Usilie Kwa Nini Huolewi, Jiulize Wanaoolewa Wakoje?
LICHA ya kwamba makubaliano ya ndoa hufikiwa na watu wawili, mwanaume na mwanamke lakini ni ukweli usiopingika kuwa mwanaume ana nafasi kubwa ya kuubeba uhusiano ufike kwenye hatua ya ndoa. Mwanaume anaubebaje uhusiano? Nitafafanua! Katika mila na desturi za Kitanzania, mara nyingi mwanaume ndiye anayemuanza mwanamke. Anamuona, anavutiwa naye, anamueleza na ndipo baadaye mwanamke naye anakuja kujibu mapigo ya upendo. Wapo pia wanawake wanaoanza kuvutiwa na wanaume kisha kuanza kuwaeleza lakini ukweli utabaki palepale, mwanaume ndiye atakayefanya taratibu za ndoa.
Hata kama mahari atatoa mwanamke, kiutaratibu, mwanaume ndiye atakayemtolea mahari mwanamke na huo ndio mpango wa Mungu. Mwanaume (Adam) aliumbwa kwanza, mwanamke (Hawa) akafuatia. Ushahidi wa Biblia kwa
Wakristo huu hapa: “Bwana Mungu akasema, si vyema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.”-Mwanzo 2:18, 21-24. Ongezea na hii kutoka kwa Mtume Muhammad kwa Waislam: “Enyi vijana, aliye na uwezo wa kuoa aoe. Kufanya hivyo kutamsaidia kuinamisha macho yake chini na kuwa mtii. Na utii ni sehemu ya imani.”-Mtume Mohammad. Mifano inatosha? Ongezea kidogo na huu: “Adam akasema, sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu basi ataitwa mwanamke…Kwa hiyo mwanaume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe nao watakuwa mwili mmoja.”
MAANA YA MIFANO
Nimetoa mifano hiyo makusudi ili kukukumbusha kwamba mwanaume ana nafasi gani kwa mwanamke, na ikuamshe kuwasoma wanaume wanataka kale ‘kaheshima’ ka kutangulia. Wanawake wengi wamekuwa wakilia, wana kiu ya kuolewa lakini bahati mbaya wanajikuta hawaolewi. Wanalazimisha lakini wapi, mambo yanakuwa yaleyale kila uchao. Rafiki yangu, hakuna sababu ya kutafuta mchawi.
Haihitaji kwenda kwa mganga kusafisha nyota, kikubwa unachopaswa kufanya ni kutathimini ndoa kwa upana wake. Jifunze kupitia wenzako walioolewa. Jiulize wana kitu gani cha ziada? Wanaowaoa wanavutiwa na nini? Wanaume ni watu wa aina gani? Leo nitakumegea siri. Pamoja na kwamba wanaume wanapaswa kuwaheshimu wanawake lakini asikwambie mtu, wanaume wanapenda zaidi kuheshimiwa.
Mwanaume anapenda kuibeba dhana ya ‘kichwa cha familia’ kwa mikono miwili hivyo ukitaka kumpatia, mpe hiyo nafasi kwa asilimia mia moja uone ‘balaa’ lake. Halafu, kwani kuna ubaya gani ukimzidishia dhana hiyo ya kichwa cha familia hata kama ni mara kumi zaidi? Utajiongezea sifa ya ziada.
Mwanaume anahitaji kuwa na mwanamke ambaye atamsikiliza. Atamheshimu, atampa thamani ya mume katika ndoa yake.
JIFUNZE KWA WALIOTULIA
Ruhusu akili yako ijifunze. Kubali akili yako ikosolewe kupitia wale unaowaona wametulia kwenye ndoa zao kwa miaka mingi. Ukifuatilia kwa undani utabaini wana kitu cha ziada. Mke ana hulka ya kike. Kuwa na haiba ya kike. Amchukulie mwanaume kama kichwa cha familia, hapo mwanaume hapindui. Atakuwa wako daima. Mke anapaswa kuwa mvumilivu. Awe na hekima ya kumsaidia mume. Kuzungumza naye kwa staha. Siyo mwanamke unazungumza na mwanaume kama vile unamsuta, unategemea nini? Mwanamke anaongea maneno machache kwa mumewe, zaidi anakuwa msikilizaji. Hata kama ni kukosoa, anamkosoa mumewe kwa staha.
Mwanamke ukibeba sifa hizo nilizoziainisha, mwanaume lazima akuheshimu. Akupe kipaumbele na ndiyo maana kuna baadhi ya wanaume hawajatulia lakini huwaambii kitu kwa wake zao. Wanatambua thamani ya upole, uvumilivu, busara na hekima kutoka kwa wake zao. Hawako tayari kuipoteza hata iweje. Watahangaika na dunia lakini mwisho wa siku wanafunga breki kwa wake zao.
Wanawake wenye sifa hizo ndiyo wanaopendwa na wanaume. Jitahidi kuwa kama wao. Wewe shughulikia hayo mengine muachie Mungu muweza wa yote atakukirimia.
NIAMINI MIMI Mungu huwa hakosei. Ukiwa na sifa hizo, ukamtegemea yeye, utamtuliza mwanaume hata kama alikuwa na tabia ya kurukaruka. Tukutane wiki ijayo! Tunaweza kubadilishana mawazo kupitia kurasa zangu za Facebook, Twitter na Instagram, napatikana kwa jina la Erick Evarist.
Post a Comment