Mahakama ya Rufaa Yawakana CHADEMA
Mahakama ya Rufaa imesema hakuna rufaa ya uchaguzi wa Jimbo la Longido iliyopo mahakamani hapo.
Mahakama
imetoa kauli hiyo wakati Chadema ikiilalamikia Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) kuhusu kufanyika uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo hilo
kwa madai kwamba kuna kesi mahakamani hapo.
Uchaguzi
huo mdogo ulifanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa Longido kwa tiketi ya
Chadema, Onesmo ole Nangole ushindi wake kutenguliwa na Mahakama Kuu.
Mara
kadhaa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Ole Nangole wamekaririwa
na vyombo vya habari wakidai kwamba kuna rufaa katika Mahakama ya
Rufani.
Viongozi
hao wamekuwa wakiilalamikia NEC kuwa iliendesha uchaguzi mdogo katika
jimbo hilo wakati rufaa ya kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomvua
ubunge Ole Nangole ikiwa haijatolewa uamuzi.
Hata
hivyo, Mahakama ya Rufaa imesema uchaguzi mdogo uliofanyika Longido
ulikuwa halali kwa kuwa hakuna rufaa yoyote iliyoko mahakamani hapo.
Naibu
Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Elizabeth Mkwizu amesema hakuna rufaa
yoyote kupinga hukumu ya uchaguzi wa Longido iliyoko mahakamani hapo,
bali kuna maombi.
“Hapa
hatuna rufaa ya uchaguzi wa Jimbo la Longido, bali kuna maombi ya
kuongezwa muda wa kuwasilisha ‘notice of appeal’ (taarifa ya kusudio la
kukata rufaa). Walileta notice of appeal lakini ikatupiliwa mbali, sasa
wanaomba muda ili waiwasilishe tena,” alisema na kuongeza:
“Maombi si rufaa, kwa hiyo haya maombi yasingeweza kusimamisha shughuli za uchaguzi.”
Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Mahakama ya Rufaa, maombi hayo yamepangwa kusikilizwa na Jaji Jacob Mwambegele Februari 5.
Wakati
wa usikilizwaji wa maombi hayo, mwombaji kupitia kwa mawakili wake
atalazimika kutoa sababu za kuiridhisha Mahakama ni kwa nini alichelewa
kuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa.
Ikiwa
Mahakama haitaridhika na sababu zake, itatupilia mbali maombi hayo
lakini ikiridhika nazo itamruhusu kuwasilisha taarifa ya kusudio la
kukata rufaa.
Baada
ya kuwasilisha taarifa hiyo, atasubiri kupata kumbukumbu za rufaa,
yaani nyaraka zitakazohusika kwenye rufaa yake, ikiwamo hukumu
anayoilalamikia, mwenendo wa kesi ya msingi na vielelezo vilivyotumika.
Akipata
nyaraka hizo, ndipo atakapowasilisha rufaa kamili, yaani sababu za kwa
nini anapinga hukumu iliyomvua ubunge wa jimbo hilo, na upande wa pili
(wajibu rufaa) nao utawasilisha hoja zake na baada ya Mahakama
kusikiliza hoja za pande zote ndipo itatoa hukumu.
Ole
Nangole alivuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Juni 29, 2016
kutokana na kesi ya uchaguzi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa kiti
hicho kwa tiketi ya CCM, Dk Steven Kiruswa akipinga ushindi wake.
Baada
ya Mahakama kumvua ubunge, Ole Nangole kupitia mawakili John Materu na
Dancan Oola aliwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa kupinga
hukumu hiyo.
Hata hivyo, taarifa hiyo ya kusudio la kukata rufaa ilitupiliwa mbali na Mahakama kutokana na kasoro za kisheria.
Baada
ya kutupiliwa mbali, kwa kuwa muda wa kisheria wa siku 14 za
kuwasilisha kusudio la kukata rufaa ulikuwa umeshaisha, waliwasilisha
maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha taarifa hiyo.
Maombi hayo pia yalitupiliwa mbali na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, ndipo wakapeleka maombi Mahakama ya Rufani.
Post a Comment