Slaa: Hizi ndizo sababu za nchi kutotawalika • Lema aibuka, amtaka RC aache kumtumia vitisho.
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibrod Slaa amefafanua kauli yake, kwa kutaja sababu kadhaa ambazo
zitasababisha nchi isitawalike kama alivyowahi kuonya.
Mwaka juzi, Dk. Slaa alimtaka Rais Jakaya Kikwete kuwa makini na
kuchukua hatua za haraka kurejesha amani kabla Watanzania hawajaishiwa
uvumilivu na utawala wa serikali yake.
Hata hivyo, kauli hiyo ya kwamba nchi haitatawalika, kwa siku za
karibuni imekuwa ikipotoshwa na viongozi wa serikali na CCM wakidai kuwa
CHADEMA ilikuwa ikimaanisha kufanya vitendo vya fujo ili kuidhoofisha
Serikali ya Rais Kikwete.
Akihutubia mkutano wa hadhara jana mjini Njombe katika Jimbo la Njombe
Kusini linaloongozwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda uliofanyika kwenye
viwanja vya National Housing, Dk. Slaa alisema alichomaanisha ni
mtiririko wa matukio ya watu kunyanyaswa.
“Narudia tena hapa kuwa itafika mahali nchi hii haitatawalika na
itamshinda Kikwete. Yaliyojiri Rwanda na Burundi kuhusu ukabila wananchi
waliyapigia kelele mapema, lakini watawala wakapuuza, kilichofuata nchi
zikavurugika,” alisema.
Dk. Slaa ambaye aliambatana na baadhi ya wabunge wa chama hicho
waliokuwa wamesimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa siku tano,
alifafanua kuwa hatari hiyo ya amani kutoweka nchini aliiona mapema kama
kiongozi wa siasa, ndiyo maana akaonya.
“Tangu mapema manyanyaso ya wananchi hayasikilizwi, sakata la korosho
Lindi tuliliona kwenye ziara yetu mwaka jana, wabunge wetu wakalifikisha
bungeni lakini serikali ikapuuza, sasa wananchi wa Lindi na Mtwara
wameishiwa na uvumilivu, CCM wanadai ni CHADEMA,” alisema.
Katibu huyo alitumia fursa hiyo kuwapa pole wananchi wa Liwale kwa
vurugu zilizotokea juzi na kuharibu mali mbalimbali akisema kuwa
walipigwa mabomu wakidai haki zao.
“Adui wa Kikwete si CHADEMA, Slaa wala Mbowe kama CCM na serikali yao
wanavyopotosha, bali wajue kuwa adui ni manyanyaso wanayofanyiwa
wananchi, wamechoka na hilo ndilo nililoonya kuwa itafika mahali nchi
haitatawalika,” alisema.
Dk. Slaa mbele ya wabunge wake, Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini),
Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) na Ezekiel Wenje (Nyamagana) alisema kuwa
hata vurugu bungeni zinatokana na Bunge hilo kuongozwa kwa misingi ya
vyama badala ya kujali maslahi ya kitaifa.
Alisema kuwa wananchi wa kila kada wamechoka na maisha duni, hivyo
wanaishinikiza serikali yao iliyokuwa imekataa kuwasikiliza ichukue
hatua sasa.
“Walimu kutopewa mishahara yao, wanafunzi wanaendelea kufeli kwa
sababu walimu hawajaboreshewa mazingira ya kutoa elimu bora, watu
wachache kuendelea kunufaika na jasho la wengi, hayo yote yamesababisha
Watanzania kuishiwa uvumilivu.
“Na utawala wa serikali umedhihirisha kwa mara nyingine kuwa Kikwete
ameendelea kufumbia macho mambo hayo, nchi inazidi kukosa mwelekeo,”
alisema.
Dk. Slaa aliongeza kuwa aliposema nchi haitatawalika, alimaanisha
serikali itatue kero za wananchi, itekeleze wajibu wake badala ya
kufanya siasa kwenye matatizo.
“Serikali ingekuwa makini wangenisikiliza, mambo yanayotokea sasa
yasingetokea. Serikali imekuwa ikiishi kwa matukio, likitoka hili
linakuja jingine, likimalizika hili linaibuka jipya,” alisema.
Lema amuonya RC
Habari kutoka Arusha zinasema kuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless
Lema ambae ametangazwa kusakwa na Jeshi la Polisi mkoani humo, jana
alijitokeza na kutangaza mgogoro na Mkuu wa Mkoa Magesa Mulongo.
Lema alisema kuwa Mulongo amemtumia vitisho kupitia ujumbe wa maandishi kwenye simu (sms).
Akizungumza na waandishi wa habari katika mgahawa wa Ethiopia jijini
Arusha, Lema alisema amepokea ujumbe wa maandishi kutoka kwa Mulongo
ukisomeka; “umeruka kihunzi cha kwanza, nitakuonyesha kuwa mimi ni
serikali, ulikojificha nitakupata na nitakupa kesi ninayotaka mimi.”
Lema alionesha sms hiyo kwa waandishi wa habari, ikiwa imetumwa kutoka katika namba 0752 960276 ambayo alidai ni ya Mulungo.
“Nilimjibu kuwa nimekupata, nimekuelewa na nipo tayari. Na ujumbe huo
ulionesha kuwa ulipokelewa katika simu ya mkuu wa mkoa. Huo ni
mwendelezo wa vitisho vyake kwangu,” alisema.
Alisema kuwa hatambui chanzo halisi cha Mulongo kumtumia vitisho
hivyo, lakini akasema tayari ameishamjua vyema mkuu huyo wa mkoa na
kamwe hatamuogopa bali atatoa ushirikiano wowote kwake.
“Nimeshangaa kusikia kwenye vyombo vya habari jana kuwa mkuu wa mkoa
ameagiza nikamatwe kwa kuchochea vurugu katika Chuo cha Uhasibu wakati
mimi nilifika hapo kuzungumza na wanafunzi na kuwazuia wasiandamane.
“Mimi namshangaa sana huyu Mulongo, nilimpigia simu mimi kumuarifu na
kumuita kuzungumza na wanafunzi ili kutoa tamko la serikali na akaahidi
kufika baada ya dakika 10, lakini akafika baada ya saa moja,” alisema.
Mulongo alipoulizwa na mwandishi wetu kuhusu madai ya kumtumia Lema
ujumbe wa vitisho, alionesha kushangazwa na maelezo hayo lakini hakukiri
wala kukataa.
“Unaandikia chombo gani? Sasa huo ujumbe anaosema nimemtumia umeuona unatoka kwangu?” Alihoji.
Akizungumzia vitisho hivyo, Dk. Slaa alisema kuwa CHADEMA
wamekubaliana kumchukulia hatua za kisheria Mulongo kwa kumfungulia kesi
mahakamani.
Alisema vitisho hivyo ni hatari na pia ni kielelezo cha matumizi mabaya ya madaraka.

Post a Comment