Jela miaka 28 kwa kuchoma nyumba
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Sumbawanga imemhukumu kifungo
cha miaka 28 jela kila mmoja wa wakazi wanane wa kijiji cha Lusaka
baada ya kupatikana na kosa la kuchoma moto nyumba za baadhi ya wakazi
wa kijiji hicho kwa tuhuma za imani ya kishirikina.
Hukumu hiyo ilitolewa na hakimu wa mahakama hiyo, Manase Goroba, baada
ya kuridhishwa na maelezo ya upande wa mashtaka kuwa watu hao walitenda
kosa hilo.
Katika maelezo ya awali ya mwendesha mashtaka wa Jeshi la Polisi,
Mkaguzi Msaidizi Emmanuel Shani, aliieleza mahakama hiyo kuwa mnamo Mei
13 washtakiwa hao nyakati za usiku walijikusanya na kwenda kubomoa
nyumba ya wakazi wenzao wa kijiji hicho kutokana na tuhuma za uchawi
ikiwa ni kinyume cha sheria.
Shani alisema katika tukio hilo licha ya kubomoa nyumba hizo pia
walimjeruhi Vestina Mwananzumi (29) kwa kumkata na panga mguuni kisha
kudaiwa kumuua Michael George (68).
Waliokumbwa na adhabu hiyo ya kifungo ni pamoja na Oden Msongela
(40), Filberth Abel maarufu kama Majaliwa (40), Gilbert Mwanandenje
(43), Sabas Alfred (18), Edwin Masimba (30), Michael Simfukwe (33),
Marres Namazari (28) na Wenslaus Kankwale (30).
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Goloba alisema kuwa alitoa adhabu hiyo ili
iwe fundisho kwa watu wengine kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo na
hata mauaji ndani ya mkoa huo vinavyosababishwa na tuhuma za imani ya
kishirikina.
Licha ya adhabu hiyo bado watu hao wanakabiliwa na kesi nyingine ya
tuhuma ya mauaji ya Michael George ambaye aliuawa katika tukio hilo.

Post a Comment