Ahadi zawa mwiba kwa JK
AHADI za ujenzi wa barabara za lami zilizopata kutolewa na Rais
Jakaya Kikwete wakati akiomba kura mwaka 2010, zimezua balaa na kuibua
mzozo bungeni.
Hali hiyo ilitokana na swali la Mbunge wa Buhambwe, Felix Mkosamali
(NCCR- Mageuzi), kuhoji utekelezaji wa ahadi ya Rais Kikwete ya kujenga
barabara ya Nyakanazi-Kibondo-Kigoma katika kiwango cha lami.
Pia alihoji ahadi ya Rais Kikwete ya ujenzi wa barabara ya Kibondo
Mjini yenye urefu wa kilomita 1.5 na ujenzi wa barabara ya kimataifa ya
kutoka Kibondo –Mabamba mpaka wa Burundi.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge alisema
serikali bado iko mbioni kutekeleza ahadi hizo kutegemea na upatikanaji
wa fedha.
Alisema ahadi za rais zitatekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha kwani mwisho wa ahadi zake ni mwaka 2015.
Kutokana na majibu hayo, Mkosamali aliuliza swali la nyongeza na
kutumia maneno yaliyotafsiriwa kama ni kashfa kwa Rais Kikwete.
“Mhesmiwa Naibu Spika, sikubaliani na majibu mepesi ya Mheshimiwa
Naibu Waziri. Hivi unataka kusema ahadi za Rais Kikwete kujenga barabara
ya Kibondo ilikuwa ya uongo? Ina maana alisema uongo ili kupata sifa ya
kuchaguliwa kuwa rais?”
Swali hilo la nyongeza ambalo hata hivyo lilijibiwa vizuri na Naibu
Waziri wa Ujenzi, lilimkera Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi ambaye alisimama na kuomba mwongozo wa
spika akipinga lugha iliyotumiwa na Mkosamali dhidi ya Rais Kikwete.
“Mheshimiwa Naibu Spika, mbunge aliyeuliza swali la msingi kuhusu
ahadi za rais, wakati akiuliza swali la nyongeza, alitumia maneno makali
dhidi ya rais kinyume cha kanuni za Bunge.
“Anasema rais alisema uongo au alisema uongo ili achaguliwe, sio maneno ya kistaarabu kutumika hasa kwa rais.
“Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni ya 61 (2) inasema mbunge hatatumia
kumdhihaki rais au kulishawishi Bunge kuamua jambo fulani dhidi ya rais.
“Nimesimama sio kutaka aombe radhi, bali kuwakumbusha vijana wawe
makini na matumizi ya lugha, hasa lugha ya kuudhi. Mwongozo wangu ni
kutaka uwakumbushe wabunge matumizi mazuri ya lugha, ni hilo tu,”
alisema na kuketi.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) ambaye ni mnadhimu
kambi ya upinzani bungeni, kwanza alimtaka Waziri Lukuvi afute kauli
yake kwamba kuna vijana kwa madai kuwa ndani ya Bunge hakuna vijana.
”Pili, Waziri Lukuvi amemwelewa vibaya mbunge maana hajasema rais
muongo. Alitaka kujua kama ahadi ya rais ni ya uongo. Na tatu mbunge
hakutaka kushawishi Bunge kuchukua hatua dhidi ya rais,” alisema Lissu.
David Kafulila, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi), naye alisimama
na kuongeza kuwa waziri amepotosha umma na huo ni uchochezi.
Mkosamali naye alisimama na kusema kuwa hajamtukana rais bali alitaka kujua kama ahadi hiyo ni ya uongo au la.
Akitoa mwongozo wake, Naibu Spika aliwataka wabunge kutumia lugha ya kistaarabu.
Mbali ya swali la Mkosamali, wabunge wengine waliohoji ahadi ya ujenzi
wa barabara katika maeneo yao ni Ester Bulaya (Viti Maalumu), Paul
Rwanji (Manyoni Magharibi), wote CCM na Said Arfi wa Mpanda Kati
(CHADEMA), ambao nao waliohoji ahadi za Rais Kikwete za ujenzi wa
barabara katika maeneo yao.

Post a Comment