Sababu Zilizowafanya Wazee wa Baraza Wamtie Hatiani Lulu Michael

Wazee
wa baraza wameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa mwigizaji
wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu Lulu amehusika kumuua bila
kukusudia msanii mwenzake, Steven Kanumba.
Wakitoa
maoni yao jana baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, wazee
hao walieleza kuwa Lulu ndiye aliyesababisha kifo cha mpenzi wake huyo
wakati wa ugomvi baina yao usiku wa Aprili 7, 2012.
Wakizungumza
mmoja baada ya mwingine, wazee Omary Panzi, Sarah Lugoma na Rajabu
Mlawa, walihusisha tukio la Kanumba kujibamiza kichwa ukutani na
kusukumwa na mshtakiwa.
“Kutokana
na sababu na uainishi wa kesi (ushahidi) wa pande zote, mimi kwa upande
wangu nimeridhika kuwa Elizabeth (Lulu) ameua bila kukusudia,” alisema
mzee Mlawa na kuongeza: “Katika ugomvi, inawezekana hekaheka za
kujinusuru, alitumia nguvu kumsukuma Kanumba na kuanguka ukutani. Hivyo,
kwa maoni yangu kosa la kuua bila kukusudia kwa Elizabeth
limethibitika.”
Akitoa
maoni yake, Sarah Lugoma alisema Kanumba alifariki dunia kutokana na
ugomvi baina yake na mpenzi wake (Lulu) kwa kuwa ndani kulikuwa giza,
Kanumba aliteleza wakati wa ugomvi huo akaanguka.
“Hivyo mshtakiwa aliua bila kukusudia,” alisisitiza Lugoma wakati akihitimisha maoni yake.
Mzee
mwingine, Panzi alisema Kanumba aliteleza na kuanguka wakati wa ugomvi
huo, mshtakiwa ndiye aliyehusika na kifo chake kwa kuua bila kukusudia.
Hata
hivyo, maoni ya wazee hao wa baraza siyo hukumu halisi ya Mahakama bali
yanayotokana na mtazamo wao tu katika hali ya kawaida nje ya sheria kwa
namna walivyousikiliza ushahidi wa pande zote.
Hivyo,
kumtia hatiani mshtakiwa huyo hakumaanishi kuwa tayari ana hatia kwa
kuwa maoni hayo hayamfungi jaji katika hukumu yake ambaye huongozwa na
sheria husika.
Kwa
hiyo, hatima ya msanii huyo kama ana hatia au la itabainishwa na
Mahakama Novemba 13 wakati Jaji Sam Rumanyika anayesikiliza kesi hiyo
atakapotoa hukumu.
Jaji Rumanyika aliwakumbusha wazee hao muhtasari wa ushahidi uliotolewa na pande zote kabla ya kutoa maoni yao.
Jaji
Rumanyika akieleza kwa ufupi kilichozungumzwa na kila shahidi wa pande
zote, alitoa mwongozo kwa wazee hao pamoja na mambo mengine, kutoa maoni
yao bila kuongozwa na huruma wala kuogopa chochote.
“Mnalo
jukumu la kutoa maoni yenu bila kuongozwa na huruma wala vitisho.
Mnatakiwa kutoa maoni yenu kwa mujibu wa ushahidi mliousikia,” alisema
Jaji Rumanyika.
Aliwaeleza
kuwa kama walivyosikia ushahidi wa upande wa mashtaka kuwa umejikita
kwenye ushahidi wa kimazingira, mshtakiwa ndiye aliyekuwa mtu wa mwisho
kuwa na Kanumba.
Alisema
ushahidi wa kimazingira lazima uwe ni vipande ambavyo ni mnyororo
(muunganiko) unaomhusisha mshtakiwa kuwa ndiye ametenda kosa.
“Kama
mkiona kuwa mshtakiwa ametoa maelezo ya kutosheleza basi mnaweza kusema
hana hatia, lakini kama mna maoni tofauti pia mtaniambia,” alisema Jaji
Rumanyika na kuongeza:
“Mkiona
kuwa kifo hicho kilitokana na ugomvi, basi shtaka lake huwa ni la kuua
bila kukusudia, mkishawishika kwa vyovyote na kwa namna yoyote ile
mshtakiwa hakuhusika na kifo hiki msisite pia kunipa maoni yenu.”
Post a Comment