ad

ad

MAZOEZI YA YANGA TANGANYIKA PAKERS

First Eleven Yanga hii hapa
SIKU chache baada ya Charles Mkwasa kujiunga na Yanga akitokea Ruvu Shooting, amekianika kikosi chake cha kwanza ambacho inaonyesha ndicho atakachokitumia.
Kikosi cha kwanza, maarufu kama First Eleven chini ya Mkwasa, kinaonekana kuwa na mabadiliko kidogo sana.
 

Ila baadhi ya wachezaji waliokuwa wanaaminiwa na Brandts aliyetupiwa virago hivi karibuni, wanaonekana watakaa benchi kwa Mkwasa.
 

Mkwasa ambaye amejiunga na Yanga kama kocha msaidizi, hivi sasa ndiye anaongoza mazoezi ambayo juzi na jana yalifanyika kwenye Viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar.
 

Katika mazoezi hayo, Mkwasa alipanga vikosi viwili, kimoja kikionekana ndiyo kitakuwa First Eleven.
 

Kikosi cha kwanza ambacho ndiyo hasa chenyewe, kilikuwa hivi; Deogratius Munishi 'Dida', Juma Abdul, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Haruna Niyonzima, Hassan Dilunga, Jerry Tegete, Emmanuel Okwi na Hussein Javu.
Kikosi cha pili kilikuwa hivi; Juma Kaseja, Issa Ngao, David Luhende, Rajab Zahiri, Ibrahim Job, Hamis Thabiti, Hamis Kiiza, Nizar Khalfan, Said Bahanuzi, Reliants Lusajo na Abdallah Mguhi ‘Messi’.
 

Hata hivyo, kitaalamu, kipa anayecheza kikosi cha kwanza, hupangwa dhidi ya washambuliaji tegemeo, maana yake, Kaseja ndiye anarudi kuwa kipa namba moja.
Lakini inaonekana Twite amepewa nafasi ya Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliyekuwa majeruhi na Domayo rasmi amechukua nafasi ya Athumani Iddi ‘Chuji’ aliyesimamishwa. Brandts alikuwa akiwatumia wawili hao kulingana na uzito wa mechi.
 

Kingine tofauti alichokifanya Mkwasa ni kumchezesha mshambuliaji Hussein Javu pembeni badala ya katikati huku akimrudisha Tegete ambaye hakuwa akipewa asilimia mia na Brandts.
 

Brandts zaidi alipenda kuwatumia Didier Kavumbagu na Hamis Kiiza nafasi ambayo ameichukua yeye Tegete na ile ya Kiiza amepewa Okwi.
 

Hata hivyo, Mkwasa anaweza kuendelea kufanya mabadiliko ya kikosi chake hicho kulingana na siku zinavyokwenda na ushiriki wa wachezaji hao mazoezini.
Taarifa kutoka ndani ya benchi la ufundi la Yanga zinasema: “Kweli hicho ndiyo kikosi, kama atakifanyia mabadiliko ni kidogo sana na hiyo itakuwa ni baada ya kupona kwa Mrisho Ngassa ambaye ameanza mazoezi.
 

"Huenda Tegete ataondoka pale, ila inategemea na atajituma vipi. Ila amewakubali sana Javu na Dilunga, lakini pia Kaseja amewekwa upande mwingine kwa maana maalum, naamini huyu ndiye kipa namba moja lakini kocha alitaka kujaribu kitu, hivyo Dida atakuwa anasubiri," alisema kiongozi huyo.
 

Alisema Nadir Haroub 'Cannavaro' na David Luhende wamepoteza sifa ya kuwa katika kikosi hicho kutokana na viwango vyao kushuka na mfano mzuri ni mechi ya Nani Mtani Jembe waliyolala 3-1 kwa Simba, hivyo watalazimika kufanya kazi ya ziada.
Alipoulizwa Mkwasa kuhusiana na pangapangua hiyo, alijibu kwa kifupi: "Muda ukifika kila kitu kitakuwa wazi, kikosi huwa hakifichiki."
Powered by Blogger.