Kupandisha nauli Dar kutaathiri maskini.
Tumesikitishwa mno na hatua ya Mamlaka ya
Udhibiti wa Safari za Majini na Nchikavu (Sumatra), kupandisha nauli za
daladala, mabasi ya kwenda mikoani, usafiri wa reli na tozo za majini
kuanzia Aprili 12. Hatua hiyo, kwa mujibu wa Sumatra imetokana na maombi
mbalimbali ya wadau katika sekta ya usafirishaji kwamba gharama za
uendeshaji wa vyombo hivyo zimepanda mno.

Akitangaza nauli hizo mpya jijini Dar es Salaam juzi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Ahmad Kilima alisema nauli za daladala zitaongezeka kwa asilimia 24.46 kulingana na umbali, hivyo kupanda kati ya Sh400 na Sh750 kwa safari. Wanafunzi watalipa Sh200 kwa njia zote jijini Dar es Salaam.
Tungetaka ieleweke hapa kwamba kusikitishwa kwetu na kupanda kwa nauli hakuna maana kwamba tunaelekeza lawama kwa Sumatra pekee. Ni kweli Sumatra ina udhaifu wake, lakini katika hili tunadhani Serikali ndiyo inayopaswa kubeba lawama kwa kusababisha kupanda kwa gharama za usafirishaji kwa kuweka kodi nyingi zisizokuwa na vichwa wala miguu.
Serikali kila mwaka inapandisha kodi za mafuta, bima za magari, leseni za barabara, leseni za udereva, kodi za ukaguzi na kodi za vipuri. Umiliki wa chombo cha usafiri sasa umekuwa wa gharama kubwa na ndiyo maana tunasema Sumatra haina jinsi isipokuwa kuwanusuru watoa huduma za usafirishaji na gharama hizo kubwa kwa kupandisha viwango vya nauli kila inapobidi.
Pamoja na kwamba nauli pia zitapanda kwa mabasi yaendayo mikoani, usafiri wa reli na majini, sisi tunadhani madhara makubwa ya hatua hiyo yatawakumba kwa kiasi kikubwa abiria wa daladala zinazotoa huduma katika miji yote hapa nchini, hasa jijini Dar es Salaam ambako maelfu kwa maelfu ya abiria wenye kipato kidogo wanategemea usafiri huo katika shughuli zao za kila siku.
Kutokana na ukubwa wa Jiji la Dar es Salaam lenye wakazi wapatao milioni tano katika wilaya tatu za Kinondoni, Temeke na Ilala, abiria wanalazimika kupanda mabasi matatu au manne kwenda na kurudi kwenye shughuli zao za kila siku.
Kutoka sehemu moja kwenda nyingine imekuwa siyo tu karaha kubwa, bali inachukua muda mrefu kutokana na misururu ya magari inayosababishwa na miundombinu mibovu.
Serikali sasa italazimika kujipanga vizuri ili kukabiliana na hali hiyo. Lazima itambue kwamba kupandisha nauli mara kwa mara siyo suluhisho la kudumu na kwamba mkakati mbadala ni kuwekeza katika usafiri wa reli vijijini na mijini.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe juzi alionyesha kufahamu suluhisho la tatizo hilo aliposema Serikali itaanzisha treni maalumu jijini Dar es Salaam zitakazohudumiwa na kuendeshwa kirahisi kwa kutumia njia zilizopo na kuunganishwa na vituo vikuu vya mabasi yaendayo mikoani vya Boko (Tegeta), Luguruni (Mbezi) na Mbagala Rangitatu.
Mapendekezo kwamba Serikali ipandishe kima cha chini cha mishahara ni upuuzi, kwani siyo wakazi wote mijini ni waajiriwa wa Serikali. Hatua hiyo ikichukuliwa itasababisha mfumuko wa bei usiokwisha, kwani bidhaa zote muhimu zitapanda. Wakati huohuo, wakazi wa mijini lazima waepuke safari zisizo za lazima na wawe tayari kutembea kwa miguu kwa sababu hali ya usafiri huko tuendako haitabiriki.
Post a Comment