TFF yaibeza Yanga kususa sherehe za kukabidhi zawadi kwa washindi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema kuwa sherehe za
kukabidhi zawadi kwa washindi wa Ligi Kuu Tanzania Bara zitafanyika kama
zilivyopangwa hata kama Yanga hawatashiriki.
Sherehe hizo ambazo zimeandaliwa na wadhamini wa Ligi Kuu ya Vodacom zimepangwa kufanyika Julai 3 kwenye ukumbi wa Hoteli ya Double Tree Masaki.
Hata hivyo, Yanga imekuwa ikikaririwa mara kwa mara kupitia kwa msemaji wake, Baraka Kizuguto kuwa haishiriki sherehe hizo kwa kuwa Vodacom wamechelewa kutoa zawadi zao kwa kuwa Ligi imemalizika toka Mei 18 na zawadi kutolewa Julai.
Vodacom tayari walishatoa sababu za kuchelewa
kutoa zawadi hizo kuwa ni kutotaka kuingilia programu za timu ya Taifa
ambayo ilikuwa na kibarua cha michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali
za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco, hata hivyo Stars ilishatupwa nje ya
michuano hiyo baada ya kufungwa na Moroco.
Katibu mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema sherehe hizo zitafanyika hata Yanga hawatashiriki.
Osiah alisema: “Kama walikuwa na shida ya fedha
wangeandika barua wakaomba wapatiwe fedha zao mapema, mbona wakati
mwingine wanafanya hivyo.”
“Kwanza kwa kiongozi wa klabu kubwa kama Yanga kumzungumzia mdhamini wa Ligi vibaya ni aibu, hayo mambo ya malumbano na vurugu yalishapitwa na wakati, wanatakiwa wazungumzie mazuri.”
Wakati Osiah akisema hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi Wallace Karia alisema: “Yanga wakitaka kuja kwenye sherehe waje, wasipotaka waache, na wasipokuja zawadi hatuwapelekei.”
Yanga inastahili kupata kiasi cha Sh70 milioni baada ya kumaliza ligi ikiwa na kwanza na kutwaa ubingwa wa bara.

Post a Comment