
“Aisee kumbe ni wewe, mimi naitwa
Innocent, pole sana aisee!”
“Ahsante, kwa hiyo mke wangu yuko wapi?”
“Waliondoka asubuhi kwa machele hadi
kijiji cha Mwangika ambako walikodisha Landrover kuwapeleka Sengerema lakini taarifa
nilizonazo ni kwamba hawajafika, huko mbele kuna daraja limevunjika, wapo hapo
mpaka hivi ninavyoongea na wewe!”
Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Jumatatu


Post a Comment