I Miss My God! (Namkumbuka Mungu Wangu) -02
Msichana mrembo, Jackline Manyilizu anajifungua mtoto mrembo, mwenye mchanganyiko wa Kiafrika na Kizungu. Ni mtoto mzuri aliyeitwa Theresia, muonekano wake unamfanya kila mtu kujiuliza maswali mengi, hakuna anayejua ni mwanaume gani aliyezaa na Jackline mtoto mrembo kama huyo.
Theresia anakua, uzuri wake unamchanganya kila mtu aliyekuwa akimwangalia. Ukiachana na urembo wake huo, msichana huyo amebarikiwa kuwa na akili nyingi mno. Anaongoza darasani tangu chekechea mpaka kidato cha nne.
Baada ya kumaliza kidato cha nne na kuongoza Tanzania nzima, kumi bora wanaitwa ikulu na kupata chakula na rais. Huko, Theresia anakutana na kijana aliyeitwa Joshua. Wanazungumza mengi, Theresia anamwambia Joshua kwamba ndoto zake hapo baadaye ni kuwa mtawa kitu kinachomfanya kijana huyo kushtuka, inakuwaje msichana mrembo kama yeye awe mtawa?
SONGA NAYO...
JOSHUA alimwangalia Theresia kwa mshangao, macho na akili yake yalikuwa hayawasilishi kitu cha kufanana, hapakuwa na uwezekano kabisa wa msichana mrembo kiasi hicho awe mtawa.
Msichana mrembo kama alivyokuwa Theresia, hakutakiwa kuwa mtawa, alitakiwa kuwa na kazi fulani nzuri ambayo ingemfanya kuchanganyika na wanaume au hata kuwa mwanamitindo mkubwa hapo baadaye kama alivyokuwa Naomi Campbell.
“It doesn’t make sense!” alijikuta ametamka maneno hayo kwa sauti akitikisa kichwa chake.
“It makes a lot of sense!”(Ina maana kubwa sana)
“For the first time the church is going to have the most beautiful woman in the history of man!”(kwa mara ya kwanza kanisa litakuwa na mwanamke mrembo kuliko wote katika historia ya mwanadamu!)
“Really?”(hakika?)
“Yeah!”(ndiyo!)
“And who is that woman?”(na huyo ni nani?)
“Theresia!”
“Wow! That’s will be God’s Glory, huh!”(huo utakuwa ni Utukufu wa Mungu! Au siyo?)
“Stop kidding Theresia, you can not betray your country which needs brains to solve its challenges and go become a nun, that’s betraya!”(acha utani Theresia, huwezi kuisaliti nchi yako inayohitaji watu wenye akili kutatua matatizo halafu uende kuwa Mtawa, huo ni usaliti!)
“Joshua please mind your own business, this is life, it is for me to choose!”(Joshua tafadhali fuatilia mambo yako, haya ni maisha, mimi ndiye wa kuchagua!)
Mama yake Theresia alikuwa kando akiwasikiliza kwa makini, yeye peke yake kwenye mkusanyiko huo ndani ya ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye alikuwa amevalia nguo za bei rahisi, mwili wake ukitetemeka kwa hofu.
“Forgive me!”(nisamehe!) alisema Joshua na Theresia akatikisa kichwa chake juu kuonyesha kwamba amemsamehe “Is this your mom?” Joshua akaongeza swali jingine akitaka kufahamu kama mwanamke aliyekuwa hapo ni mama yake.
“Yes!”(ndiyo)
Joshua alimsogelea mama yake Theresia na kuanza kuongea naye juu ya kumshauri mwanaye afikirie vizuri uamuzi wake wa kuwa mtawa, mama akamwita Theresia karibu yao, wote wawili wakaanza kumshambulia kwa ushauri lakini hakuwa tayari kusikiliza.
“Mbona unalia mwanangu? Ni furaha tu au?’
“Ni furaha mama!”
“Ukienda shule jitahidi sana, una nafasi kubwa ya kuwa kiongozi hapo baadaye, unaweza hata kuwa kuja kuikalia hii ofisi siku moja, binadamu wachache sana wana akili kama zako, ukikwama chochote nitafute nitakusaidia mpaka utimize ndoto zako, kumbuka mwanangu ni zamu ya wanawake kushika usukani wa taifa letu, hu!hu!hu!” alimaliza waziri Mtaturu kwa kicheko lakini alishangaa kumuona Theresia wala hashtuki.
“Na wewe ongea naye mheshimiwa waziri!” Joshua alisema na kumfanya waziri ahisi kulikuwa na kitu.
“Kwani unataka kuwa nani? Kama wasiwasi wako ni fedha ya kusoma, serikali itakusomesha.”
“Mimi?”
“Ndiyo.”
“Nataka kuwa mtawa.”
“Mtawa? Hebu sema tena, unamaanisha mtawa wa kanisani au mtawa ina maana nyingine tena? Ni cheo fulani?”
“Mtawa kanisani.”
“Wewe mtoto! Hebu usiniudhi…”
“Nahisi wito moyoni mwangu, ndicho kitu pekee ambacho Mungu anataka nifanye maishani mwangu.”
“Huyo siyo Mungu, labda wa herufi ndogo…”
“Nimeshaongea naye sana lakini hasikii,” mama yake akajazia.
Hakuna ushauri uliofanikiwa kumbadilisha Theresia, alishafikia uamuzi huo tangu akiwa na miaka kumi, muda wote akisoma shule ya awali kanisani, rafiki yake mkubwa alikuwa ni sista Clara Davidson, raia wa Marekani aliyekuja nchini kujitolea akiwa chini ya shirika la watawa waitwao Wa-Fransisca ama kwa Kiingereza Franciscan Sisters of Mary ambao makao yake makuu yalikuwa Columbus, Marekani.
Mtawa huyu alimpenda Theresia, ndiye aliyemfundisha kuongea Kiingereza cha Kimarekani, alimweleza mengi kuhusu maisha ya utawa, historia za wanawake ambao waliyatoa maisha yao kwa Mungu, wakaishi kama watawa mpaka kifo chao na hatimaye kuwa watakatifu, akimtajia mfano wa Mtawa wa Kanisa Katoliki, Mother Theresa wa Calcutta.
“Mpendwa Theresia, maisha hayana maana yoyote hata kama ungekuwa na kila kitu, mwisho ni kifo, cha muhimu ni baada ya kufa utakwenda wapi mwanangu, lazima twende Mbinguni, huko ndiko tutaishi maisha mazuri, tiketi ya kwenda mbinguni ni matendo yetu, tujitoe kwa Mungu kama walivyojitoa wanawake wenzetu huko nyuma, wakayatoa maisha yao sadaka na leo hii ni watakatifu, Theresia nitafurahi sana nikikutana na wewe Mbinguni siku moja…”
Maneno haya ya sista Clara aliyoambiwa Theresia akiwa mtoto mdogo yalizama na kuweka mizizi akilini mwake, kwake mwanamke wa mfano akawa Sista Clara, aliporejea kwao Marekani ambako baadaye alikufa kwa ugonjwa wa saratani, Theresia akiwa na umri wa miaka kumi, darasa la nne, ndipo alikata shauri la kuwa mtawa ili siku akifa aende Mbinguni kukutana na Sista Clara.
Hakuna siku hata moja iliyopita bila maneno haya kusikika moyoni mwa Theresia, hakuwahi kumshirikisha mama yake, lakini aliwahi kwenda Parokiani wakati wa likizo na kumwambia Mkuu wa Watawa wa wakati huo Sista Adventina Kimaro juu ya nia yake ya kuwa Mtawa baada ya kumaliza kidato cha sita.
“Kweli umeamua kuwa mtawa mwanangu?”
“Ndiyo sista.”
“Basi wakati wa likizo uwe unakuja kuishi nasi hapa ili uanze kujifunza kuishi kitawa kabla!”
“Sawa Sista.”
Wakati wa likizo zote Theresia aliishi parokiani, lakini hata siku moja hakuwahi kufungua mdomo wake kumweleza mama yake juu ya nia ya kuwa mtawa, alipomaliza kidato cha nne ndipo alifungua mdomo wake na kuweka kila kitu wazi, mama yake alipinga kabisa, kwa sababu yeye ndiye mtoto pekee aliyekuwa naye.
***
Shule zilipofunguliwa Theresia alirejea tena shule ile ile ya Mtakatifu Columbus kwa kidato cha tano na cha sita, mama yake aliamini katika miaka ile miwili angeweza kubadili msimamo, jambo ambalo hakulifahamu ni kwamba mtoto wake alianza kuzama mitandaoni kusoma kwa undani mambo ya utawa na hata kuanza kuchagua mashirika ya kuyatumikia.
Ni huko mitandaoni ndiko alikokuta na Shirika la Watawa lililoitwa Martinaclaran Sisters, ambalo kazi yake kubwa ilikuwa ni kuuombea Ulimwengu, lilianzishwa na watawa wawili Martina Deogratius na Clara Matthews mwaka 1702, waliozaliwa katika familia tajiri lakini wakaamua kuuacha utajiri wa wazazi wao na kumkabidhi Mungu maisha, wakawa waombaji wa usiku na mchana mpaka walipokufa.
Mnyororo wa maombi uliendelea, wasichana wengi wakiacha maisha ya kifahari na kujiunga na shirika hilo la kuombea ulimwengu na watu wenye dhiki. Mtu yeyote aliyejiunga na shirika hili alitakiwa kufanya maombi saa ishirini na nne, hakutakiwa kuonana au kukutana na wanadamu, kifupi kwa ndugu zake ilikuwa ni kama amefariki dunia kwani wasingemwona mpaka mwisho wa uhai wake.
“I want to be a Martinaclaran”(Nataka kuwa Mtawa wa shirika la Martinaclara) Theresia alijisemea moyoni mwake baada ya kufikia uamuzi huo.
Akaendelea na masomo yake ya kidato cha tano na sita mpaka kumaliza, majibu ya mtihani yalipotoka, kama kawaida yake alikuwa ameshika namba moja Tanzania nzima akiwa na pointi 1.3 huku akiwa amefaulu masomo yote matatu kwa kupata alama 100 kitu kilichoishangaza mno Tanzania. Yeye na mama yake wakakaribishwa tena Ikulu ambako alikabidhiwa zawadi na kukutana tena na Waziri wa elimu Mheshimiwa Mtaturu.
“Hongera mwanangu, bado unataka kuwa mtawa?”
“Ndiyo mama, tena sana!”
“Mh!”
Je, nini kitaendelea katika maisha ya Theresia? Joshua James yuko wapi? Fuatilia wiki ijayo siku ya Jumapili.
Post a Comment