Brazil, Hispania kiama leo -Kombe la Mabara katika mechi ya fainali.
MABINGWA wa dunia, Hispania, leo wanakabiliwa na kibarua kigumu
cha kuivua Brazil taji la Kombe la Mabara katika mechi ya fainali
itakayochezwa usiku kwenye Uwanja wa Maracana, jijini hapa.
Timu hizo zinakutana zikiwa na rekodi tofauti, Hispania ikiwa bingwa wa dunia na Kombe la Ulaya,
Brazil ni mabingwa wa kihistoria wa Kombe la Dunia wakijitwisha mara tano na mara tatu Kombe
la Mabara, mwaka 1997,2005 na 2009.
Hiyo inazifanya timu hizo zishuke dimbani zikiwa na hofu kutokana na
zote kucheza soka ya kiwango cha juu, ingawa Brazil inashika nafasi ya
22 kwa ubora wa soka duniani huku Hispania chini ya kocha wake Vicent
del Bosque ikiwa nafasi ya kwanza.
Hispania wanashuka dimbani wakiwa na nguvu ya kutosha kupigania rekodi
ya kuwa timu ya kwanza duniani kutwaa mataji manne makubwa mfululizo,
baada ya kutwaa ubingwa wa Mataifa ya Ulaya ‘Euro 2008,’ Kombe la Dunia
2010 na Euro 2012.
Kwa Hispania, ni fainali ya kwanza baada ya mwaka 2009 kufungwa na
Marekani mabao 2-0 katika hatua ya nusu fainali. Wafungaji walikuwa Jozy
Altidore dakika ya 27 kabla ya Clint Dempsey kufunga la pili dakika ya
74.
Kipigo hicho kikaipeleka Hispania katika mechi ya mshindi wa tatu,
ambapo walifanikiwa kuwafunga wenyeji Afrika Kusini mabao 3-2 katika
muda wa nyongeza baada ya kumaliza dakika 90 kwa sare ya 2-2.
Wakati Hispania wakiwania rekodi hiyo, Brazil wanaingia Maracana
wakitaka kutwaa taji la tatu mfululizo la michuano hiyo baada ya kutwaa
miaka ya 2005 na 2009, ambalo litakuwa la nne katika historia ya nchi
hiyo, baada ya awali kutwaa mwaka 1997.
Hispania inatoka kuifunga Italia kwa mikwaju ya penalti 7-6, katika
nusu fainali, iliyoisha kwa sare ya 0-0 kwa dakika 120 za mpambano huo
juzi, saa 24 baada ya Brazil kutangulia fainali kwa kuichapa Uruguay kwa
2-1.
Ingawa dunia inaishuhudia Hispania iliyoimarika katika miaka ya
karibuni, Brazil wameonesha uimara mkubwa katika michuano hii na nyota
wao wakiongozwa na Neymar, wana hamu ya kushinda wakiwa Maracana, dimba
ambalo Brazil ilitwaa Kombe la Dunia mwaka 1970.
“Timu hizi zina historia na utamaduni mkubwa wa soka. Hispania wana
nyota mahiri kikosini, hali kadhalika iko hivyo kwa Brazil,” amekaririwa
akisema Neymar, muda mfupi baada ya Hispania kuitoa Italia na kuwafuata
‘Samba Boys’ fainali.
Hata hivyo, Neymar na wenzake wanakabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka
kwa nguli wa zamani wa soka ya nchi hiyo na dunia, Pele, ambaye anadai
kuwa kikosi cha sasa cha Brazil hakina ‘nguvu ya kutosha’ kuambulia
kombe ama zawadi za daraja la juu.
Kocha wa Brazil, Luiz Felipe Scolari, amesema: “Hispania imeshinda
kila kitu katika kipindi cha miaka mitano au sita iliyopita. Lakini sisi
tutacheza katika aina yetu ya mchezo,” alisisitiza, huku akikana
kuwabeza wapinzani wao baada ya kufuzu kwa mikwaju ya penalti.
“Wao walianzia katika mechi laini, hatua ya makundi ilikokuwa kundi
moja na nchi dhaifu ya Tahiti. Sisi bado tunawaheshimu wao, lakini
tutaonesha na kuthibitisha ubora wetu dimbani,” alisisitiza Scolari.
Wakati Brazil ilichomoka kutoka kundi A, ikizipiga kumbo Italia,
Mexico na Japan, mpinzani wake Hispania, alitokea kundi B, akizipiku
timu za Uruguay, Nigeria na Tahiti.
BBC Sport/Super


Post a Comment