ad

ad

Azam kuipa Yanga SC ubingwa wa Bara leo?.

INGAWA timu za soka za Azam na Coastal Union ya Tanga ndizo zinakumbana leo kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, matokeo ya mechi hiyo yanaweza kuipa Yanga ubingwa wa 24 tangu kuanza kwa ligi hiyo mwaka 1965.

Yanga inayoongoza ligi hiyo kwa pointi 56, inahitaji pointi moja tu katika mechi mbili zilizosalia kabla ya kufungwa kwa pazia la ligi hiyo iliyoanza Septemba 15, mwaka jana ikishindanisha timu 14.


Kwa vile uwezo wa Azam inayoifuatia kwenye msimamo wa ligi hiyo ni pointi 56 kama itashinda mechi zake zote tatu zilizobaki ikiwemo ya leo, sare tu katika mechi hiyo itatosha kuipa Yanga ubingwa bila kutoka jasho.

Hiyo ni kutokana na mazingira kuwa kama Azam itatoka sare au kufungwa, haitakuwa na ubavu wa kufikisha pointi 56 ambazo tayari zimefikiwa na Yanga chini ya Kocha wake Ernis Brandts huku ikisaliwa na mechi mbili dhidi ya Coastal Union na Simba.

Kama Azam itashinda katika mechi ya leo, Yanga italazimika kusubiri majaliwa ya ubingwa kutoka kwa Coastal Union ambapo matokeo ya sare tu yatatosha kuipa ubingwa.

Akizungumzia mechi ya leo, Stewart John Hall alisema jana kuwa kwa maandalizi waliyofanya na ubora wa nyota wake, hawana sababu ya kufungwa na kuwasihi wapenzi na mashabiki wao kujitokeza kwa wingi kuwashangilia.

Hall alisema licha ya soka kuwa na matokeo ya kufungwa, kushinda au sare, wao wamejiandaa kushinda kwani ingawa Yanga imebakisha pointi moja kutwaa ubingwa wa ligi hiyo uliotemwa na Simba, lakini katika soka lolote linaweza kutokea.

“Matokeo ya mechi ya kesho (leo) kila mtu anayapeleka kwa Yanga, lakini mimi na vijana wangu tutajitahidi kushinda ili kuzidi kujiongeza pointi hata kama hazitatosha kutupatia ubingwa, sio matokeo yetu yaipe Yanga ubingwa kabla ya kwisha kwa ligi,” alisema Hall.
Katika hatua nyingine mechi kati ya Ruvu Shooting na Simba iliyokuwa ichezwe jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, imesogezwa hadi Mei 5 kutokana na uwanja huo kwa jana kutumiwa kwa maandalizi ya sherehe za maadhimisho ya Mungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura wanawaomba radhi wapenzi na mashabiki wa soka kwa usumbufu uliojitokeza na kusema Jumapili ijayo Simba sasa watacheza na Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
“TFF inawaomba radhi mashabiki kwa usumbufu uliojitokeza kutokana na mabadiliko hayo ya ghafla,” alisema Wambura na kuongeza kuwa Simba watashuka dimbani Jumapili kucheza na Polisi Morogoro katika Uwanja wa Taifa.
Powered by Blogger.