ad

ad

Umaarufu si tiketi ya uzinifu

KAMA ilivyo ada tumekutana tena kwenye kona yetu ya mahaba kukumbushana mawili matatu pia kwa wasiojua kabisa basi wajifunze kupitia hapa. Yangu hali mzima buheri wa afya njema, nina imani nanyi mu wazima.

Najua mna shauku ya kujua nini kimeandaliwa kwa siku ya leo, lakini nitakuwa mwizi wa fadhira kushindwa kutoa shukurani zangu kwa wasomaji wote waliotuma maoni yao katika kushauri, kupongeza na kukosoa nawashukuru sana kwa kuonyesha tupo pamoja.

Nina imani kichwa cha habari hapo juu kinajieleza kuhusu tabia zilizokosa muelekeo heshima hata picha mbaya mbele ya jamii kwa kila mtu anayepata umaarufu. Wapo wanao wadharau hata marafiki zao kisa ameonekana kwenye filamu au katika tamthilia runingani.

Kutokana na kuonekana kumekuwa kukiwajengea umaarufu mbele za watu hata kuonekana lulu mbele ya macho yaou, kwa majina yao kutajwa sana na au kuandikwa kwenye vyombo vya habari.

Kutokana na uwezo mdogo wa watu wenyewe ambao huenda kwao ni kama kipofu kuona bila kutegemea, hujikuta wakichanganyikiwa na kujua baada ya kuwa maarufu anatakiwa kufanya kitu gani hasa baada ya wao kuwa kioo cha jamii.

Lakini imekuwa tofauti kwa wasanii wetu ambao kila anayepata umaarufu, anakuwa na msululu wa wanaume au wanawake. Limekuwa jambo la kawaida kila siku wasanii kusikika yupo na huyu kesho na mwingine. Wengi huamini wanapendwa kwa vile unapokuwa mtu maarufu muda wa kutongoza unakuwa mdogo zaidi ya kutongozwa tena na watu wenye uwezo wao.

Kila kukicha kumekuwa na sifa mbaya za wasanii maarufu za uzinifu, kupiga picha chafu za ngono, kutembea na wake na waume za watu hata kuvunja ndoa za watu. Hii imekuwa ikiziweka pabaya tasnia zote za filamu, urembo na muziki, na kuonekana ni chombo cha uzinifu.

Kwa wasanii wa kike wamekuwa kama Kunguru wa Zanzibar kwa waume za watu, ukiangalia asilimia 75 ya wasanii wa kike wanatembea na wanaume za watu. Hii imekuwa ikiwanyima raha wanawake walioolewa na kujuta mtu kuwa maarufu ni hatari kwa ndoa zao.

Wasanii wamekuwa kina baba na mama huruma wasiojua kukataa kila anayekuja mwenye fedha au anayejirahisi kwao twende, kwa uchunguzi wangu mdogo ni wasanii wachache wanao jiheshimu na kuthamini utu wao na kufahamu ni nini cha kufanya na jamii itajifunza nini kupitia umaarufu wao.

Kumbuka kama wewe umekuwa maarufu na kila siku unabadili wanaume au wanawake kama nguo, unafiriki mzazi akielezwa mtoto wake anataka kuingia katika tasnia ya filamu atakubali?, ni wazi kwamba hatokubali. Kumbuka matendo yenu yatapunguza watu ambao nao wana ndoto ya kuwa wasanii wakubwa tena maarufu.

Mfano mdogo kila siku tunasikia kila atakayeulizwa husema kuwa hiki si umalaya lakini wote walio juu wanatabia chafu za kimalaya ambazo hazifurahishi masikoni kwa watu. Kila mrembo ana skendo chafu tena ‘Miss’ maarufu lazima awe na skendo chafu.

Nataka niliweke wazi hili, nina imani wengi wafanyao ni kutokana na ulimbukeni tu pengine wa sifa walizopata bila kutegemea na kujikuta wanashindwa kujiongoza mwenyewe kwa vile hawakutegemea kufika pale.
Na umaarufu siyo tiketi ya uzinifu kwa kuwa baba au mama huruma kwa kuutoa mwili wako sandakalawe. Mwili wako una thamani kubwa katika maisha yako pia tabia yako ndiyo CV ya maisha yako itakayokusaidia siku za mbeleni kukuweka sehemu nzuri.

Tumia umaarufu wako kuyajenga maisha yako kama kuingia mikataba na makampuni kuongeza bidii ili siku moja uvuke mipaka zaidi, siyo kugeuzwa jamvi la wageni. Na ukifika juu usijisahau na kujiona hakuna kama wewe, jiulize waliotangulia wapo wapi na kila kitu kina mwisho wake.

Wakati wako ukipita uwe umejitengenezea maisha yako na si kuwa na sifa ya kutembea na watu wengi au kuandikwa kwa tabia mbaya. Hivi unavyoandikwa vibaya mzazi wako anauweka wapi uso wake? Waoneeni huruma wazazi wenu, na umaarufu usikubadilishe na kuwa bingwa wa uzinifu.
Powered by Blogger.