MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi imetupilia mbali mashitaka yaliyokuwa yamefunguliwa na serikali dhidi ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA) kwa madai ya kumtukana Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya
Dodoma imetupilia mbali mashitaka yaliyokuwa yamefunguliwa na serikali
dhidi ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA) kwa madai ya
kumtukana Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Eliezel Luvanda
alitupilia mbali mashitaka hayo kutokana na hati ya mashitaka dhidi ya
mbunge huyo kuwa na upungufu.
Luvanda alisema kwa mujibu wa kifungu cha sheria cha 132 (20) hati
hiyo haikuwa na maelezo ya kutosheleza kuonesha ni lugha gani iliyodaiwa
kuwa ni ya matusi aliyotumia mshitakiwa huyo dhidi ya Pinda.
Awali akisoma hati hiyo, Mwendesha Mashitaka, Hariet Lopa alidai kuwa
Juni 24 mwaka huu akiwa katika Manispaa ya Dodoma, Mbilinyi aliweka
ujumbe wenye lugha ya matusi dhidi ya Waziri Mkuu Pinda kinyume cha
sheria.
Kabla ya hakimu kutoa hukumu hiyo, wakili na mwanasheria wa CHADEMA,
Tundu Lisu, aliwasilisha utetezi wake mbele ya mahakama hiyo akiitaka
kuitupilia mbali kesi hiyo kwa vile hakuna matusi yanayotajwa yakidaiwa
kutolewa na mbunge huyo dhidi ya Pinda.
Lissu alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha sheria cha 132 (20), hati
hiyo haikuwa na maelezo ya kutosheleza kuonesha ni lugha gani
iliyotumika na ni matusi gani, hivyo haiwezi kuwa kesi ambayo inaweza
kuendelea kusikilizwa.
Lissu alidai kuwa maneno yanayodaiwa yangesababisha uvunjifu wa amani
hayakutajwa katika hati hiyo huku akihoji upande wa mashitaka unataka
Sugu ajitetee kwa shitaka lipi.
Aliendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa kama hati hiyo ya mashitaka
iliyopelekwa mahakamani hapo itaendelea kutumika, itakuwa imekiuka
sheria, hivyo akaitaka mahakama hiyo kuifuta kesi hiyo.
Hakimu Luvanda alipomtaka mwendesha mashitaka wa serikali kujibu hoja
ya Lissu, alishikilia msimamo wake na kuiomba mahakama kuendelea
kuisikiliza kesi hiyo kwa madai kuwa ni mpya, hivyo makosa ambayo yapo
yatafanyiwa marekebisho wakati shauri likiendelea.
Hata hivyo Lissu alipinga kauli ya mwanasheria wa serikali kwa madai
kuwa hati ya mashitaka ni chafu na imeandaliwa ovyo, hivyo mahakama
kukubali kuendelea kusikiliza kesi hiyo ni kosa na hivyo ni vyema
ikatupiliwa mbali.
“Mheshimiwa hakimu naomba kesi hii itupiliwe mbali kwa kuwa hati ya
mashitaka ni chafu na ni ya ovyo.
Naomba itupiliwe mbali na mtuhumiwa
aachiwe huru,” alisema Lissu na kuongeza kuwa wapo tayari hata kesho
kuendelea na kesi hiyo ikiwa serikali itaandaa hati sahihi.
Hata hivyo, baada ya hakimu huyo kutoa hukumu hiyo, mwendesha
mashitaka alidai wataendelea na upelelezi na ukikamilika wataandaa hati
mpya.
Akizungumza mara baada ya hukumu hiyo, Lissu alisema mahakama hiyo
imetenda haki na kama upande wa mashitaka haukuwa umeridhika na hukumu
hiyo, ujipange upya na kupeleka hati ya mashitaka.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) alisema hata
hivyo kufutwa kwa kesi hiyo hakumaanishi mteja wake hawezi kushitakiwa
tena, kwani bado Waziri Mkuu Pinda anaweza kwenda polisi kutoa maelezo
kama anaona kweli ametendewa kosa hilo.
Kwa upande wake, Sugu baada ya kuachiwa huru alisema kuwa anachoshauri
ni Pinda kujitafakari upya juu ya kauli zake anazozitoa hasa
kuhamasisha watu kupigwa.
Awali, Sugu alikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa tuhuma kuwa
aliweka ujumbe mfupi katika mtandao wa kijamii ambao ulikuwa unamtusi
Waziri Mkuu Pinda.
Hata hivyo, alikuwa akipelekwa katika kituo cha polisi cha kati kwa
mahojiano na jana ilikuwa ni mara ya kwanza kufikishwa mahakamani.

Post a Comment