ad

ad

She is too young to die -3


Baada ya kupata taarifa za mkewe kukwama kijijini kwao  alipokwenda kusalimia, hali yake ikiwa mbaya, kijana  mwenye mafanikio kifedha  akimiliki kampuni ya kuuza kompyuta iitwayo WorldCom, Gilbert anaamua kukodisha helkopta kwenda eneo la tukio kumwokoa mke wake lakini akiwa angani kwenye kijiji hicho haoni kitu chochote zaidi ya maji na rubani anamwambia hapakuwa hata na mahali pa helkopta kutua! Je, nini kitaendelea? SONGA NAYO…

  Yalikuwa yamebaki masaa  matano kabla basi la Nyehunge Express  kutoka Kahunda kwenda Mwanza halijampitia  Salome  kwenye kijiji cha  Mwangika  kumpeleka Mwanza ambako angepata ndege siku hiyo hiyo na kurejea Dar es Salaam, mvua kubwa  ilipoanza kunyesha.
Ilikuwa kubwa kuliko zote zilizowahi kutokea katika ukanda huo,   watu wazima waliokuwepo tarehe 9, desemba mwaka 1961, siku ambayo Tanzania ilipata uhuru waliifananisha mvua hiyo na ya Uhuru lakini hata hivyo bado walikiri ilizidi kwa wingi wa maji yaliyokuwa yakipita juu ya ardhi kama mito. Nyumba nyingi zilikuwa zimejaa maji, mito ilifurika ndani ya muda mfupi na kuwafanya watu kushindwa kutoka ndani ya nyumba zao.
Salome alikuwa ndani ya kibanda kidogo nyumbani kwao, ambacho ndani yake tayari kilishajaa maji mpaka miguuni, pembeni mwake alikuwepo mama yake akimtuliza na kumwondoa wasiwasi juu ya safari yake, maneno yakiwa yale yale kwamba mvua ingekatika na angepelekwa barabarani ambako angepanda basi na kuondoka lakini hali haikuwa hivyo, mvua ilizidi kumwagika,  upepo  mkali  ulizidi kuvuma na kuezua mapaa ya nyumba nyingi, hakuna aliyekuwa na uhakika wa kubaki salama! Waumini wa dini ya Romani Katoliki walikuwa na Rozali zao mikononi,  wakimwomba Mungu awanusuru,  kila mtu alisali kwa dini yake ili balaa lililokuwa mbioni kutokea lipite tu.
“Nilitaka kuondoka juzi, lakini nikasita…sasa unaona balaa linanikuta? Nitafanya nini mimi na tarehe zangu za kujifungua zimewadia?”  aliwaza Salome akilia huku mama yake akimpigapiga mgongoni, kichwa chake kilikuwa kikimuwazia Gilbert  na mtoto aliyekuwemo tumboni. Ghafla tumbo likaanza kumuuma.
Mwanzoni alifikiri ni tumbo la kawaida ambalo lingeacha baada ya muda mfupi lakini haikuwa hivyo, lilizidi kupamba moto! Kichwani akaanza kutafakari kama labda alikuwa amekosea kuhesabu tarehe zake za kujifungua lakini akagundua alikuwa sahihi, kulikuwa bado kuna wiki tatu mbele. Bila kutegemea alisikia akilowa katikati ya miguu yake na kuhisi kitu kama maji kilikuwa kikipita taratibu.
“Mh! Nini tena?” alijiuliza na kunyanyuka mahali alipokuwa kuingia chumbani akipita  ndani ya maji, akapandisha nguo alizokuwa nazo juu na kumulika kwa kibatari, hakuamini alipoona damu inatoka!
“Mama! Mama!” aliita.
“Bee!
“Hebu njoo!”
“Kuna nini?”
“Njoo tu!”
Mama yake akaingia ndani ambako Salome hakutoa maelezo kwa mdomo zaidi ya kumfunulia mama yake na kumwonyesha nguo zake za ndani, alipoiona damu yeye mwenyewe alishtuka na kumuuliza kama siku zote za kujifungua zilikuwa zimefika maana halikuwa jambo la kawaida  hata kidogo kuona   mama mjamzito akitokwa na damu sehemu za siri.
“Siku bado mama,  bado kama siku ishirini na moja hivi!”
“Sasa hii damu inatoka wapi?”
“Hata mimi sijui!”
“Hebu ngoja nimwambie baba yako akamwite mama Mataluma aje atuambie tatizo ni nini!”
“Sawa mama, fanyeni hivyo,  tumbo linaniuma sana!” Salome alikubali, kwa jinsi hali ilivyokuwa ikizidi kubadilika hakuwa na  la kufanya tena, kwake lolote ambalo lingeweza kusaidia lilikuwa ni sawa!
Baba yake alichukua panga na kutoka nje kulikokuwa na mvua na upepo mwingi, isingekuwa ni  kwa sababu ya tatizo  la mtoto wake hakika asingetoka nje ya nyumba yake usiku huo, hali ilikuwa mbaya mno! Maji mengi yalikuwa yakipita  pamoja na magoto makubwa, alitamani kurudi ndani lakini alipomfikiria Salome alianza kukanyaga ndani ya maji akienda mbele,  mara kadhaa akidumbukia kwenye mashimo na kuanguka lakini hakukata tamaa,  kulikuwa na  kilometa mbili mpaka kufika nyumbani kwa mama Mataluma,   lakini ilikuwa ni lazima afike.
Mbele kidogo akiwa peke yake njiani, alishtukia wimbi kubwa la maji likija kwa kasi na kumzoa, akajitahidi kwa uwezo wake wote kusimama lakini haikuwezekana maji yakaanza kumvuta kumpeleka chini kulikuwa na mto! Alilia na kupiga kelele lakini hakukuwa na msaada wowote, mbele alijaribu kushika mzizi lakini akang’oka nao na kuzidi kupelekwa mbele hatimaye pumzi ikaanza kumpungua,  giza likaingia machoni na hakujua kilichoendelea baada ya hapo.
Salome na mama yake waliendelea kusubiri kwa karibu masaa manne bila mzee ………………kurudi, vichwani mwao wakafikiri labda alikuwa amefika kwa mama Mataluma lakini akashindwa kurudi. Muda wote huo Salome aliendelea kuvuja damu huku akilalamika maumivu makali ya tumbo, kwake haikuwa shida kuketi na kulala majini tena! Hisia za kifo kabla hajakutana na Gilbert zikaanza kumwingia kichwani mwake.
Saa kumi na mbili asubuhi hali ya Salome ikiwa mbaya mvua ilipungua, mama yake akatoka nje ya nyumba na kuanza kupiga mayowe akiwaita watu waje kumsaidia,  nusu saa baadaye nyumba yake ilishazungukwa na wanakijiji wakitaka kufahamu nini kilikuwa kimetokea, miongoni mwao alikuwepo mzee Mataluma,  mume wa mama Mataluma.
“Mwanangu anaumwa sana!”
“Nini?”
“Ni mjamzito,  damu nyingi zinamtoka, anahitaji msaada wa haraka vinginevyo atakufa!”
“Baba yake?”
“Aliondoka usiku kwenda kumwita mama Mataluma lakini bado hajarejea mpaka hivi sasa!”
“Mbona kwangu hakufika?” mzee Mataluma aliingia kati.
“Kwa kweli sifahamu, naomba tu mnisaidie kwanza huyu mtoto apate msaada!”
“Yuko wapi?”
“Ndani!”
Wanakijiji waliingia na kumkuta Salome amelala chini kwenye maji yaliyobadilika rangi na kuwa mekundu sababu ya damu aliyokuwa akivuja! Ilikuwa ni hali ya kutisha, walipomwita aliitika na kuwaeleza juu ya maumivu aliyokuwa nayo, hakuna alichoomba zaidi ya kufikishwa hospitali haraka.
“Au mpigieni mume wangu simu!”
“Salome umesahau kwamba huku hakuna simu mwanangu?” Mzee mmoja aliongea.
“Tumbeneni kwenye machela mpaka barabarani angalau tutafute gari ya kukodi twende Sengerema,  Mungu atatusaidia tutamfikisha salama!”
“Haya sawa!”
Wakakubaliana na kuchukua kitanda  cha kamba ambacho wazazi wake walitumia na kumlaza juu yake, kisha  kuanza kutembea haraka kuelekea  kijiji cha Mwangika kilichokuwa  barabarani, huko ndiko magari yalipatikana. Walifanikiwa kumfikisha akiwa salama na wakafanikiwa kupata Landrover ya kukodi kwa gharama ya shilingi laki moja kwenda Wilayani Sengerema, akapakiwa ndani yake pia mama akakubali kufuatana naye na safari ikaanza wakipita kwa taabu kwenye vijiji vya Bupandwa, Kafunzo kwa  sababu ya wingi wa maji barabarani,  walipofika kijiji cha Bilulumo, walikuta daraja kubwa limevunjika, maji ya mto yakipita juu! Magari yaliyotokea upande wa pili yakiwa yameshindwa kuvuka.
“Hapa hatuna jinsi tena!” dereva wa Landrover alisema akitingisha kichwa chake.
“Vipi baba?” mama yake Salome aliuliza.
“Mama hapa hatuwezi kupita!”
Salome alikuwa kimya, wala hakuelewa kilichoendelea damu nyingi zikimtoka. Muda huo huo mvua kubwa ikaanza kunyesha tena na maji yakazidi kujaa mtoni.
Je, nini kitaendelea? Fuatilia

No comments

Powered by Blogger.