Rufaa zote zatupwa TFF..Malinzi, Nyamlani, Manji, Wambura wapeta
KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jana
ilitoa matokeo ya pingamizi zilizowasilishwa dhidi ya wagombea kwenye
Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho hilo na Bodi ya Ligi Kuu huku wagombea wote
waliopingwa wakipeta.
Ikitumia kanuni za uchaguzi ibara ya 11(4), kamati hiyo iliyokutana Januari 30 ilipitia pingamizi
hizo zilizowasilishwa kwao na wadau mbalimbali wa soka ambapo siku hiyo walitakiwa kuzitetea
hoja zao kwa vielelezo kama ilivyokuwa kwa watuhumiwa.
Jamal Malinzi aliyekuwa akipingwa na Agape Fue kuwania nafasi ya urais
kwa madai ya kuvunja katiba kwa kufanya juhudi za kukwamisha juhudi za
shirikisho hilo kuitaka mikoa kuridhia mabadiliko ya katiba kwa waraka
kutekeleza agizo la Shirikisho la Soka Afrika (Caf) na Kimataifa (Fifa),
ameshinda.
Fue pia alidai Malinzi hana sifa ya uzoefu wa miaka mitano katika uongozi wa soka, pia amekosa.
Pingamizi kuhusu uadilifu na haiba ya kuliwakilisha shirikisho hilo
kimataifa, zote hizo mbili zimetupiliwa mbali kutokana na mpingaji
kushindwa kutokea kuthibitisha madai yake.
Kwa mujibu wa taarifa ya shirikisho hilo iliyosainiwa na Katibu Mkuu
wake, Angetile Osiah, mgombea mwingine wa nafasi hiyo Athuman Nyamlani
aliyekuwa akipingwa na watu wawili: Mintanga Yusuph Gacha na Medard
Justinian, pia ameshinda tuhuma dhidi yake.
Tuhuma zilizokuwa zikimkabili Nyamlani ni kwamba kwa vile ni Hakimu
Mkazi wa Mahakama ya Tanzania, hivyo anakosa kigezo na sifa ya kugombea
nafasi hiyo kwa mujibu wa Judicial Service Act, Public Service Act 2002
na Code of Conduct for Judicial Officers of Tanzania.
Hoja nyingine za kumpinga Nyamlani ni kuwa akiwa rais wa TFF kutakuwa
na mgoganao wa kimaslahi pia alikosa umakini na uadilifu kwa kushindwa
kutimiza vema wajibu wake hadi akaunti ya shirikisho hilo kufungiwa na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Vilevile kamati hiyo imetupa pingamizi dhidi ya Michael Wambura
aliyekuwa akipingwa kuwania nafasi ya Makamu wa Rais wa Shirikisho hilo
na wadau Saidi Rubea na Josea Samuel Msengi kwa tuhuma mbalimbali.
Wakati Msengi akiondoa pingamizi lake, tuhuma za Rubea hazikukidhi matakwa ya Kanuni za
Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(2), hivyo anabaki kupambana na Nasib Ramadhan na Wallace Karia.
Kamati ya Uchaguzi imetupilia mbali tuhuma hizo baada ya Mintanga
Yusuph Gacha kushindwa kutokea kutetea pingamizi huku Medard Justinian
akishindwa kuithibitishia kamati kuwa alikuwa na ufahamu wa kutosha wa
pingamizi lake ikiwemo viambatanisho vyake, hali iliyoonyesha kuwa
pingamizi lilikuwa la hila na udanganyifu.
Kwa upande wa wagombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji waliokuwa
wakipingwa, Athuman Kambi,
Eliud Mvela, Epaphra Swai, Vedastus Lufano na Mugisha Galibona, pia
zote zimetupiliwa mbali kwa kukosa nguvu kwa mujibu wa kanuni za
uchaguzi.
Aidha kamati hiyo imetupa pingamizi dhidi ya Yusuf Manji anayewania
nafasi ya uenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu iliyokuwa imewekwa na wadau
Daniel Kamna na Juma Magoma, kwamba hana uzoefu wa miaka mitano, pia
hajawahi kucheza soka au kuwa kocha, mwamuzi au kushiriki uendeshaji
ngazi ya mkoa au Ligi Daraja la Kwanza.
Kamati hiyo imetupa pia pingamizi dhidi ya Saidi Muhamed anayeomba
nafasi ya Makamu wa Bodi ya Ligi iliyowekwa na Frank Mchaki kwamba si
Mwenyekiti wa Azam, hivyo anakosa sifa, pia ameandika maelezo ya uongo
kwenye fomu.
Madai hayo yametupwa kwa kutokidhi matakwa Kanuni za Uchaguzi za TFF
Ibara ya 11(2) kwani haikuambatanishwa na vielelezo kuthibitisha
maelezo ya pingamizi.
Pingamizi nyingine iliyotupwa ni dhidi ya Hamad Yahya Juma anayeomba
kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, aliyekuwa akipingwa na
Mchaki kwamba si Mwenyekiti wa Klabu ya Mtibwa, hivyo hana sifa.
Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho hilo umepangwa kufanyika Februari 24,
ukitanguliwa na ule wa Bodi ya Ligi Kuu utakaofanyika Februari 22.

Post a Comment