ad

ad

Yanga kulinda heshima ya ubingwa leo.

WAKIWA tayari na uhakika, mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu 2012/13 Yanga, wanashuka katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam leo kuvaana na Coastal Union ya Tanga, ikiwa ni kati ya mechi nne za ligi hiyo zitakazopigwa kwenye viwanja tofauti.
 Yanga licha ya kuwa bingwa tayari, imedai itateremka katika dimba hilo kuibuka na pointi tatu muhimu ili kulinda heshima na hadhi yao kama vigogo vya soka hapa nchini na Afrika Mashariki na Kati.

Kiburi hicho cha Yanga kinatokana na maandalizi ya mwisho waliyoyafanya wiki hii katika gym ya Quality Center pamoja na mazoezi kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola, Mabibo jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Baraka Kiziguto, kikosi kizima kipo fiti kwa ajili ya mechi mbili zilizosalia na kudai kuwa, Salum Telela aliyekuwa anasumbuliwa na nyama za paja naye kajumuika na wenzake.

Katika hatua nyingine, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema mchezo huo namba 172 utachezeshwa na mwamuzi Simon Mberwa kutoka Pwani akisaidiwa na Said Mnonga na Charles Chambea wote wa Mtwara wakati mwamuzi wa mezani atakuwa Hashim Abdallah wa Dar es Salaam na Kamishna David Lugenge kutoka Iringa.

Wambura alisema viingilio katika mechi hiyo itakayoanza saa 10:15 jioni ni sh 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh 8,000 rangi ya chungwa, sh 15,000 kwa VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh 20,000.

Mechi nyingine itakuwa ni kati ya Mtibwa Sugar na African Lyon itakayochezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana wa Dodoma kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro.
Nayo Kagera Sugar iliyo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro huku Azam Complex Chamazi, maafande wa JKT Ruvu na Tanzania Prisons watapigishana kwata, wakati Ruvu Shooting itakuwa nyumbani kwenye uwanja wake Mabatini Mlandizi, Pwani kuwakabili ndugu zao Oljoro JKT ya Arusha.
Powered by Blogger.