ad

ad

Mume Alivyowaua Mkewe n Kichanga Chake kwa Jembe


KATIKA eneo la Matosa Darajani, Goba wilaya ya Kinodnini jijini Dar es Salaam wakati mama, kichanga chake cha umri wa miezi minne na mdogo wake wa kike walipouawa kwa jembe huku mtuhumiwa namba moja akitajwa kuwa ni mume wa mwanamke huyo.

Tukio hilo lililovuta hisia za wengi, linadaiwa kuwa chanzo chake ni wivu wa kimapenzi, huku ikielezwa zaidi kuwa mume alichukua hatua hiyo mara tu baada ya kurejea nyumbani kwake akitokea safarini mkoani Mbeya na kumkuta mkewe na kichanga hicho alichoamini kuwa si mali yake bali mwanaume mwingine aliyekuwa na uhusiano naye haramu wa kimapenzi.

Kwamba, kama ilivyo katika simulizi za hadithi ya wimbo wa bongofleva uitwao Bushoke, unaoelezea namna mume alivyokuwa akihisi kurubuniwa na mkewe na kujikuta akilea watoto wasiokuwa wa damu yake, ndivyo pia hisia kali za wivu kwa mtuhumiwa zinavyodaiwa kusababisha maafa hayo yaliyowaacha wapendwa wa marehemu wakiwa katika majonzi makubwa.

Taarifa za Kipolisi, zinamtaja mtuhumiwa kuwa ni Mhasibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Ami Lukule, anayedaiwa kufanikisha mauaji hayo kwa kutumia jembe kumuua mkewe aitwaye Pendo Likule, kichanga chake kiitwacho Joshua na shemejiye wa kike, Magreth Samwel.

Inaelezwa kuwa baada ya kufanya mauaji hayo, mtuhumiwa aliifungia miili ndani ya nyumba yao hiyo na kukimbilia kusikojulikana.

Akizungumzia zaidi kuhusu tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Benedict Kitalika alisema tayari jeshi lake limeanza msako mkali dhidi ya mtuhumiwa, ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kupatiwa taarifa hizo juzi.

“Taarifa nimepata jana (Alhamisi), majira ya asubuhi. Ni kwamba kuna kijana anayesoma Mbeya alikuja kumtembelea ndugu yake. Kufika pale nyumbani, akakuta hali siyo ile ambayo ameizoea hasa kwa kuona kuna ukimya fulani,” alisema wakati akielezea namna mauaji hayo yalivyofahamika.
Mke aliyeuawa (kushoto).

Akieleza zaidi, Kamanda Kitalika alisema kuwa baada ya kijana huyo kuona kumejaa ukimya, alitoa taarifa kwa majirani na polisi na baada ya hapo, ndipo polisi walipofika na kuvunja mlango na kukuta maiti hizo.

“Huyo Ami aliacha message (ujumbe) kuwa polisi wasihangaike ni yeye amefanya hicho kitendo kutokana na kwamba mke wake siyo mwaminifu. Alikuwa anamtuhumu mke wake kuwa mtoto wake aliyemuua siyo wake… na kwamba amezaa na watu wengine,”

Alisema kuwa mtuhumiwa anadhaniwa kutekeleza mauaji hayo kwa kutumia jembe kwa sababu walilikuta eneo hilo likiwa limetapakaa damu .

“Tumehisi mtuhumiwa alitumia jembe kuwaua maana tumekuta jembe limejaa damu na maiti tumekuta zimeumia sehemu mbalimbali za kichwa na kwenye shingo … na kwa mtoto kaumizwa sehemu za tumbo,” alisema.

Akieleza zaidi, alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na uchunguzi kamili utafanywa na madaktari kabla maiti kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.
Ami Lukule anayedaiwa kutekeleza tukio hilo.


MAJIRANI WANENA
Baadhi ya majirani walielezea msikitiko yao kuhusiana na mkasa huo, huku baadhi wakidai kuwa tukio hilo lilitokea baada ya mtuhumiwa kutoka safarini mkoani Mbeya na kukuta mtoto huyo aliyekuwa akiamini kuwa si wake.

Hata hivyo, hakukuwa na taarifa rasmi za kuthibitisha madai kwamba mtuhumiwa alitenda unyama huo mara tu baada ya kurejea kwake akitokea safarini. 

 “Kama ni tuhuma za mkewe kukosa uaminifu, ni heri basi hata angemuacha huyo kichanga na shemeji yake ambao hawana hatia… inasikitisha sana,” alisema mmoja wa majirani.

Jirani mwingine aitwaye Asha John, alisema kuwa hakuna mtu ambaye anajua muda ambao ulifanyika kwa mauaji hayo na kwamba taarifa walizipata baada ya ndugu yao kufika katika nyumba hiyo na kushtushwa na ukimya uliokuwapo.

“Hakuna anayejua muda ambao mauaji yalifanyika maana hatujasikia kelele zozote. Lakini nahisi tukio hilo limefanyika ule muda ambao mvua ilikuwa ikinyesha sana…ile iliyochanganya kuanzia saa moja hadi saa 4:00 usiku, siku ya Jumatano,” alisema Asha.

Akieleza zaidi, alisema kuwa jana majira ya asubuhi,  alifuatwa na ndugu wa marehemu na kumpatia taarifa kuwa mazingira aliyoyaona yapo tofauti na kumjulisha kuwa anakwenda kutoa taarifa polisi.

Alisema kuwa wakati kijana huyo akielekea kutoa taarifa polisi, yeye alikwenda kuwajulisha viongozi wa serikali ya mtaa kwa ajili ya kufika katika nyumba hiyo na kujua kile ambacho kinaendelea.

“Huyu kijana kilichomfanya afike nyumbani hapo kumuangalia ndugu yake ni kwamba (mtuhumiwa) alimpigia simu mkwe wake majira ya saa 8:00 usiku bila kuzungumza chochote… na asubuhi ilipopigwa simu ya mkewe, ilikuwa ikiita bila kupokelewa na ndipo alipotumwa kijana huyo kuja kuwaangalia kuna nini,” alisema Asha.

Aliongezea kuwa:”Hata kijana huyo alipofika hapa nyumbani alikuwa akipiga simu inaita haipokelewi,  akiangalia milango imefungwa, alivyochungulia kwenye dirisha akaona mtu kama kalala… lakini alishangaa kuona ukimya ambao hajauzoea, ndipo ikabidi aje kutoa taarifa na baadaye kwenda polisi,” aliongeza Asha.

 “Sisi kama majirani kwa kweli tukio hili tumetuumiza sana… na limetusikitisha maana ni kitendo cha kinyama, halafu huyu mwanamke alikuwa anatafuta mtoto muda mrefu… alikuwa anahangaika hospitali, mara aende kwa walokole, yaani kajifungua hivi karibuni na hata mshono wake haujapona,” alidai Asha.

CREDIT: NIPSAHE

No comments

Powered by Blogger.