KUTANA NA ISABELA, BILIONEA NAMBA MOJA BARANI AFRIKA ALIYEAMUA KUINGIA KWENYE SOKA
Na Saleh Ally
HAKUNA
ubishi kuwa hapa nyumbani mchezo maarufu zaidi ni soka. Lakini duniani
kote, soka ndiyo mchezo wenye mashabiki wengi zaidi tena kwa kiwango
kikubwa cha asilimia nyingi.
Wafanyabiashara watatu wakubwa ndiyo wameamua kuwekeza katika soka na mabadiliko yamekuwa yakionekana hata kama si sehemu zote.
Said Bakhresa, yeye ameamua kuanzisha timu yake ya Azam FC. Imekuwa na
mafanikio makubwa kwa muda mfupi ingawa haijaweza kuwashawishi mashabiki
sana kama ilivyo kwa wakongwe, Yanga na Simba.
Yusuf
Manji, bilionea ambaye amekuwa hataki kuonekana au kujitangaza sana kwa
maana ya utajiri, yeye alikuwa tayari kuwekeza Yanga kwa njia ya
kukodisha lakini inaonekana kumekuwa na figisu, jambo linaloonekana
kuikwamisha Yanga na kuifanya iingie katika mwendo wa kusuasua.
Wakati
Yanga bado hawajajua kipi ndiyo au hapana, Simba wapo kwenye mchakato
wa kukubali Sh bilioni 20, ofa kutoka kwa bilionea kijana zaidi barani
Afrika Mohammed Dewji ambaye utajiri wake unafikia dola bilioni 1.4
(zaidi ya Sh trilioni tatu).
Mo Dewji anataka kununua hisa za Simba kwa asilimia 51 ili kuanza kuiendesha kwa nafasi na kuhakikisha kunakuwa na mabadiliko.
Wakati
mabilionea hao wa Tanzania wameingia katika soka, upande wa Angola,
mwanamama tajiri zaidi nchini humo na tajiri zaidi kuliko wanawake wote
barani Afrika, Isabela dos Santos, yeye amechaguliwa kuwa rais wa klabu
kongwe ya Petro Luanda, hali ambayo inaonyesha wazi sasa ameamua kuingia
kwenye soka.
Utajiri
wa Isabela ni dola bilioni 3.3 (zaidi ya Sh trilioni 7). Kumbuka
mwanamama huyu mwenye watoto watatu ni mtoto wa Rais Jose Eduardo dos
Santos wa Angola.
Lakini
ni mke wa Sindika Dokolo, bilionea kutoka DR Congo, pia ni mtoto wa
bilionea wa miaka nenda rudi wa nchini humo. Wawili hao walikutana
wakiwa shule barani Ulaya ambako walianzisha uhusiano wa kimapenzi.
Klabu
ya Petro de Luanda ilianzishwa mwaka 1980 na kupata mafanikio makubwa
baadaye. Lakini miaka ya kuanzia 2000, ilianza kudorora na sasa Isabela
anakuwa kama mkombozi. Ushindi wake wa cheo cha rais, bila shaka ni kama
ukombozi kwa mashabiki wa klabu hiyo kwa kuwa wanajua Isabela ni
mwanamama wa chuma ambaye hatakubali kuendesha kitu kinachodorora.
Isabela
ni injinia kitaalamu. Lakini amekuwa mfanyabiashara aliyejijenga katika
mafuta, madini hasa almasi lakini barani Ulaya hasa Ureno na Hispania
amewekeza katika makampuni makubwa ya simu ambako anaingiza kiwango
kikubwa cha fedha.
Lakini hivi karibuni kajiingiza kwenye biashara ya saruji na ameanza umiliki wa mabenki, hasa nchini Ureno.
Baadhi
ya wananchi au wanasiasa wapinzani wamekuwa wakipinga kwamba
anapendelewa sana kwa kuwa ni binti wa kwanza wa rais dos Santos, akiwa
ni mtoto wa kwanza wa mkewe wa kwanza.
Mwanamama
huyo ambaye pia ni Rais wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Angola,
anasifika kwa kuwa na tabia ya kutaka ushindi au mafanikio makubwa kwa
kila anachokiongoza.
Kabla
aliwahi kuwekeza nchini Marekani katika mpira wa magongo. Lakini baada
ya kushinda katika uchaguzi na kuwa Rais wa Petro de Luanda, alisisitiza
anataka kuona timu hiyo inakuwa kubwa zaidi barani Afrika.
Isabela anasema fedha ni suala linalotokana na ubunifu na uwezo wa uamuzi hasa katika uchapaji kazi.
Amesisitiza,
kama Waangola na hasa watu wa Klabu ya Petro de Luanda wanaamua kwa
kushirikiana naye bega kwa bega, basi hakuna anayeweza kuizuia klabu
hiyo kurudisha sifa yake na kuwa kubwa sana.
Kwa
mashabiki wa Petro de Luanda ni faraja upya, lakini hofu kubwa ni kwa
mashabiki wa timu nyingine. Kwamba fedha za Isabela na kwa kuwa ndiye
binti kipenzi wa Rais wa Angola ambaye amekaa madarakani tokea mwishoni
mwa miaka ya 1980, huenda upendeleo unaweza kuwa wazi.
Wengi
wanaamini hata waamuzi, viongozi wa Shirikisho la Soka la Angola,
watakuwa waoga na kuipa nafasi Petro de Luanda kufanya vizuri hata
isipostahili.
Utaona,
kuingia kwa bilionea huyo namba moja kwa upande wa wanawake Angola na
Afrika nzima, kumewagawanya wengi. Wapo walio na faraja kuu na wengine
hofu hasa ya haki, imetawala.
Isabela
kasisitiza kwamba mafanikio ndani ya Angola ni namba moja lakini
anachotaka yeye ni Petro de Luanda kuwa klabu kubwa zaidi Afrika na
angependa kuona inazipa shida kubwa timu kubwa kutoka Afrika Kaskazini,
Magharibi na ikiwezekana zile za Afrika Kusini huku akiitaja Mamelodi
Sundowns ambayo pia iliwahi kuwa na rais mwanamama.
Isabela
anaishi kwenye nyumba ya kifahari ambayo inaaminika ni ghali zaidi
kuliko Ikulu ya Angola ambayo inaongozwa na baba yake mzazi. Lakini si
rahisi kuipiga picha kutokana na ulinzi mkali.
Anamiliki
boti ya kisasa, ndege mbili kwa ajili yake na magari zaidi ya 12 ya
kifahari likiwemo aina ya Maybach Exelero lenye thamani ya dola 250,000
(zaidi ya Sh milioni 544) ambalo wengi waliamini ni la kisela na si kwa
mtu kama yeye.
Kwa
kuwa ana umri wa miaka 43, Isabela amekuwa haoni shida ‘kujiachia’ na
msisitizo wake ni kwamba yeye ni mama kijana anayehitaji kuishi
anavyoamini anataka.
Lakini
amekuwa akisisitiza kuwa, sasa furaha yake ni soka na anaamini
uwekezaji wake katika mchezo huo utakuwa sawa na ilivyo kuwekeza katika
madini au zaidi.
Hakuna
aliyepinga kuingia kwake katika uwekezaji. Wengi wanajua si mpenzi sana
wa soka au haujui vizuri. Lakini wanaamini kwa kuwa ni mfanyabiashara,
atasaidia kupatikana kwa mabadiliko kwa kuwa anajua ili kufanya biashara
vizuri katika soka, basi lazima timu inayotaka kufanya vizuri ishinde
na kupata makombe.
Isabela
anataka makombe yamsaidie kupata biashara. Hivyo lazima atahakikisha
Petro de Luanda inaamka na kuwa bora zaidi ya sasa na kumsaidia kupata
na kufanya biashara ya uhakika.


Post a Comment