Zitto, Lissu, Mnyika walinusuru Bunge jana asubuhi ilisababisha Bunge kuahirishwa kwa muda kuiptisha bajeti ya Wizara ya Maji.
MIONGOZO mitatu iliyoombwa na wabunge, Zitto Kabwe, Tundu Lissu
na John Mnyika, jana asubuhi ilisababisha Bunge kuahirishwa kwa muda
kuiptisha bajeti ya Wizara ya Maji iliyowasilishwa bungeni wiki
iliyopita na Profesa Jumanne Maghembe.
Kizazaa hicho kilitokana na hatua ya Waziri wa Fedha na
Uchumi, William Mgimwa, kulitangazia Bunge kuwa ameongeza sh bilioni 184
kwenye bajeti hiyo ambayo awali ilikuwa sh bilioni 398 bila wabunge
kugawiwa nakala.
Hata hivyo, Spika wa Bunge Anna Makinda alilazimika kumtaka
Waziri Mgimwa kuja na nakala ya tamko la serikali kuhusu nyongeza hiyo
ya bajeti iliyofanyika na kuisambaza kwa wabunge.
Pia aliitaka Wizara ya Maji kuja na vitabu vinavyoonyesha
nyongeza ya mafungu ya miradi ya maji iliyoongezeka ili kutoa fursa kwa
wabunge wakati wa kupitia vifungu hivyo.
Wiki iliyopita bajeti hiyo ilikwama baada ya wabunge wengi
waliochangia mjadala wa hoja hiyo, kukataa kuiunga mkono kwa madai kuwa
kiasi cha fedha kilichotengwa na serikali, hakiwezi kuondoa tatizo la
maji nchini.
Kutokana na ufinyu huo, Spika Makinda aliagiza Kamati Ndogo ya
Bajeti, Wizara ya Fedha na
Wizara ya Maji, kukutana na kujadili namna
ya kupata fedha za nyongeza katika nakisi ya bajeti hiyo.
Zitto (Kigoma Kaskazini) alisema kanuni inawataka mawaziri wa
serikali kugawa nakala ya taarifa wanazozitoa bungeni ili wabunge waweze
kuibana serikali pale inaposhindwa kutimiza mipango yake.
“Mheshimiwa Spika, waziri alipotangaza kwamba wameongeza fedha
kwenye bajeti ya maji, ulimbana aseme wameongeza kiasi gani. Lakini
kibaya zaidi, waziri hakuwa hata na kikaratasi, tamko la serikali
linatolewa bila wabunge kupata nakala ya taarifa hiyo, jambo ambalo ni
kinyume kabisa na kanuni za Bunge.
“Hapa tuna hofu kwamba tunapigwa changa la macho maana hakuna
mahala ambapo serikali ‘inajikomiti’ na sisi tutashindwa kuibana,”
alisema.
Zitto alitolea mfano wa Wizara ya Uchukuzi kwamba mwaka jana
iliongezewa sh bilioni 94, lakini serikali hadi sasa imeshindwa kutoa
fedha hizo, hivyo aliomba mwongozo wa Spika kama Mgimwa alikuwa sahihi
au la.
Naye Lissu (Singida Mashariki), alitilia mkazo mwongozo wa
Spika kwa kumtaka waziri awasilishe taarifa kwa wabunge kwa mujibu wa
kanuni 49 (3).
Baadaye Mnyika (Ubungo), alitaka mwongozo kutaka Waziri wa
Maji, kuwa Prof. Maghembe wakati akitangaza miradi ya maji iliyofanyiwa
marekebisho kwa kuongeza fungu la bajeti, marekebisho hayo yaonekana
kwenye vitabu vya wabunge ili iwe rahisi kufuatilia.
Akitoa mwongozo wake, Makinda alisema tatizo la waziri kutoa
taarifa ya serikali na nakala kutosambazwa kwa wabunge, lilitokana na
waziri huyo kupewa taarifa jana asubuhi hivyo hakuweza kujiandaa.
Hata hivyo, alimuagiza Waziri Mgimwa kuja na nakala ya taarifa ya serikali kuhusu marekebisho hayo wakati wa jioni.
Kuhusu wizara kutofanya marekebisho ya nyongeza ya mafungu ya
fedha zilizoongezwa kwenye baadhi ya miradi ya maji nchini, Makinda
alisema hali hiyo inatokana na ugeni wa kutumia
Kamati ya Bajeti ambayo
imefanya kazi kubwa ya kusaidia kuainisha maeneo ya mafungu
yaliyoongezwa.
Baada ya mvutano wa hapa na pale katika baadhi ya vifungu, hatimaye bajeti hiyo ilipitishwa na wabunge.

Post a Comment