ad

ad

Wanafunzi 200 Ileega hawajui kusoma.

WANAFUNZI 217 wa madarasa tofauti katika Shule ya Msingi Ileega, kata ya Mabira, wilaya ya Kyerwa, mkoani Kagera, wamebainika kutokujua kusoma na kuandika.


Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Renatus Kamanzi, aliwaeleza wajumbe wa kamati ya shule juzi kuwa sababu kubwa ya wanafunzi hao kutojua kusoma na kuandika ni utoro, uhaba wa walimu na baadhi ya wazazi kutokuwa na ushirikiano.

Alifafanua kuwa katika orodha hiyo, wanafunzi darasa la pili ni 63, la tatu 69, la nne 53, la tano 27, la sita 7 na darasa la saba ni wanafunzi wanane.
Alisema shule hiyo ina wanafunzi 866, walimu 10 na nyumba za walimu saba.

Alitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili shule hiyo kuwa ni uhaba wa walimu, vyumba vya madarasa, upungufu wa vitabu vya kiada na ziada, utoro na uchangiaji hafifu wa michango ya shule.

Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo, Cleophace Rugemalira, alisema kuwa kamati hiyo imejipanga kukutana na wadau wa elimu ili kuhakikisha wanakabiliana kikamilifu na changamoto hizo.

Alisema kuwa wazazi wanachangia ongezeko la utoro kwa wanafunzi ikiwemo kutochangia maendeleo ya shule na kwamba watachukuliwa hatua za kisheria.
Naye Afisa Elimu Shule za Msingi wilayani humu, Gideon Mwesiga, alisema kuwa ofisi yake inaendelea kudhibiti tatizo la utoro wa walimu na kuchukua hatua.
Powered by Blogger.